Home » News and Events » STAMICO yafurahishwa na ziara ya Waziri wa Madini Mhe. Kairuki

STAMICO yafurahishwa na ziara ya Waziri wa Madini Mhe. Kairuki

Karibu Mgeni mwenyeji apone, hivyo ndivyo wanavyoweza kusema wana STAMICO baada ya kutembelewa na Waziri wa Madini Mh. Angellah Kairuki kujionea hali halisi ya Shirika.

  • Waziri wa Madini Mheshimiwa Angellah Kairuki (MB) akizungumza na wafanyakazi wakati wa ziara ya kutembelea Shirika la Madini la Taifa iliyolenga kuboresha miradi na ustawi wa Shirika, tarehe 27 Aprili, 2018 katika ofisi za STAMICO
  • Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Kanali Mhandisi Sylvester Ghuliku akisoma taarifa ya miradi ya Shirika wakati wa kikao cha pamoja na Waziri
  • Mheshimiwa Waziri wa Madini Angellah Kairuki (MB) akitoa maelekezo kwa viongozi wa Shirika kuhusu uboreshaji wa miradi ya STAMICO wakati akipokea taarifa ya miradi ya STAMICO
  • Sehemu ya Watumishi wa STAMICO wakifuatilia maelekezo toka kwa Waziri wa Madini Mhe. Angela Kairuki wakati wa ziara yake.

Katika wiki ya mwisho ya mwezi Aprili Waziri wa Madini Mh. Angellah Kairuki alitembelea Shirika la Madini ili kujadiliana kwa pamoja na watumishi wa Shirika hilo namna  ya kuendeleza miradi mbalimbali itakayoleta tija kwa taifa.

Katika ziara hiyo Mh. Waziri aliongozana na  Naibu Waziri wa Madini Mh. Dotto Biteko na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila.

Ziara hii imeleta mwamko mpya kwa wana STAMICO kwani imetoa nafasi kwa wafanyakazi kufanya majadiliano ya ana kwa ana na viongozi wa juu wa Wizara ya Madini na kutafuta suluhisho la pamoja katika kukabiliana na changamoto katika miradi.

IMG_6599

Wakati wa ziara hiyo Mh. Waziri alipokea taarifa ya uendeshaji wa miradi ya Shirika sambamba na changamoto za miradi kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Kanali Mhandisi Sylvester Ghuliku.

Viongozi hao wa juu kutoka wizarani walitumia muda mrefu STAMICO kujadili namna nzuri ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Shirika. Majadiliano hayo yaliangalia utekelezaji wa mradi, changamoto na mbinu mbalimbali za kuondokana na changamoto hizo.

Alisema ameamua kutembelea STAMICO ili aweze kuifahamu vizuri zaidi miradi yake, kuona changamoto na kutafuta mbinu mbadala za kutatua changamoto zinazolikabili Shirika katika miradi hiyo.

Ameelekeza STAMICO kuangalia jinsi Mashirika ya madini katika mataifa mengine yanavyosimamia miradi yao hususan  ile iliyoko chini ya kampuni tanzu na pia kupata uzoefu kutoka kwa wawekezaji wengine ndani ya nchi ili kuweza kuanza uzalishaji kwa kutumia mtaji mdogo.

Aidha, ameahidi kuongeza nguvu ya kiutendaji pale itakapohitajika ili kuliona Shirika linasonga mbele na linakuwa na manufaa kwa serikali na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wa STAMICO, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Kanali Mhandisi Sylvester Ghuliku amemshukuru Waziri na ujumbe wake kwa nia yake ya dhati aliyoionesha kutaka kuiinua STAMICO na miradi yake.

Pia amefurahishwa na ushirikiano wa hali ya juu wanaoupata kutoka wizarani na kuiomba Wizara kuendelea kutoa ushirikiano wa hali na mali ili kuhakikisha STAMICO inaimarika.

Mh. Waziri ameitembelea STAMICO ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu kuteuliwa kwake na ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu ili kupunguza changamoto za mtaji pamoja na upungufu wa rasilimali watu hasa kwenye ngazi za uongozi ili kurahisisha uendeshaji wa miradi ya Shirika.

========================================MWISHO==================================================

 

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 

Copyright © 2020 State Mining Corporation. All Rights Reserved.