Home » News and Events » STAMICO yashiriki katika maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi duniani 2019

STAMICO yashiriki katika maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi duniani 2019

  • Wakiri Uzalendo na Uwajibikaji ni suluhu katika kukuza Maslahi Bora Sehemu ya Kazi

Wafanyakazi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) wameungana na Wafanyakazi wengine nchini kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani mwaka 2019 Kimkoa na Kitaifa ambapo wamekiri uzalendo na uwajibikaji ni suluhu muhimu katika kukuza masilahi bora sehemu ya kazi.

Wafanyakazi hao wa STAMICO wamebainisha hayo katika mahojiano maalum yayoliyofanywa na Mwandishi wa Habari hii mara baada ya kumalizika kwa Sherehe za maadhimisho Siku ya Wafanyakazi mkoani Dar es Salaam ambapo Kitaifa yaliadhimishwa mkoani Mbeya.

Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani mwaka 2019 ni “Tanzania ya Uchumi wa Kati inawezekana, wakati wa Mishahara na Maslahi Bora kwa Wafanyakazi ni SASA”.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi TAMICO tawi la STAMICO-Makao Makuu, Dar es Salaam Bwana Denis Silas (wa kwanza kulia) akiongoza Wafanyakazi kutoa salaam kwa Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Paul Makonda (hayupo pichani) wakati wa Sherehe za Mei Mosi, katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Walioshikilia bango Mhandisi Migodi Suleiman Khalid (wa pili kutoka kulia) na Mwenyekiti wa Kamati ya Vijana Tawi la TAMICO-STAMICO Makao Makuu- Dar es Salaam Bwana Mohamed Omary Kaunya.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi TAMICO tawi la STAMICO-Makao Makuu, Dar es Salaam Bwana Denis Silas (wa kwanza kulia) akiongoza Wafanyakazi kutoa salaam kwa Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Paul Makonda (hayupo pichani) wakati wa Sherehe za Mei Mosi, katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Walioshikilia bango Mhandisi Migodi Suleiman Khalid (wa pili kutoka kulia) na Mwenyekiti wa Kamati ya Vijana Tawi la TAMICO-STAMICO Makao Makuu- Dar es Salaam Bwana Mohamed Kaunya.

 

Wakizungumzia kuhusu kauli mbiu hiyo Wafanyakazi hao wa STAMICO wamesema lazima wajifunge mkanda na kuchapa kazi kizalendo, kuimarisha ubunifu na kukuza uwajibikaji, hatua ambayo itasaidia kuinua mapato ya Taasisi zao na maslahi ya watumishi kwa ujumla.

“Ni wakati muafaka kwa Wafanyakazi kuacha kulalamika na kulaumu Viongozi katika maeneo yetu ya kazi, bali tuchape kazi kikamilifu kwa kushirikiana na Menejimenti ili kutafuta suluhisho la pamoja la kutatua changamoto zetu ili  tutekeleze majukumu yetu kwa ufanisi mkubwa hatimaye tuweze kupata maslahi bora katika kazi.” Alifafanua Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodi, Nishati, Ujenzi na kazi nyinginezo (TAMICO) tawi la STAMICO Makao Makuu, Dar es Salaam Bwana Denis Silas.

 Akizungumza kwa njia ya simu kutoka mkoani Mbeya, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa STAMICO Bwana Deusdedith Magala amewapongeza Wafanyakazi kwa ushiriki wao katika Sherehe za Mei Mosi 2019 na amewataka wachape kazi kwa juhudi na maarifa bila manung’uniko; kwani Serikali imetoa dhamana kwa STAMICO kusimamia rasilimali adimu na muhimu ya Madini nchini.

Wafanyakazi wa STAMICO wakiwa nje ya Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam tayari kwa kuanza maandamano ya kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani 2019 kwa mkoa wa Dar es Salaam.

Wafanyakazi wa STAMICO wakiwa nje ya Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam tayari kwa kuanza maandamano ya kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani 2019 kwa mkoa wa Dar es Salaam.

“Nikiwa Mkurugenzi wa Rasilimali na Utawala nasema moshi mweupe kwa STAMICO umeanza kuonekana hivyo kila mmoja wetu achape kazi na kuboresha nidhamu ya kazi ili kukuza ufanisi kwa manufaa mapana ya Shirika na Taifa kwa ujumla. Wakati wa kuonesha matokeo ni sasa hatunabudi kuunga mkono juhudi za Serikali ya Aawamu ya Tano ya kuhakikisha kuwa yananufaisha Taifa.” Alibainisha Bwana Magala.

Aidha, Magala ameitaka Menejimenti ya STAMICO kuongeza kasi ya ubunifu na kufanya maamuzi sahihi na kwa wakati katika Vitengo, Idara na Kurugenzi zao ili kuliwezesha Shirika kutekeleza kwa wakati majukumu yake, ikiwemo miradi yake ya ubia, inayoendeshwa na Kampuni Tanzu na ile inayotekelezwa kwa ushirikiano na Wazabuni.

Alisisitiza kuwa STAMICO kama mwekezaji katika sekta ya madini kwa niaba ya Serikali ina wajibu mkubwa wa kuchangia katika Pato la Taifa.

 

============================================MWISHO==============================================

Imeandaliwa na:

Koleta Njelekela

Meneja Masoko na Mawasiliano kwa Umma,

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO),

S.L.P 4958,

Dar es Salaam.

Simu: +255-22-2150029, 

Barua Pepe: info@stamico.co.tz

Tovuti: http://www.stamico.co.tz

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 

Copyright © 2020 State Mining Corporation. All Rights Reserved.