Home » News and Events » Wachimbaji wadogo na Wanunuzi wa Madini Kanda ya Ziwa wapatiwa mafunzo ya Mfumo wa Kielektroniki

Wachimbaji wadogo na Wanunuzi wa Madini Kanda ya Ziwa wapatiwa mafunzo ya Mfumo wa Kielektroniki

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limewawezesha wachimbaji wadogo na wanunuzi wa madini Kanda ya Ziwa kupata mafunzo maalum ya namna ya kutumia mfumo wa kielektroniki (Small Scale Mining Portal) katika kupata taarifa zihusuzo sekta ya uchimbaji mdogo wa madini zikiwemo masoko na bei za madini.

Aidha, mafunzo yalihusisha pia matumizi ya mtandao wa Kompyuta na simu za mkononi kaatika kupata taarifa hizo.
Akifungua mafunzo hayo wiki iliyopita jijini Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa Victoria Magharibi Mhandisi David Mulabwa alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa wachimbaji wadogo kwa kuwa yanawapa ufahamu mpana wa kujua masoko na bei za kila siku duniani kutoka kwa wanunuzi mbalimbali na pia kuwasaidia kuchagua mnunuzi mwenye bei nzuri zaidi yenye thamani halisi ya madini (Value for money) Mhandisi Mulabwa alisema kwa pamoja na kujua bei lakini mafunzo hayo yamelenga pia kuwawezesha Wachimbaji wadogo kupata taarifa mbalimbali zinazohusu madini na sekta ya uchimbaji mdogo kupitia mtandao huo.

Afisa Tehama Mwandamizi kutoka STAMICO Bw. Daudi Bupilipili akitoa mafunzo ya ufahamu wa matumizi ya mfumo wa Kielektroniki kwa wachimbaji wadogo na wanunuzi wa madini jijini mwanza Juzi. Walio kaa meza kuu kutoka kushoto ni; Mgeni rasmi Kamishina Msaidizi wa Madini kanda ya ziwa Victoria Magharibi Mhandisi David Mulabwa, Mwenyekiti wa Wachimbaji wa dogo mkoa wa Mwanza Bw. Richard Seni na Mwakilishi wa SMRP Bi. Veronica Nangale.

Akimkaribisha mgeni rasmi kwa ajili ya ufunguzi wa mafunzo hayo, Meneja Uchimbaji Mdogo kutoka STAMICO ambae ndie Mratibu na muandaaji wa mafunzo hayo Bw. Tuna Bandoma alimtaarifu mgeni rasmi kuwa miongoni mwa faida ya mafunzo hayo ni kwamba wachimbaji wadogo wamesogezwa karibu na mlezi wao ambae ni STAMICO.

Aidha, aliwaarifu kuwa kupitia mfumo huo wachimbaji watapata taarifa mbalimbali zikiwemo orodha ya vifaa na bei zake pamoja na mahali vinapopatikana, taarifa za upatikanaji wa mitaji na teknolojia ya uchenjuaji wa madini kwa miradi yao ya uchimbaji na uchenjuaji madini.

Bw. Bandoma aliongeza kuwa, baada ya mafunzo hayo wachimbaji hao watakuwa na fursa ya kuuliza na kuwasiliana kuhusu jambo lolote linalowahusu hususani katika shughuli zao kwa kuingia na kufanya mawasiliano ya moja kwa moja na STAMICO kupitia ukurasa maalum ulioandaliwa mahususi kupitia tovuti ya mfumo huo (www.ssm-stamico.co.tz) na majibu yao watayapata moja kwa moja kupitia simu zao za mkononi.

Bw. Bandoma alisema kuwa sekta ya uchimbaji mdogo imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za ukosefu wa vifaa na zana stahiki vya uchimbaji, ukosefu taarifa sahihi za masoko ya madini ya uhakika, ukosefu wa mitaji kwa miradi ya uchimbaji mdogo wa madini. Kutokana na changamoto hizo alidokeza kuwa STAMICO imeendelea na itaendelea kuzishughulikia kwa kutafuta majawabu stahiki kwa kusaidiana na wadau wengine kama Serikali kupitia Wizara, GST, SIDO na SMMRP. Alisema kuwa bado jukumu la msingi la STAMICO litaendelea kuwa ni kuwasaidia wachimbaji wadogo kitaalamu kuboresha shughuli zao kwa kuongeza uzalishaji ulio bora zaidi.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya matumizi ya mfumo wa Kielektroniki katika kupata taarifa wakiwa katika picha ya pamoja. Walio kaa kutoka kushoto ni; Ismail Sadik Mnunuzi wa Madini, Mwenyekiti wa Wachimbaji wadogo mkoa wa Mwanza Bw. Richard Seni, Kamishina Msaidizi wa Madini kanda ya ziwa Victoria Magharibi Mhandisi David Mulabwa , Meneja Uchimbaji Mdogo kutoka STAMICO Bw. Tuna Bandoma, Mwakilishi wa SMRP Bi. Veronica Nangale na Bw. Muniko Magoiga mchimbaji mdogo.

Naye mwenyekiti wa Wachimbaji wadogo (MWEREMA) Bw. Mzakir Kasirate akizungumza wakati wa mafunzo hayo alisema anaishukuru STAMICO kwa kuandaa mafunzo hayo, kwani kupitia mafunzo hayo wamejifunza mengi na wamepata uelewa mkubwa ikiwemo matumizi ya mfumo wa mtandao wa kompyuta kupata taarifa, kufuatia bei ya soko la madini kutoka kwa wanunuzi mbalimbali lakini kubwa zaidi kupata nafasi ya kuuliza maswali kwa njia ya mtandao wa kompyuta na kupokea majibu kwa njia ya simu za mkononi.

STAMICO iliratibu mafunzo hayo ambayo ni ya kwanza hapa nchini kupatiwa wachimbaji wadogo ikiwa na lengo la kuwaunganisha wachimbaji wadogo, wanunuzi wa madini na STAMICO kupitia mtandao huo ili kuwezesha kupatikana kwa taarifa za uhakika na wakati zihusuzo bei za madini, vifaa na namna bora ya uchimbaji ulio salama.

===========================================MWISHO============================================

Imeandaliwa na:

Issa Mtuwa
Afisa Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma,
Shirika la Madini la Taifa,
Plot 417/418, Barabara ya Umoja wa Mataifa, Upanga,
S.L.P 4958,
Dar es Salaam.
Simu: +255-22-2150029, 
Barua Pepe: info@stamico.co.tz
Tovuti: http://www.stamico.co.tz

====================

Copyright © 2018 State Mining Corporation. All Rights Reserved.