Home » News and Events » “Karibu nyumbani STAMICO Dkt. Venance Mwasse”

“Karibu nyumbani STAMICO Dkt. Venance Mwasse”

IMG_6558-1024x862B

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt. Venance Mwasse (Kulia) akisalimiana na Wafanyakazi mara ya baada ya kuwasili katika ofisi za makao makuu ya Shirika hilo zilizopo Upanga, Dar es Salaam

STAMICO yampokea kwa furaha Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wake mpya Dkt. Venance Mwasse katika ofisi za makao makuu zilizopo Upanga jijini Dar es Salaam mnamo tarehe 8 mwezi wa kumi na moja mwaka 2019.

Dkt. Mwasse amepokelewa kwa hafla fupi wakati amewasili rasmi ofisini hapo kuanza kazi baada ya uteuzi wake uliofanywa na Wizara ya Madini.

Akiongea na wafanyakazi wa STAMICO katika hafla hiyo Dkt. Mwasse ambaye alishawahi kufanya kazi katika kampuni tanzu ya STAMICO ya STAMIGOLD Biharamulo Mine (SBM), ametumia nafasi hiyo kumshukuru Mwenyezi Mungu na Wizara ya Madini kwa uteuzi huo na pia Wafanyakazi wa STAMICO kwa ujumla kwa mapokezi yao mazuri.

Dkt. Mwasse amesema dhamira yake ni kuona STAMICO inasimama na kufikia malengo hivyo ameahidi kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha Shirika linapata nyenzo zitakazo liwezesha kuendesha miradi yake na kufikia malengo iliyojiwekea kwa manufaa ya Wananchi na Taifa kwa ujumla.

Aidha, amewataka Wafanyakazi kushirikiana kwa kuwa  ushirikiano ni kitu muhimu katika kuhakikisha Shirika linasonga mbele, na ameifananisha STAMICO na timu ya mpira ambapo wachezaji wanatakiwa kushirkiana ili kuiwezesha timu yao kupata ushindi.

IMG_6694

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt. Venance Mwasse (pichani kushoto) akiongea na wafanyakazi baada ya kupokelewa katika ofisi za STAMICO

“kama kiungo mchezeshaji nitahakikisha natengeneza mazingira mazuri yatayowawezesha wachezaji (watumishi) kupeleka mpira golini, hivyo basi ni jukumu letu sote kushirikiana na kuhakikisha STAMICO inafikia malengo yake iliyojiwekea” alisisitiza Dkt. Mwasse.

Akiongea wakati akimkaribisha katika familia ya Wana-STAMICO, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala Bw. Deusdedith Magala amempongeza  na kumkaribisha Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Mwasse ambapo alimwelezea jinsi wafanyakazi walivyokuwa na imani kwa uongozi mpya katika kuhakikisha Shirika hili linapaa.

Wafanyakazi wakimsilikiliza kwa makini Dkt. Mwasse wakati akitoa nasaha zake mara baada ya kukaribishwa STAMICO

Aidha, kwa upande wa wafanyakazi Bw. Hamis Mdoe  amesema amefurahishwa sana na uteuzi huo, kwa kuwa Dkt. Mwasse alishawahi kufanya kazi na STAMICO akiwa Kaimu Meneja wa STAMIGOLD hivyo ni mtu anayelifahamu Shirika vizuri na ni matarajio yao  kupata mafanikio kupitia uongozi wake.

Kabla ya uteuzi huo Dkt Mwasse alikuwa Tume ya Madini akiwa Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini akitokea  kampuni tanzu ya STAMICO iitwayo STAMIGOLD, ambako alikuwa Kaimu Meneja Mkuu kuanzia Disemba 2017 hadi Disemba 2018.

Aidha, ameshawahi kufanya kazi kwa ukaribu na STAMICO wakati akiwa Mkurugenzi wa Ukaguzi wa iliyokuwa Wakala ya Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), hivyo analifahamu Shirika kwa mapana yake.


MWISHO

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 

Copyright © 2020 State Mining Corporation. All Rights Reserved.