Home » News and Events » Tanzania na Indonesia zasaini makubaliano ya awali kushirikiana sekta ya Madini

Tanzania na Indonesia zasaini makubaliano ya awali kushirikiana sekta ya Madini

SEVEN CRP

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse akikabidhi zawadi kwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa Kampuni PT. Timah TBK ya nchini Indonesia, Trenggono Sutioso baada ya kusaini makubaliano ya ushirikiano baina ya taasisi wanazozisimamia yaliyofanyika katika Ofisi ya Waziri Mkuu jijini Dar es Salaam, Desemba 2019.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Angellah Kairuki na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo wameshuhudia uwekaji wa saini wa makubaliano baina ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dkt. Venance Mwasse  na  Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa Kampuni  PT. Timah TBK ya nchini Indonesia, Trenggono Sutioso yaliyofanyika katika Ofisi ya Waziri Mkuu jijini Dar es Salaam.

Kampuni ya TP Timah PTK inamilikiwa na serikali ya Indonesia kwa asilimia 65 na asilimia 35 zilizobaki zinamilikiwa na wananchi kupitia mfuko wa hisa wa nchi hiyo.

Taasisi hizi mbili, zimeingia makubaliano yatakayowezesha ushirikiano katika shughuli za utafiti wa madini, uwekezaji, uchimbaji na uendelezaji wa sekta ya madini kwa ujumla.

Kwa kuanzia kampuni zitashirikiana katika kuendeleza leseni 15 zinazomilikiwa na STAMICO zenye aina mbalimbali za madini yakiwemo madini ya Bati (Tin), chuma, rare earth na phosphate.

Akizungumza wakati wa uwekaji saini wa makubaliano hayo, Naibu Waziri Mhe. Nyongo aliyeshuhudia tukio hilo kwa niaba ya Waziri wa Madini alisema amefurahishwa sana na uamuzi wa Serikali ya Indonesia wa kuonesha nia ya kuwekeza katika sekta ya madini nchini.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo wa (nne toka kushoto) akiwa na mashuhuda wa uwekaji saini makubaliano ya ushirikiano baina ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Kampuni ya PT. Timah TBK ya nchini Indonesia yaliyofanyika katika Ofisi ya Waziri Mkuu jijini Dar Es Salaam.

Mhe. Nyongo amesema, Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga katika kuwasaidia na kuwalinda wawekezaji wa nje hivyo kuwahakikishia usalama wa mali waliyowekeza nchini. “Tanzania ni moja ya nchi zinazosifika kwa kuwa na mazingira salama na sera nzuri kwa uwekezaji”. Alisisitiza.

Aidha, Mhe. Nyongo ameeleza kuwa sekta ya Madini nchini ni moja ya sekta zinazokuwa kwa kazi huku ikisifika kwa kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali madini yakiwemo madini ya metali, madini ya viwanda pamoja na madini ya ujenzi.

Pamoja na uwepo wa madini hayo, Tanzania ni mahala pekee yanapopatikana madini adhimu duniani, madini ya tanzanite. Pamoja na hayo Tanzania nchi ya nne katika uzalishaji wa madini ya Dhahabu ikiongozwa na Afrika Kusini, Ghana na Mali.

 

Wengine walioshuhudia uingiaji wa makubaliano hayo ni Balozi wa Tanzania nchini Indonesia, Dkt Ramadhan Dau, Waziri wa Bahari na Uwekezaji nchini Indonesia, Luhut Binsar Panjaitan, watendaji kutoka STAMICO na Tume ya Madini.

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 

Copyright © 2020 State Mining Corporation. All Rights Reserved.