Home » News and Events » Katibu Mkuu “MEM” azindua Bodi ya Wakurugenzi STAMICO

Katibu Mkuu “MEM” azindua Bodi ya Wakurugenzi STAMICO

Katibu Mkuu: Bodi mna kazi kubwa ya kufanya ili STAMICO ifikie malengo

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Prof. Justus Ntalikwa amezindua Bodi mpya ya Wakurugenzi ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), kwenye ukumbi wa Mikutano STAMICO Jijini Dar es Salaam leo na kuikabidhi bodi hiyo vitendea kazi huku akiwaelekeza kuwa kazi ya kwanza ni kukamilisha safu ya uongozi wa juu wa Shirika wakianzia na nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika.

Kabla ya kuzindua rasmi Bodi hiyo iliyoteuliwa na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo, Katibu Mkuu aliwaambia wajumbe wa bodi kuwa Waziri anaimani na nao na kwamba usimamizi wao kwenye shirika hili utapelekea kufikia malengo na matarajio ya serikali.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Prof. Justus Ntalikwa katikati walio kaa akiwa na Wajumbe wa Bodi ya STAMICO na Viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini mara baada ya kuzinduliwa kwa Bodi hiyo makao makuu ya STAMICO Jijini Dar es Salaam. Wengine ni kutoka kushoto walio kaa, Mwenyekiti wa Bodi Balozi Alexender Muganda, Naibu Katibu Mkuu anae shughulikia Madini Prof. James Mdoe, Kaimu Kamishna wa Madini Mha. Ally Samaje, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Bi. Zena Kongoi, waliosimama kushoto ni Bw. Abdalah Mussa, Dkt. Coretha Komba, Dkt. Lightness Mnzava na Bw. Felix Maagi

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Prof. Justus Ntalikwa katikati walio kaa akiwa na Wajumbe wa Bodi ya STAMICO na Viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini mara baada ya kuzinduliwa kwa Bodi hiyo makao makuu ya STAMICO Jijini Dar es Salaam. Wengine ni kutoka kushoto walio kaa, Mwenyekiti wa Bodi Balozi Alexender Muganda, Naibu Katibu Mkuu anae shughulikia Madini Prof. James Mdoe, Kaimu Kamishna wa Madini Mha. Ally Samaje, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Bi. Zena Kongoi, waliosimama kushoto ni Bw. Abdalah Mussa, Dkt. Coretha Komba, Dkt. Lightness Mnzava na Bw. Felix Maagi

“Wizara ina imani na matarajio makubwa na Bodi hii katika kusimamia ipasavyo shughuli za Shirika ili kutimiza malengo ya uanzishwaji wake katika Sekta ya Madini. Bodi inalo jukumu kubwa la kuhakikisha miradi yote iliyo chini ya STAMICO inaendelezwa na kusimamiwa ipasavyo ili kuiletea Serikali manufaa ikiwemo gawio katika migodi ya ubia” alisema Katibu Mkuu Prof. Ntalikwa.

Aidha Katibu Mkuu aliwaambia wajumbe wa Bodi kuwa wanayo kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha Shirika hilo linasimama na kuwa mhimiri wa uchumi wa Taifa kwani nchi ina raslimali nyingi za madini. Aliwaomba wajumbe kupitia Sera na Sheria ya Madini 2010 kama miongozo na kwamba mtazamo wao uwe unalenga Shirika kujiendesha lenyewe kwa siku za usoni na liwe na mwenendo wa kibiashara.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini (Madini) Prof. James Mdoe  aliyeambatana na Katibu Mkuu kwenye uzinduzi huo wa bodi, awali aliwaambia wajumbe wa Bodi kuwa yeye amepewa dhama ya kusimamia eneo la Madini na kwamba uwepo wa Bodi hiyo unampa faraja kwa kuwa ni dhamira yake kuona STAMICO inakuwa kama mashirika mengine ya Umma kwenye mataifa ya wezentu ambapo ushikilia uchumi wa taifa husika.

“Naiomba Bodi tushirikiane kuhakikisha Shirika linatekeleza majukumu yake kikamilifu na kuleta tija kwa Taifa” alisema Prof. Mdoe.

Mara baada ya Bodi hiyo kuzinduliwa rasmi, Mwenyekiti wa Bodi hiyo Balozi Alexander Muganda alipata fursa ya kuongea kwa niaba ya Bodi hiyo mpya. Balozi Muganda alimshukuru Waziri kwa kuonesha imani kwa wajumbe wa Bodi kwa kuwateuwa na kwamba amepokea maelekezo yote na ameahidi kuyatekeleza.

“Ndugu Mgeni wa heshima awali ya yote kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi uliyoizindua muda mfupi uliopita nakushukuru kwa kutuamini kulisimamia Shirika hili. Naomba niseme kwamba nimepokea maelekezo yote na niseme sio maelekezo bali maagizo yaliyotolewa na kwamba kilicho baki kwetu ni utekelezaji wa maagizo hayo, naomba kukuahidi kuwa tutatekeleza” Alisema Balozi Muganda.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Prof. Justus Ntalikwa katikati akiongoza tukio la uzinduzi wa Bodi mpya ya wakurungezi wa Shirika la Madini la Taifa kwenye ukumbi wa mikutano STAMICO Jijini Dar es Salaam leo tarehe 02/06/2016

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Prof. Justus Ntalikwa katikati akiongoza tukio la uzinduzi wa Bodi mpya ya wakurungezi wa Shirika la Madini la Taifa kwenye ukumbi wa mikutano STAMICO Jijini Dar es Salaam leo tarehe 02/06/2016

Awali Kaimu Mkurugenzi Mtendji wa STAMICO Bi. Zena Kongoi aliwakaribisha wageni na kusema tukio la uzinduzi wa Bodi hiyo lilikuwa linasubiriwa kwa hamu kubwa na Menejimenti na watumishi wote wa STAMICO hivyo wamejawa na furaha kubwa.

Miongoni mwa Miradi ambayo STAMICO inamiliki ni, Miradi ya ubia ni pamoja na ule wa TanzaniteOne unaomilikiwa kwa 50/50%,  Mgodi wa Dhahabu wa Buckreef  kati ya TANZAM2000 55% na STAMICO 45%, Mgodi wa Dhahabu wa STAMIGOLD Biharamulo Mine, Mgodi wa Dhahabu Buhemba, Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira, na Mradi wa Ununuzi wa Madini ya Bati Kyerwa yote ikiwa inamilikiwa kwa 100% na STAMICO, pia inamiliki leseni za utafutaji wa madini zipatazo 49.

Pamoja na uwepo wa miradi hiyo sambamba  na lesseni za utafutaji wa madini Menejimenti ya STAMICO inaendelea na ubunifu wa miradi mbalimbali mipya ukiwemo  mradi mkubwa wa uzalishaji wa Kokoto unaotarajiwa kuanza mara baada ya hatua zote kukamilika.

 ================MWISHO===============

Imeandaliwa na:

Issa Mtuwa
Afisa Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma,
Shirika la Madini la Taifa,
Plot 417/418, Barabara ya Umoja wa Mataifa, Upanga,
S.L.P 4958,
Dar es Salaam.
Simu: +255-22-2150029, 
Barua Pepe: info@stamico.co.tz
Tovuti: http://www.stamico.co.tz
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 

Copyright © 2018 State Mining Corporation. All Rights Reserved.