Home » News and Events » STAMICO yakutana na wawakilishi wa vyama vya uchimbaji mdogo wa madini

STAMICO yakutana na wawakilishi wa vyama vya uchimbaji mdogo wa madini

  • Ni hatua ya kutambua changamoto zao ili kuunda mkakati wa pamoja wa kuzitatua.
  • Hatimaye kuwafikisha katika uzalishaji wa madini wenye ufanisi na tija kubwa zaidi unaozingatia usalama na hifadhi ya mazingira salama.

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kama mlezi wa wachimbaji wadogo nchini limekusudia kuimarisha ushiriki wa wadau wa uchimbaji mdogo vikiwemo vyama vya wachimbaji wadogo, katika kubaini changamoto zinazoikabili sekta ndogo ya uchimbaji mdogo ili kuweka mikakati ya pamoja ya utatuzi wa changamoto hizo.

Viongozi wa Wachimbaji Wadogo 52 kutoka mikoa 22 ya Tanzania Bara (FEMATA, REMAS, TAWOMA WIMA na TASPA); Wafanyabiashara wa madini (TAMIDA) pamoja na Maafisa Waandamizi kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mradi wa Uendelezaji Rasilimali za Madini (SMMRP) na STAMICO walishiriki kikao kazi hicho.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Bi. Zena Kongoi (watatu kutoka kulia waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Vyama vya Wachimba Wadogo (FEMATA, REMAS, TAWOMA WIMA na TASPA); Wafanyabiashara wa madini (TAMIDA) pamoja na  Maafisa Waandamizi kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mradi wa Uendelezaji Rasilimali za Madini (SMMRP) na STAMICO waliohudhuria kikao kazi kilichofanyika hivi karibuni STAMICO Makao Makuu Dar es Salaam.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Bi. Zena Kongoi (watatu kutoka kulia waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Vyama vya Wachimba Wadogo (FEMATA, REMAS, TAWOMA WIMA na TASPA); Wafanyabiashara wa madini (TAMIDA) pamoja na Maafisa Waandamizi kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mradi wa Uendelezaji Rasilimali za Madini (SMMRP) na STAMICO waliohudhuria kikao kazi kilichofanyika hivi karibuni STAMICO Makao Makuu Dar es Salaam.

Lengo kuu likiwa ni kuinua na kuendeleza shughuli za uchimbaji mdogo ili ziweze kuleta tija na ufanisi mkubwa kwa jamii na Taifa kwa ujumla huku zikizingatia usalama na uhifadhi wa mazingira.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Bi Zena Kongoi ameyasema hayo hivi karibuni wakati akifunga Kikao kazi cha siku mbili baina ya Shirika hilo na Wadau wa Uchimbaji Mdogo wa Madini nchini, kilichofanyika katika ofisi za Makao Makuu ya STAMICO, zilizopo jijini Dar es Salaam.

Bi. Kongoi amesema STAMICO imeandaa Mwongozo wa Mafunzo ya Kitaalam na Kiufundi kwa wachimbaji wadogo (Technical Training Guidelines for Small Scale Miners) utakaoliwezesha Shirika na wadau wake kutoa mafunzo ya kitaalam kwa wachimbaji wadogo, ili kukuza uelewa na kuongeza ufanisi wa uendeshaji wa miradi ya wachimbaji wadogo nchini.

“Nimefarijika kuona wadau wamekuwa na utayari wa kujadili changamoto kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi. STAMICO imejipanga kufanya vikao kazi na wadau wa uchimbaji mdogo kila baada ya miezi minne (4) ili kuboresha utendaji na kujenga uhusiano mzuri kati yetu na wadau wengine katika kuindeleza sekta ya uchimbaji mdogo” alifafanua Bi. Zena Kongoi.

Awali, Meneja wa Uchimbaji Mdogo wa STAMICO Bw. Tuna Bandoma amesema STAMICO kama mlezi wa wachimbaji wadogo imebaini kuwa moja ya changamoto kubwa wanazokutana nazo wachimbaji na wadau wa madini ni pamoja na upatikanaji wa taarifa za kijiolojia, ukosefu wa vifaa vya teknolojia stahiki ya uchimbaji na uchenjuaji wa madini, upatikanaji wa mitaji ya miradi ya uchimbaji mdogo na taarifa za masoko.

Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala Bw. Deusedith Magala (aliyesimama pichani) akifungua Kikao kazi cha siku mbili kati ya STAMICO na Wadau wa Uchimbaji Mdogo wa Madini Nchini kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo  kilichafanyika hivi karibuni STAMICO Makao Makuu, jijini Dar es Salaam. Aliyekaa kushoto kwake ni Meneja wa Uchimbaji Mdogo-STAMICO Bwana Tuna Bandoma, Mhandisi Migodi wa Wizara ya Nishati na Madini Chacha Marwa (wa pili kutoka kushoto) na Meneja Masoko na Uhusiano kwa Umma-STAMICO Bi Koleta Njelekela.

Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala Bw. Deusedith Magala (aliyesimama pichani) akifungua Kikao kazi cha siku mbili kati ya STAMICO na Wadau wa Uchimbaji Mdogo wa Madini Nchini kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo kilichafanyika hivi karibuni STAMICO Makao Makuu, jijini Dar es Salaam. Aliyekaa kushoto kwake ni Meneja wa Uchimbaji Mdogo-STAMICO Bwana Tuna Bandoma, Mhandisi Migodi wa Wizara ya Nishati na Madini Chacha Marwa (wa pili kutoka kushoto) na Meneja Masoko na Uhusiano kwa Umma-STAMICO Bi Koleta Njelekela.

Aidha, Bw. Bandoma amesema licha ya changamoto hizo STAMICO, imechukua jitihada za awali kuhakikisha inawezesha wachimbaji wadogo kupata taarifa za kijiolojia na mashapo ya madini kwa kufanya tafiti kwa gharama nafuu na kupitia taarifa zilizopo, kwa lengo la kushauri juu ya upatikanaji wa madini katika maeneo ya uchimbaji mdogo.

Aidha, Bw. Bandoma alijulisha wadau kuwa kwa sasa taarifa mbalimbali zihusuzo wachimbaji wadogo zitakuwa zikitolewa kupitia mfumo kielectroniki (Small Scale Mining Portal) uliozinduliwa mwezi Februari, 2016 ili kutoa taarifa za uchimbaji mdogo kuhusu bei za madini na masoko katika jitihada za kukuza soko la madini la ndani na nje.

“Nawapongeza wachimbaji wadogo kwa ushiriki wenu mkubwa katika kikao kazi hiki kwani huu ni mwanzo na msingi wa kuondoa matatizo yanayowakabili wachimbaji wadogo hususani baada ya kufahamu changamoto katika maeneo yao na kuweka mikakati ya pamoja ya namna ya kuleta suluhisho la kudumu” aliongeza Bw. Bandoma.

Akiongea kwa upande wa wadau, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa TAMIDA Bw. Rogers Sezinga ametoa rai kwa wadau wa madini nchini kutumia fursa iliyotolewa na Serikali tangu katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita ya kuwaendeleza wachimbaji wadogo kwa kupata taarifa na ushauri wa kitaalam utakowezesha kujiimarisha katika uzalishaji madini na hivyo kuweza kutoka katika uzalishaji duni kwenda uchimbaji wa kati wenye tija zaidi.

“Changamoto tunazokumbana nazo katika uchimbaji madini ni pamoja na ukosefu wa mbinu bora za kuhudumia mitambo, kutofahamu bei elekezi za madini, ukosefu wa soko, elimu ya kuandika michanganuo ya miradi na miundo mbinu ya barabara katika maeneo ya miradi ya uchimbaji” aliongezea Bw. Sezinga.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TAWOMA Mkoa wa Manyara Bi. Rachel Njau ameiomba Serikali kupitia STAMICO kuongeza idadi ya wachimbaji wadogo katika utoaji wa ruzuku, huku ikizingatia mazingira magumu ya uchimbaji na kutoa kipaumbele kwa wanawake ambao hutumia nguvu nyingi kukabiliana na mazingira magumu ya uchimbaji madini.

Kwa ujumla wao, wadau hao wameiomba Serikali kuwa karibu na Vyama vya Wachimbaji Wadogo ili waweze kutatua changamoto zao za elimu, mitaji, vifaa vyenye teknolojia ya kisasa na kuimarisha ulinzi wa masoko ya ndani na nje ya nchi.

Baadhi wa Wadau wa Uchimbaji Mdogo wa Madini kutoka mikoa 22 ya Tanzania Bara wakifuatilia uwasilishaji wa mada mbalimbali wakati wa kikao kazi hicho kilichoandaliwa na STAMICO.

Baadhi wa Wadau wa Uchimbaji Mdogo wa Madini kutoka mikoa 22 ya Tanzania Bara wakifuatilia uwasilishaji wa mada mbalimbali wakati wa kikao kazi hicho kilichoandaliwa na STAMICO.

Kikao kazi hicho baina ya STAMICO na Wadau wa Uchimbaji Mdogo wa Madini, kilifunguliwa rasmi na Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Shirika hilo, Bw. Deusdedith Magala, kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji.

Bw. Magala aliwataka wadau kutoa mapendekezo yatakayowezesha kutatua changamoto zilizopo zikiwemo za migogoro baina ya wachimbaji wadogo na wawekezaji wakubwa; hatua ambayo pia itatoa fursa kwa wadau wakiwemo STAMICO, Wizara ya Nishati na Madini, Mradi wa Uendelezaji Rasilimali za Madini (SMMRP) pamoja na wachimbaji wadogo wenyewe kufikia maazimio ya pamoja katika kuimarisha uendelezaji wa sekta ya uchimbaji mdogo nchini.

“Nachukua fursa hii kuwapeni rai kuwa msizungumzie changamoto tu, bali mtumie kikao hiki pia kuibua fursa zilizopo na zinazoweza kuwanufaisha wote kwa pamoja na hivyo kuiwezesha sekta ya Uchimbaji Mdogo kunufaisha ninyi wenyewe binafsi pamoja na Serikali kwa ujumla”. Alisisitiza Bw. Magala.

===========================================MWISHO====================================================

Imeandaliwa na:

Bibiana Ndumbaro
Afisa Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma,
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO),
S.L.P 4958,
Dar es Salaam.
Simu: +255-22-2150029, 
Barua Pepe: info@stamico.co.tz
Tovuti: http://www.stamico.co.tz
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 

Copyright © 2018 State Mining Corporation. All Rights Reserved.