Home » News and Events » Profesa Mdoe amteua Mhandisi John Nayopa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji mpya – STAMICO

Profesa Mdoe amteua Mhandisi John Nayopa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji mpya – STAMICO

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini (MEM) Profesa James Mdoe, amemteua Mhandisi John Nayopa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuanzia tarehe 28 Julai, 2017 ili kuboresha utendaji kazi.

Akihojiwa na Mwandishi wa Habari hii kwa njia ya simu, Profesa Mdoe amesema mabadiliko hayo ya Uongozi-STAMICO yatakuwa chachu ya kuongeza kasi ya kulifufua Shirika na kukuza viwango vya utekelezaji wa miradi ya uchimbaji madini, hatimaye kukuza mapato kwa Shirika na Taifa kwa ujumla.

PICHA 1

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya STAMICO Balozi Alexander Muganda akiwa katika kikao cha kuitaarifu Menejimenti ya STAMICO, kuhusu mabadiliko ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, yaliyofanyika hivi karibuni. Kulia kwake ni Kaimu Mkurugenzi Mpya wa STAMICO Mhandisi John Nayopa na kushoto kwake ni aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo, ambaye atapangiwa kazi nyingine, Bw. Hamis Komba.

“Utekelezaji wa miradi ya STAMICO bado unalegalega. Ni matarajio yangu kuwa Mhandisi Nayopa atachapa kazi ya kulifufua Shirika ili litekeleze majukumu yake kikamilifu kama Shirika mahususi la Madini la Taifa” Alifafanua Profesa Mdoe.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya STAMICO Balozi Alexander Muganda amempongeza Mhandisi Nayopa kwa uteuzi huo, na kumtaka awe mbunifu zaidi katika kuliendesha Shirika Kibiashara na kwa ufanisi mkubwa.

“Fanya maamuzi shirikishi na Menejimenti kutatua changamoto za miradi huku ukishirikisha Wadau na Wizara ya Nishati na Madini katika kuyatafutia ufumbuzi masuala yanayohitaji maamuzi katika ngazi ya Wizara” Alielekeza Balozi Muganda.

Aidha, ameitaka Menejimenti ya STAMICO kufanya mapitio ya miradi ya Shirika na kutengeneza Mpango-Biashara (Business Plan) utakaouzika kwenye taasisi za fedha, ili kufanikisha upatikanaji wa  mitaji kwa ajili ya miradi ya uchimbaji na uendelezaji Wachimbaji wadogo nchini.

Mhandisi Nayopa ambaye alikuwa Afisa Madini Kanda ya Kusini Magharibi, anachukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Bw. Hamis Komba, ambaye pia amekaimu nafasi hiyo kwa miezi saba tu tangu Januari–Julai 2017; atapangiwa kazi nyingine.

Akizungumza katika makabidhiano ya Ofisi, Bw. Komba amempongeza Mhandisi Nayopa kwa uteuzi huo, na ameahidi kumpa ushirikiano katika kutoa ufafanuzi atakaouhitaji kikazi ili kuendeleza kazi nzuri aliyoianza kama vile uzalishaji wa Makaa ya Mawe katika Mgodi wa Kabulo, mkoani Songwe hatua ambayo itamsaidia kusonga mbele katika kuifufua STAMICO.

“Changamoto kubwa inayolikabili Shirika ni kupoteza miradi yake mikubwa iliyobinafsishwa, kama vile Kiwira, Kiwanda cha Mbolea- Minjingu Phosphates, Mgodi wa Pugu Kaolin, Kiwanda cha kukata Almasi-TANCUT, Migodi mikubwa ya Chumvi ya Uvinza na Seasalt Saadani ambayo ilikuwa inalipatia Shirika mapato makubwa yaliyowezesha kujiendesha kibiashara”. Alifafanua Bw. Komba

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji mpya wa STAMICO (anayezungumza mwenye koti jeusi) akifafanua jambo mara baada ya kuripoti katika kituo chake kipya cha kazi katika ofisi za Makao Makuu ya STAMICO, yaliyopo barabara ya Umoja wa Mataifa, Upanga jijini Dar es Salaam. Wengine in aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo, ambaye atapangiwa kazi nyingine, Bw. Hamis Komba (aliyekaa katikati) Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala Bwana Deus Magala.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji mpya wa STAMICO (anayezungumza mwenye koti jeusi) akifafanua jambo mara baada ya kuripoti katika kituo chake kipya cha kazi katika ofisi za Makao Makuu ya STAMICO, yaliyopo barabara ya Umoja wa Mataifa, Upanga jijini Dar es Salaam. Mwingine  ni aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo, ambaye atapangiwa kazi nyingine, Bw. Hamis Komba 

Aidha ameongeza kuwa, STAMICO baada ya kufutwa mwaka 1996 na kukufuliwa upya mwaka 2013/14 inakabiliwa na ukosefu wa mtaji wa TZS Bilioni 50 za kufufua Shirika na kutopata fedha za bajeti ya maendeleo kwa miaka minne mfululizo tangu 2013/14 hadi 2016/17. Shirika pia linakabiliwa na taratibu ngumu za uendeshaji miradi zinazolikwamisha lisiweze kujiendesha kibiashara na kiushindani kwa kasi kubwa.

Hivyo alimshauri Mhandisi Nayopa aendeleze jitihada zilizopo ndani ya Shirika za kutafuta mitaji, zikiwemo kubuni na kutekeleza Mpango-Biashara makini, ili kupata mitaji kutoka taasisi mbalimbali za fedha ndani na nje ya nchi” Alifafanua Bw. Hamis Komba.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji mpya wa STAMICO Mhandisi John Nayopa amemshukuru Naibu Katibu Mkuu- MEM kwa kumuamini na kumteua katika wadhifa huo na amehaidi kutomwangusha katika kutekeleza majukumu ya STAMICO kwa kadiri ya matarajio ya Serikali.

“Natambua mafanikio niliyoyakuta hapa STAMICO katika utekelezaji wa miradi mbalimbali na nitajitahidi kuweka mbele ubunifu zaidi katika kutekeleza miradi ya STAMICO, ili iwe endelevu na yenye tija kwa Shirika na Taifa kwa Ujumla” Alifafanua Mhandisi Nayopa.

Amewataka Menejimenti na Wafanyakazi wa STAMICO kumpa ushirikiano wa kina katika kubaini changamoto za miradi ili kwa pamoja waweze kutafuta fursa ya kuzitatua, badala ya kutegemea fedha ya ruzuku kutoka Serikalini katika kutatua matatizo ya Shirika.

 “ Nitazingatia dhima ya Hapa kazi tu kuboresha utendaji wa Shirika na nitashirkiana na wataalam kuijenga Tanzania yenye Viwanda kupitia bidhaa za madini zinazozalishwa na STAMICO, huku nikitoa kipaumbele katika suala zima la uongezaji thamani ili kuleta tija Viwandani.” Alifafanua Mhandisi Nayopa.

Wajumbe wa Menejimenti ya STAMICO wakiwa katika picha ya pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji mpya wa STAMICO John Nayopa (wa nne kutoka kushoto). Wa kwanza kushoto kwake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya STAMICO Balozi Alexander Muganda na wa pili kulia kwake ni aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo, ambaye atapangiwa kazi nyingine, Bw. Hamis Komba.

Wajumbe wa Menejimenti ya STAMICO wakiwa katika picha ya pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji mpya wa STAMICO John Nayopa (wa nne kutoka kushoto). Wa kwanza kushoto kwake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya STAMICO Balozi Alexander Muganda na wa pili kulia kwake ni aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo, ambaye atapangiwa kazi nyingine, Bw. Hamis Komba.

Amewataka Menejimenti na Wafanyakazi wa STAMICO na Kampuni zake tanzu kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi mkubwa huku wakizingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo katika sekta ya madini na nchi; hatua ambayo itawawezesha kuachana na utendaji kazi wa mazoea na usio na tija.

Bw. Nayopa amesema ataweka mbele mslahi ya Taifa katika kutekeleza majukumu yake na kutatua changamoto zilizopo ikiwa ni pamoja na kutafuta mitaji na kufanya mapitio ya mikataba ya miradi inayotekelezwa na STAMICO na kuiboresha ili inufaishe Shirika na Wawekezaji.

 “hatua hii itaniwezesha kubaini ni miradi gani ya STAMICO iendelezwe na miradi ipi haina tija; ili hatua za haraka za kuifunga miradi hiyo au kuboresha mfumo wake wa uendeshaji ziweze kuchukuliwa”  Alifafanua Mhandisi Nayopa.

Kuhusu suala la uendelezaji Wachimbaji wadogo nchini, Mhandisi Nayopa amewataka wadau kumpa ushirikiano katika kubaini changamoto na mahitaji yao; ili STAMICO kama mlezi wao, iweze kujiongeza katika kubuni mipango ya kuwawezesha kiufundi.

Mhandisi Nayopa ni mtaalam wa madini alyebobea kwa zaidi ya miaka 23 katika sekta ya madini ambaye anafanya kazi kwa kuzingatia mahitaji ya kisheria ya wanataaluma wa madini ikiwemo kusajiliwa katika Bodi ya Usajili wa Wahandisi (Engineers Registration Board-ERB)

Kitaaluma, Mhandisi Nayopa amefanya kazi maeneo mbalimbali yakiwemo kama vile Meneja wa Mradi wa Uendelezaji wa Rasilimali za Madini (SMMRP) unaoratibiwa na MEM; Kamishna Msaidizi sehemu ya Leseni-MEM na Mhandisi wa Migodi-Anglo Gold- Mine hususani katika mgodi wa dhahabu wa Mponeng, nchini Afrika ya Kusini.

 ============================================MWISHO===============================================

Imeandaliwa na:

Koleta Njelekela
Meneja Masoko na Mawasiliano kwa Umma,
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO),
S.L.P 4958,
Dar es Salaam.
Simu: +255-22-2150029, 
Barua Pepe: info@stamico.co.tz
Tovuti: http://www.stamico.co.tz

 

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 

Copyright © 2018 State Mining Corporation. All Rights Reserved.