Home » News and Events » Wachimbaji wadogo kuondokana na uchimbaji wa kubahatisha

Wachimbaji wadogo kuondokana na uchimbaji wa kubahatisha

Meneja Uchimbaji wa STAMICO Bw. Tuna Bandoma (aliyesimama katikati) akipata taarifa kutoka kwa Mjiolojia Mwandamizi wa STAMICO Erick Robert (wa kwanza kushoto) kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa uanzishaji vituo vya uchenjuaji madini na utoaji mafunzo kwa Wachimbaji Wadogo nchini uliopo (Centers of Excellence)-Kituoa cha Rwabasi- Buhemba, kilichopo Wilaya ya Butiama, mkoa wa Mara. Mradi huo ambao unaratibiwa na Wizara na Nishati na Madini (MEM), unatekelezwa na STAMICO na GST.

Meneja Uchimbaji wa STAMICO Bw. Tuna Bandoma (aliyesimama katikati) akipata taarifa kutoka kwa Mjiolojia Mwandamizi wa STAMICO Erick Robert (wa kwanza kushoto) kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa uanzishaji vituo vya uchenjuaji madini na utoaji mafunzo kwa Wachimbaji Wadogo nchini uliopo (Centers of Excellence)-Kituoa cha Rwabasi- Buhemba, kilichopo Wilaya ya Butiama, mkoa wa Mara. 

  • Waipongeza STAMICO/GST kwa utafiti wa Kijiosayansi na ukadiriaji wa mashapo

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limekusudia kuwainua wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika eneo la Buhemba kwa kuwaondoa toka kwenye uchimbaji wa kubahatisha na kwenda kwenye uchimbaji wenye tija utakaowawezesha kupata madini kwenye maeneo watakayoendesha shughuli zao za uchimbaji.

Hatua hiyo itafikiwa kutokana kazi ya Utafiti wa Kijiosayansi na Ukadiriaji wa Mashapo, inayoendelea kufanywa kwa ajili ya wachimbaji wadogo, katika eneo hilo la Rwabasi-Buhemba lililopo mkoani Mara.

Kazi hiyo inayotekelezwa baina ya STAMICO na Wakala wa Jiolojia Tanzania (Geological Survey of Tanzania-GST), ni hatua ya utekelezaji wa Mradi wa Uanzishaji vituo vya uchenjuaji madini na utoaji mafunzo kwa Wachimbaji Wadogo nchini (Centers of Excellence).

Utafiti huo wa Kijiosayansi na Ukadiriaji wa Mashapo, utawawezesha wachimbaji wadogo kubaini maeneo yenye madini, kiwango cha madini yaliyopo na umbali wa madini kutoka ardhini hadi kwenye mwamba na hivyo kupata taarifa sahihi za kitaalam kuhusu mashapo yaliyopo na namna watakavyoweza kufanya uchimbaji wenye tija.

PICHA 02

Meneja Uchimbaji wa STAMICO Bw. Tuna Bandoma (katikati) akipokea taarifa kutoka kwa Wataalam wa Utafiti kutoka STAMICO na GST kuhusu utafiti wa mashapo unaoendelea katika eneo la Buhemba. Anaeelezea wa kwanza kulia ni Mjiolojia Mwandamizi kutoka STAMICO Erick Robert, akifuatiwa na Mjiolojia kutoka GST Bw. Gidson Kamihanda

Akiongea na Wandishi wa Habari hivi karibuni katika eneo hilo la mradi lililopo Rwabasi-Buhemba, unakofanyika utafiti huo, Meneja Uchimbaji Mdogo, kutoka STAMICO Bw. Tuna Bandoma alisema STAMICO kama mlezi wa wachimbaji wadogo nchini, imekusudia kuwawezesha wachimbaji wadogo kutoka kwenye uchimbaji wa kubahatisha kwenda kwenye uchimbaji wa uhakika mara baada ya kukamilika kwa kazi hiyo ya  utafiti.

 “Utafiti huu utakuwa na tija sana kwa Wachimbaji Wadogo kwani ukikamilika utawafanya waweze kuchimba maeneo yaliyofanyiwa utafiti na kuachana na uchimbaji wa kubahatisha; ambapo hujiamulia kuchimba bila kufahamu kama hapo wanapochimba kuna madini au laa.” Alibainisha Bw. Bandoma

 Alisema uchimbaji wenye tija kwa wachimbaji wadogo utawanufaisha wenyewe na utaleta pia manufaa makubwa kwa Taifa, kwani kadri Wachimbaji Wadogo watakapopata madini ya kutosha, Serikali kwa upande wake itapata kodi kutokana na tozo mbalimbali zikiwemo zitokanazo na mauzo ya madini, kama ambavyo sheria ya madini ya mwaka 2010 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2017; inavyowataka Wachimbaji Wadogo kulipa kodi ya 5% kwa madini wanayouza kila wakati.

PICHA 03

Wataalam wa Uchorongaji kutoka STAMICO wakiwa katika eneo la Rwabasi-Buhemba wilaya ya Butiama mkoani Mara, wakichoronga miamba kwa kutumia mtambo wa kisasa wa uchorongaji (unaoonekana pichani) katika mfumo wa Diamond Drilling, unaomilikiwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO). Lengo ni kupata sampuli zitakazopimwa katika maabara ili kubaini kiwango cha mashapo ya madini yaliyopo katika eneo hilo.

Bandoma alisema kwa kipindi kirefu Wachimbaji Wadogo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya kutumia nguvu nyingi kuchimba kwenye maeneo kwa kubahatisha; hivyo utekelezaji wa Mradi huu wa Uanzishaji vituo vya uchenjuaji madini na utoaji mafunzo kwa Wachimbaji Wadogo nchini uliopo (Centers of Excellence) ambapo Utafiti huo wa Kijiosayansi na Ukadiriaji wa Mashapo pia unafanyika; utakuwa ni ukombozi mkubwa kwa Wachimbaji Wadogo nchini.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Wachimbaji Wadogo mkoa wa Mara, Bw. Milele Mundeba, ameishukuru Serikali kupitia STAMICO na GST kwa hatua hiyo ambayo ameitaja kuwa ni ya mafanikio makubwa kwa Wachimbaji Wadogo.

PICHA 4 BUHEMBA

Meneja Uchimbaji mdogo kutoka STAMICO Bw. Tuna Bandoma (wa pili kutoka kushoto) akitoa maelelezo kwa Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu namna utafiti wa mashapo utakavyowanufaisha Wachimbaji Wadogo, mara utakapokamilika katika eneo hilo la Rwabasi-Buhemba. Wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wachimbaji Wadogo mkoa wa Mara Bw. Milele Mundeba, Mjiolojia kutoka Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) Bw. Gidson Kamihanda na Mjiolojia mwandamizi kutoka STAMICO Erick Robert.

“Tunampongeza Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna anavyo tujali Wachimbaji Wadogo na tunaipongeza STAMICO kwa jinsi walivyo kuwa bega kwa bega na sisi Wachimbaji Wadogo, hasa katika suala hili la utafiti wa mashapo, kwa kweli tumelipokea kwa mikono miwili na tunamuahidi Mhe, Rais kuwa Wachimbaji Wadogo tukiboreshwa tutakuwa walipa kodi wazuri kupitia kipato tutakachokipata kupitia madini” alisisitiza Bw. Milele

 Naye Mjiolojia Mwandamizi kutoka STAMICO, Bw. Erick Robert, alisema STAMICO/GST iko katika hatua za kukamilisha Utafiti huo wa Kijiosayansi na na ukadiriaji mashapo katika eneo hilo la Rwabasi-Buhemba; na kwamba kuna matumaini ya kuwepo madini katika eneo hilo, kutokana na dalili za awali zilivyojionesha wakati wa uchorongaji miamba.

 Bwana Robert amewataka wananchi wa maeneo hayo ya Buhemba kuwa na subira, kwani watapewa taarifa rasmi za matokeo ya utafiti huo pindi taratibu zote zitakapokamilika zikiwemo zile zinazohusu kazi ya utafiti wa Kimaabara wa Sampuli hizo.

 

===============================================MWISHO==========================================

Imeandaliwa na:

Bw. Issa Mtuwa
Afisa Mahusiano kwa Umma,
Shirika la Madini la Taifa,
Plot 417/418, Barabara ya Umoja wa Mataifa, Upanga,
S.L.P 4958,
Dar es Salaam.
Simu: +255-22-2150029, 
Barua Pepe: info@stamico.co.tz
Tovuti: http://www.stamico.co.tz

 

 

 

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 

Copyright © 2018 State Mining Corporation. All Rights Reserved.