Home » News and Events » WACHIMBAJI MADINI KANDA YA ZIWA KUNUFAIKA NA UCHORONGAJI MIAMBA WA KISASA UNAOFANYWA NA STAMICO

WACHIMBAJI MADINI KANDA YA ZIWA KUNUFAIKA NA UCHORONGAJI MIAMBA WA KISASA UNAOFANYWA NA STAMICO

Na Bibiana Ndumbaro-STAMICO GEITA

Wachimbaji wa madini nchini wakiwemo wale wa Kanda ya Ziwa wameshauriwa kutumia njia za kitaalam za tathmini na ukadiriaji wa mashapo katika maeneo ya leseni zao za uchimbaji madini, ili kuongeza tija katika uchimbaji kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.

Mtambo wa kisasa wa uchorongaji ujulikanao kama Multipurpose Air Rotary Drill Rig ukiwa katika eneo la Mgodi wa Dhahabu wa Buckreef tayari kwa kuanza kazi za uchorongaji miamba katika Mgodi huo

Mtambo wa kisasa wa uchorongaji ujulikanao kama Multipurpose Air Rotary Drill Rig ukiwa katika eneo la Mgodi wa Dhahabu wa Buckreef tayari kwa kuanza kazi za uchorongaji miamba katika Mgodi huo

Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Uchorongaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ngudu Alex Rutagwelela ameyasema hayo hivi karibuni, katika mkutano wake na waandishi wa habari, uliofanyika katika Mgodi wa Dhahabu wa Buckreef uliopo Tarafa ya Katoro Wilaya ya Geita, mkoani Geita.

STAMICO inafanya kazi hii ya uchorongaji katika Mgodi wa Buckreef baada ya kushinda zabuni ya kazi hiyo, ambapo mteja alidhihirika kuwa Shirika lina watalaam waliobobea katika utafiti na uchorongaji, na pia linakwenda sambamba na matumizi ya teknolojia za kisasa katika utafiti, uchorongaji (Multipurpose Air Rotary Drill Rig) na uchimbaji madini kwa

ujumla.

Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Uchorongaji ndugu Alex Rutagwelela (aliyesimama kushoto) akiangalia jinsi sampuli zinavyochukuliwa kupitia kifaa maalumu mara baada ya kutoka kwenye mtambo huo wa uchorongaji

Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Uchorongaji ndugu Alex Rutagwelela (aliyesimama kushoto) akiangalia jinsi sampuli zinavyochukuliwa kupitia kifaa maalumu mara baada ya kutoka kwenye mtambo huo wa uchorongaji

Ndugu Rutagwelela amesema mara baada ya STAMICO kumaliza zabuni hiyo, mtambo utaendelea kufanya kazi katika eneo hilo la Kanda ya Ziwa kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya wachimbaji madini wanaohitaji kupatiwa huduma za uchorongaji miamba katika maeneo yao ya uchimbaji madini.

“Kama ilivyoelezwa katika Mkutano Mkuu wa Wadau wa Sekta ya Madini uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, wachimbaji madini wengi wanahitaji kupatiwa huduma hii ya uchorongaji wa kisasa kwa gharama nafuu ili waweze kubaini kiwango cha mashapo na hivyo kuweka mikakati madhubuti ya uchimbaji madini katika maeneo yao” alifafanua Mkurugenzi Rutagwelela.

Aidha, amewataka wachimbaji madini Kanda ya Ziwa kujiunga kwenye vikundi ili kuweza kumudu gharama za kazi za uchorongaji zitakazofanywa na STAMICO hatimaye waweze kubaini kiwango cha mashapo; na kuondokana na kuondokana na uchimbaji wa kubahatisha.

“Wachimbaji wengi wadogo wamekuwa wanatumia njia za kiasili (Chabo) katika kukadiria na kutathmini mashapo yao, njia inayowapa taarifa zisizo sahihi na kuwafanya washindwe kukopesheka kutokana na kukosa taarifa sahihi za kijiolojia na hivyo kuathiri muendelezo wa shughuli zao za uchimbaji madini” alieleza ndugu Rutagwelela.

Mtaalam wa uchorongaji wa STAMICO ndugu. Fransis Mayayi akiendesha mtambo wa kisasa wa uchorongaji wa STAMICO, ambao kwa sasa upo katika Mgodi wa Dhahabu wa Buckreef kwa ajili ya uchorongaji

Mtaalam wa uchorongaji wa STAMICO ndugu. Fransis Mayayi akiendesha mtambo wa kisasa wa uchorongaji wa STAMICO, ambao kwa sasa upo katika Mgodi wa Dhahabu wa Buckreef kwa ajili ya uchorongaji

Kwa upande wake, Mjiolojia wa STAMICO Revocatus Mafungo amesema mtambo huo wa kisasa wa uchorongaji utaliwezesha Shirika kuwafikia wachimbaji wengi zaidi kwa gharama nafuu kwa kuwa una nguvu ya ziada ya kufua upepo wakati wa  uchorongaji, na hivyo kutoa sampuli zenye ubora  kwa haraka na kwa usalama zaidi kwa waendesha mtambo.

Waendesha mtambo wakitoa bomba lililobeba sampuli kutoka chini ya ardhi

Waendesha mtambo wakitoa bomba lililobeba sampuli kutoka chini ya Ardhi

 

 

 

 

 

 

 

 

Mwishoni mwa mwaka 2018 STAMICO ilipokea mtambo huo wa kisasa wa uchorongaji kutoka kwa Wizara ya Madini, ili kuiwezesha STAMICO kuwafikia wachimbaji wa madini na kuweza kufanya makadirio na tathmini ya mashapo yao kwa gharama nafuu, hatua ambayo itawawezesha kupata uhakika wa kiasi cha madini kinachokadiriwa kuwepo ardhini kabla ya kuanza rasmi shughuli za uchimbaji.

 

==============================MWISHO=============================================

Imeandaliwa na:

Koleta Njelekela

Meneja Masoko na Mawasiliano kwa Umma,

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO),

S.L.P 4958,

Dar es Salaam.

Simu: +255-22-2150029, 

Barua Pepe: info@stamico.co.tz

Tovuti: http://www.stamico.co.tz

 

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 

Copyright © 2020 State Mining Corporation. All Rights Reserved.