Home » News and Events » STAMICO kutumia mradi wa Makaa ya Mawe- Kabulo kuchangia ukuaji wa viwanda nchini

STAMICO kutumia mradi wa Makaa ya Mawe- Kabulo kuchangia ukuaji wa viwanda nchini

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) linafanya jitihada za kuuendesha Mgodi wa Makaa ya Mawe-Kabulo Kisasa zaidi ili kukuza uzalishaji na kuchangia juhudi za Serikali za kuifikisha Tanzania kuwa nchi ya viwanda na yenye uchumi wa kati.

Wasimamizi wa Mradi wa Makaa ya Mawe wakiongozwa na Kaimu Mneja Mkuu wa Mgodi wa Kiwira Bwana Aswile Mapamba (wa kwanza kushoto) wakitoa maelezo ya kitaalamu kuhusu Mradi huo kwa Kamishna wa Madini Mhandisi Benjamin Mchwampaka (wa pili kutoka kulia). Kulia kwa Kamisha Mchwampaka ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya STAMICO Mhandisi Said Mkwawa.

Kaimu Mratibu wa Mradi wa Makaa ya Mawe-Kabulo Mhandisi Alphonce Bikulamchi (wa pili kutoka kulia) akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi kwa Kamishna wa Madini wa Wizara ya Nishati na Madini (MEM) Mhandisi Benjamin Mchwampaka (wa tatu kutoka kulia) alipoutembelea mradi huo hivi karibuni. Anayefuatilia taarifa ya utekelezaji (aliyesimama katikati) ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya STAMICO Mhandisi Said Mkwawa.

 

 

Mratibu wa Mradi wa Uchimbaji Makaa ya Mawe-Kabulo- Mjiolojia Alex Rutagwelela amebainisha hayo katika mahojiano maalum na Mwandishi wa Habari hii kuhusu maendeleo ya mradi huo ambao ulianza rasmi Aprili 30, 2017.

Rutagwelela amesema uendeshaji wa Mgodi wa Kabulo katika mfumo wa kisasa zaidi utaliwezesha Shirika kukuza kiwango cha uzalishaji makaa hayo, kupanua wigo wa masoko na kuongeza mapato kwa Shirika.

Amesema kwa sasa STAMICO inaimarisha barabara inayoelekea eneo la uchimbaji madini la Kabulo, ambayo iliharibiwa vibaya na mvua zilizonyesha hivi karibuni; huku ikikamilisha ukarabati wa maabara ya kupima sampuli za makaa ya mawe kwa ajili ya upimaji viwango vya makaa yatakayouzwa katika soko.

Rutagwelela amesema kwa kuanzia Shirika linachimba tani tani 300 hadi 400 za Makaa ya Mawe kwa siku, ambapo kwa mwezi linatarajia kuchimba tani 6,000 hadi 9,000 kwa kuanzia.

“kiwango cha uchimbaji wa makaa ya mawe kwa mwezi kinatarajiwa kuongezeka sambamba na ongezeko la mitambo ya uzalishaji kwa mwezi na mahitaji ya watumiaji” Alifafanua Mjiolojia Rutagwelela.

Kaimu Mratibu wa Mradi wa Makaa ya Mawe-Kabulo Mhandisi Alphonce Bikulamchi (wa pili kutoka kulia) akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi kwa Kamishna wa Madini wa Wizara ya Nishati na Madini (MEM) Mhandisi Benjamin Mchwampaka (wa tatu kutoka kulia) alipoutembelea mradi huo hivi karibuni. Anayefuatilia taarifa ya utekelezaji (aliyesimama katikati) ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya STAMICO Mhandisi Said Mkwawa.

Msimamizi wa Mradi wa Makaa ya Mawe Mhandisi Alphonce Bikulamchi akitoa maelezo ya kitaalamu kuhusu Mradi huo kwa Kamishna wa Madini Mhandisi Benjamin Mchwampaka (wa pili kutoka kulia). Kulia kwa Kamisha Mchwampaka ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya STAMICO Mhandisi Said Mkwawa.

Awamu ya kwanza ya Mradi wa uchimbaji makaa ya mawe inatekelezwa kupitia leseni zake mbili za uchimbaji mdogo wa madini Primary Mining Licences (PMLs) zilizopo ndani ya leseni ya utafiti ya Kabulo zenye ukubwa wa Hecta 16.52.

Leseni hizo mbili za Uchimbaji wa Awali wa Madini katika eneo hilo la Kabulo zina tani  zipatazo 241,865 za mashapo ya makaa ya mawe yaliyoko karibu na uso wa ardhi ambayo yanaruhusu Uchimbaji wa Mgodi wa Wazi (Open pit mining) kuendelea kufanyika.

Makaa ya mawe hutumika kama moja ya vyanzo vya Nishati katika shughuli za uzalishaji viwandani hususan viwanda vya Saruji.

Inakadiriwa kuwa mahitaji ya jumla ya Makaa ya Mawe katika viwanda vya Saruji nchini ni tani 389,000 kwa mwaka.

 

 

 

============================================MWISHO===============================================

Imeandaliwa na:

Koleta Njelekela
Meneja Masoko na Mawasiliano kwa Umma,
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO),
S.L.P 4958,
Dar es Salaam.
Simu: +255-22-2150029, 
Barua Pepe: info@stamico.co.tz
Tovuti: http://www.stamico.co.tz
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 

Copyright © 2018 State Mining Corporation. All Rights Reserved.