Home » News and Events » STAMICO washiriki Siku ya Wafanyakazi Duniani, waahidi kuchangia maendeleo ya Viwanda.

STAMICO washiriki Siku ya Wafanyakazi Duniani, waahidi kuchangia maendeleo ya Viwanda.

Wafanyakazi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) leo tarehe  1 Mei, 2017 wameshiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyoadhimishwa kimkoa katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam ambapo waliahidi kuchapa kazi ili kuchangia maendeleo ya Viwanda kupitia miradi ya uchimbaji madini inayotekelezwa na Shirika hilo.

 

Baadhi ya Wafanyakazi wa STAMICO wakijiandaa kuingia uwanja wa uhuru ya kuandamana katika Siku ya Wafanyakazi Duniani kwa mkoa wa Dar es Salaam. STAMICO pia imeshiriki katika siku hiyo katika mkoa wa Dodoma ambapo iliwakilishwa na Wafanyakazi wake wa Idara ya Utafiti na Uchorongaji yenye makao makuu mkoani humo. Aidha STAMICO pia ilishiriki madhimisho ya siku Kitaifa yaliyofanyika mkoani Kilimanjaro ambapo iliwakilishwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodi, Nishati, Ujenzi na Kazi nyinginezo (TAMICO) tawi la STAMICO Makao Makuu Mhandisi Benson Mboya.

Akizungumza mara baada ya kumalizika hafla ya maadhimisho hayo jijini, Makamu Mwenyekiti Chama cha Wafanyakazi wa Migodi, Nishati, Ujenzi na Huduma zingine, tawi la STAMICO (TAMICO) Bwana Denis Silasi, amesema wafanyakazi wa STAMICO ni muhimili mkuu katika kuwezesha viwanda kujiletea maendeleo kwa kupitia miradi mbalimbali ya madini yanayozalisha madini yakiwemo Makaa ya Mawe, Graphite, Tanzanite, Dhahabu, Madini ya viwandani na mengineyo ambayo pia hutumiwa na wenye viwanda katika uzalishaji.

“Kama kauli mbiu inavyoelezea uchumi wa viwanda uendane na kulinda Haki na heshima ya mfanyakazi, TAMICO kwa kushirikiana na Menejimenti ya STAMICO itaendelea kulinda haki za watumishi na kutetea maslahi yao ili kuhakikisha kuwa wanakuwa na motisha ya kufanya kazi wakati wote kwa manufaa na Shirika na Taifa kwa ujumla na hivyo kuiwezesha Tanzania kuwa Tanzania ya Viwanda.” Alifafanua Bwana Silasi.

Amewataka Watumishi wa STAMICO kutumia utaalam, ujuzi na weledi wao katika kutekeleza miradi mbalimbali ya uchimbaji madini inayotekelezwa na Shirika katika maeneo mbalimbali nchini. “Watanzania wanategemea sana ujuzi na utaalam wa watumishi waSTAMICO ili kuboresha hali zao za uchumi kupitia shughuli za uchimbaji madini, hususani katika miradi ambayo inatekelezwa na STAMICO moja kwa moja au ile ya ubia” Alisisitiza Makamu huyo Mwenyekiti wa TAMICOSTAMICO Bwana Silasi.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo kwa mkoa wa Dar es Salaam alikuwa Rais Mstaafu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Bi.Magreth Sitta.

============================================MWISHO===================================================

Imeandaliwa na:

Koleata Njelekela
Meneja Masoko na Mawasiliano kwa Umma,
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO),
S.L.P 4958,
Dar es Salaam.
Simu: +255-22-2150029, 
Barua Pepe: info@stamico.co.tz
Tovuti: http://www.stamico.co.tz
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 

Copyright © 2018 State Mining Corporation. All Rights Reserved.