Home » News and Events » WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI WAIPONGEZA STAMICO KWA KUWAJALI

WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI WAIPONGEZA STAMICO KWA KUWAJALI

Na Issa Mtuwa – BUHEMBA MARA

Wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu eneo la Buhemba lililopo wilaya ya Butiama mkoa wa Mara, wameipongeza STAMICO na Serikali kwa kuwajali na kutambua ugumu wanaoupata katika shughuli zao za uchimbaji hususani uchimbaji wa kubahatisha.

Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Uchorongaji Bw. Alex Rutagwelela kutoka Shirika la Madini la Taifa - STAMICO akiongea na Waandishi wa Habari wa mkoa wa Mara walioalikwa na STAMICO, kutembelea eneo la Rwabasi-BUHEMBA, ili kujionea utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi wa uanzishaji wa vituo vya mfano vya uchenjuaji madini (Centre of excellence) na utoaji mafunzo kwa wachimbaji wadogo Tanzania.

Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Uchorongaji Bw. Alex Rutagwelela kutoka Shirika la Madini la Taifa – STAMICO akiongea na Waandishi wa Habari wa mkoa wa Mara walioalikwa na STAMICO, kutembelea eneo la Rwabasi-BUHEMBA, ili kujionea utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi wa uanzishaji wa vituo vya mfano vya uchenjuaji madini (Centre of excellence) na utoaji mafunzo kwa wachimbaji wadogo Tanzania.

Wachimbaji wadogo hao wameyasema hayo hivi karibuni walipokuwa wakihojiwa na Waandishi wa Habari wa mkoa wa Mara walioalikwa na STAMICO, kuutembelea mradi  huo ulioko eneo la Rwabasi, BUHEMBA ili kujionea utekelezaji wa awamu wa kwanza ya mradi wa uanzishaji wa vituo vya uchenjuaji madini na utoaji mafunzo kwa wachimbaji wadogo Tanzania.

Wamesema tangu mwaka 2008 wamekuwa wakichimba dhahabu katika eneo la Rwabasi, lakini uchimbaji wao umekuwa hauna tija kwani wanachimba kwa kubahatisha pasipo kuwa na ishara inayowaonesha kuwa eneo wanalochimba lina madini husika au la.

Katika hatua nyingine, Wachimbaji wadogo hao wameishukuru STAMICO na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) kwa kuwezesha utekelezaji wa mradi huo kwani utasaidia kuwawezesha kukabiliana na changamoto zao zikiwemo kubaini kiwango cha mashapo ya dhahabu yaliyopo na hivyo kuepukana na uchimbaji wa kubahatisha.

Wamekiri kuupokea kwa mikono miwili mradi huo huku wakifurahia maamuzi yaliyofanywa na Serikali ya kuteua eneo lao kuwa la moja ya vituo vya mifano, kwani hatua hiyo itawasaidia kutoka kwenye uchimbaji wa kuhabatisha na kuwafanya wawe wachimbaji bora na wenye uhakika, kwamba maeneo wanayochimba, yamefanyiwa utafiti na uchorongaji hivyo kuchimba na kuwa na uhakika wa  kupata madini ya dhahabu ili kuongeza kipato chao.

“Kwanza kabisa niipongeze Serikali na STAMICO na GST kwa uamuzi wao wa  kutusaidia sisi wachimbaji wadogo, kitendo ambacho tumekifurahia sana kuona hawa mabwana wa STAMICO  na GST wamekuja. Tunashukuru sana kwa kutuondosha kwenye uchimbaji wa kubahatisha na kutuelekeza kwenye uchimbaji wa kitaalam na wenye tija” alisema Omahe Makina mchimbaji mdogo ambae pia ni Mhasibu wa Mwangaza Mining.

Naye, Bw. Machela Mwakambe Maseke, mchimbaji aliyewawakilisha Wachimbaji wadogo wa Buhemba kutoa neno, aliipongeza Serikali kwani inatambua shida zao, na kwamba ushauri wa kitaalam unaotolewa na taaisi zinazotekeleza mradi huu, unawasaidia, na hivyo wameiomba Serikali kuendelea kuwasadia zaidi kwa kuwa wao hiyo ndio kazi yao ya kuwaingizia kipato katika maisha yao.

Mchimbaji mdogo wa madini eneo la Rwabasi-BUHEMBA mkoani Mara, Bw. Machela Mwakambe Maseke, mwenye tochi kifuani, akitoa shukrani kwa serikali, STAMICO na GST mbele ya waandishi wa habari kwa kusikia kilio chao cha muda mrefu.

Mchimbaji mdogo wa madini eneo la Rwabasi-BUHEMBA mkoani Mara, Bw. Machela Mwakambe Maseke, mwenye tochi kifuani, akitoa shukrani kwa serikali, STAMICO na GST mbele ya waandishi wa habari kwa kusikia kilio chao cha muda mrefu.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Uchorongaji wa STAMICO Mjiolojia Alex Rutagwelela, alisema lengo la Serikali na STAMICO ni kuona wachimbaji wadogo wanaondokana na uchimbaji duni na wa kubahatisha, huku wakiachana pia na dhana potofu ya kuhusisha shughuli zao za uchimbaji na Imani za Kishirikina.

“Mradi huu unalenga kubainisha maeneo yote yenye madini na kuelekeza kwa wamiliki wa kisheria wa leseni husika kwamba madini hayo yanapatikana katika umbali gani kutoka ardhini kwenda chini na hivyo kuwasaida wachimbaji wadogo kuwa na uhakika wa kupata madini, pindi wanapochimba.

Bwana Rutagwelela aliongeza kuwa, dhamira ya STAMICO kama Mlezi wa Wachimbaji wadogo nchini, ni kuona wanatoka kwenye uchimbaji mdogo na kwenda kwenye uchimbaji wa kati na ikibidi wafikie katika hatua ya uchimbaji mkubwa.

Mradi huo unaotekelezwa kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Raslimali za Madini (SMMRP), unafadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia Wizara ya Nishati na Madini unatarajiwa kugharimu jumla ya dola za Kimarekani 3.7 M ambazo karibu na Tsh. 8.2 Bilioni.

Mtambo mpya (RIGI) wa STAMICO ukifanyakazi katika eneo la wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu Rwabasi-BUHEMBA mkoani Mara.

Mtambo mpya (RIGI) wa STAMICO ukifanyakazi katika eneo la wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu Rwabasi-BUHEMBA mkoani Mara.

“Sisi (STAMICO) ni walezi wa wachimbaji wadogo, tumepewa jukumu na kuwalea na kuwasimamia hivyo tunalo jukumu kubwa juu yao la kuhakikisha uchambaji wao unakuwa wenye tija na manufaa yao na Taifa kwa ujumla.” Alisisitiza  Bw. Rutagwelela.

Baada ya kukamilika kwa mradi huu, jumla ya vituo saba vya mfano (Centers’ of Excellence vitakuwa vimeanzishwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini, yakiwemo Kituo cha Itumbi-Chunya (Mbeya), Kantente-Ushirombo (Geita), Buhemba –Butihama (Mara), Mpanda (Katavi), Kange (Tanga), Kyerwa Syndicate (Kyerwa-Kagera) na Masakasa (Lindi) ambapo vituo vyote ni vya madini ya dhahabu ispokuwa Kyerwa (Bati),Kange (Limestone) na Masakasa (Chumvi).

 

 

 

============================================MWISHO===============================================

Imeandaliwa na:

Koleta Njelekela
Meneja Masoko na Mawasiliano kwa Umma,
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO),
S.L.P 4958,
Dar es Salaam.
Simu: +255-22-2150029, 
Barua Pepe: info@stamico.co.tz
Tovuti: http://www.stamico.co.tz

 

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 

Copyright © 2018 State Mining Corporation. All Rights Reserved.