Home » News and Events » Nina imani na Bodi Mpya ya STAMICO – Waziri Biteko

Nina imani na Bodi Mpya ya STAMICO – Waziri Biteko

Na Issa Mtuwa-STAMICO

Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko amezindua Bodi mpya ya Wakurugenzi ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) huku akielezea imani na matumaini yake kwa bodi hiyo katika kuisimamia STAMICO ili itekeleze majukumu yake katika ufanisi mkubwa na tija kwa Taifa.

Waziri wa Madini, Mhe. Doto Biteko akiongea wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi mpya ya STAMICO, hafla iliyowakutanisha Menejimenti ya STAMICO, Wajumbe wa Bodi na Viongozi Waandamizi wa Wizara ya Madini. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Madini Mhe. Stanslaus Nyongo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu, Bw. Issa Nchasi. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Bodi Generali (Mstaafu) Michael Joseph Isamuhyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Kanali Mhandisi Sylivester Ghuliku.

Waziri Biteko ameyasema hayo jijini Dar es salaam katika hafla ya uzinduzi wa Bodi hiyo iliyofanyika katika ofisi za Makao Makuu ya STAMICO, ambapo pia alikabidhi vitendea kazi kwa Mwenyekiti mpya wa Bodi ya STAMICO Meja Jenerali (Mstaafu) Michael Joseph Isamuhyo pamoja na wajumbe wa Bodi hiyo.

“ Nina imani kubwa sana na ninyi katika kulisimamia Shirika hili, nendeni mkabadilishe taswira ya Shirika. Mhe. Rais aliniambia yule afande (Mwenyekiti wa Bodi) atakwenda kufanya kazi, na ninyi niliowateuwa mimi nina imani kubwa na ninyi; shirikianeni mhakikishe STAMICO inatakeleza majukumu yake ipasavyo na hatimaye ipeleke gawio Serikalini ifikapo Juni 2019” Alisisitiza Mhe. Biteko.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya STAMICO, Meja Jenerali (Mstaafu) Michael Joseph Isamuhyo akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko baada ya kuzindua Bodi hiyo na kuwakabidhi vitendea kazi.

Amesema tangu kuanzishwa kwa STAMICO muda mrefu uliopita, haijawahi kupeleka gawio Serikalini, hivyo Bodi hiyo mpya inawajibu wa kuhakikisha kuwa STAMICO inazalisha kwa faida na kupeleka gawio Serikalini.

“Tumieni mamlaka mliyopewa ya kulisimamia Shirika hili, mkiwa na lengo la kuifanya STAMICO kuwa Shirika tegemeo kwa kupeleka gawio Serikalini” alibainisha Mhe. Biteko

Waziri huyo wa Madini ameihakikishia Bodi hiyo kuwa Wizara yake itatoa ushirikiano mkubwa kwa Bodi na Shirika na kwamba ataendelea kutupia jicho lake kwa STAMICO na kuchukua hatua stahiki za maboresho endapo atabaini vitu vinakwenda hovyo hovyo.

Naibu Waziri wa Madini Mhe. Stanslaus Nyongo akiongea kwenye hafla ya uzinduzi wa Bodi mpya ya STAMICO uliofanyika Makao Makuu ya STAMICO jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Madini Mhe. Stanslaus Nyongo akiongea kwenye hafla ya uzinduzi wa Bodi mpya ya STAMICO uliofanyika Makao Makuu ya STAMICO jijini Dar es Salaam

Aidha, Mhe. Biteko ameipongeza STAMICO kwa hatua nzuri iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi yake, hususani Mradi wa Makaa ya Mawe wa Kabulo-Kiwira kwani  hatua hiyo inaashiria dalili njema sambamba na mipango madhubuti inayoonesha muelekeo mzuri na mpya wa uendeshaji wa Shirika hilo.

Kauli hiyo ya pongezi ilitokana na taarifa fupi ya utekelezaji wa miradi ya Shirika iliyosomwa awali na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Kanali  Mhandisi Sylvester Ghuliku.

Mhe. Biteko ameiagiza Bodi ya STAMICO kufuatilia hisa za Kampuni Tanzu ya STAMICO ijulikanayo kama Tanzania Gemstone Industry Ltd (TGI) ambayo iliingia ubia wa 50:50 na Kampuni ya Tan Rubi & Gemstone Co. Ltd  kufanya shughuli za uchimbaji katika eneo la Mundarara, lililopo Wilaya ya Longido  mkoani Arusha.

“Naelekeza pamoja na mipango yenu yote, nendeni mkashugulikie hisa za Kampuni ya TGI kama nilivyoelezea historia yake, ili tujue tumepoteza kiasi gani na tunakubaliana na mbia tunapata kiasi gani. Niwakumbushe tu,  Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli ni awamu ya utekelezaji wa mambo yote yaliyoshindikana kutekelezwa, kwa hiyo hili mkalifuatilie na liwezekane”. Aliagiza Biteko.

Akitoa neno la shukrani kwa Mhe. Waziri, Mwenyekiti wa Bodi Meja  Jenerali (Mstaafu) Joseph Michael Isamuhyo alimshukuru Mhe. Rais kwa uteuzi huo kwani ameonesha imani kubwa juu yake.

Aidha alimshukuru Mhe.Waziri wa Madini kwa uteuzi wa wajumbe wenye mchanganyiko wa taaluma na weledi kwani mchanganyiko huo utakuza ubunifu na kuleta tija katika  kutekeleza majukumu ya Bodi na kuisimamia STAMICO kikamilifu.

“Mhe. Waziri nikuhakikishie, umesema mengi sana, mimi kama Mwenyekiti na kama ambavyo umetuahidi ushirikiano, nami nakuahidi utekelezaji wa yale uliyoyasema sambamba na miongozo inayotolewa katika kupata mwelekeo mpya wa STAMICO, sina shaka mimi na wenzangu pia tuko tayari” alisema Meja Jenerali Isamuhyo.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Kanali Mhandisi Sylvester Ghuliku akiongea kwa ufupi kuhusu hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya STAMICO muda mfupi kabla ya uzinduzi kufanywa na Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko

==============================MWISHO=============================================

Imeandaliwa na:

Koleta Njelekela

Meneja Masoko na Mawasiliano kwa Umma,

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO),

S.L.P 4958,

Dar es Salaam.

Simu: +255-22-2150029, 

Barua Pepe: info@stamico.co.tz

Tovuti: http://www.stamico.co.tz

Copyright © 2020 State Mining Corporation. All Rights Reserved.