Home » News and Events » Watumishi STAMICO kupigwa msasa kuhusu ugonjwa wa UKIMWI na magonjwa yasiyoambukiza (NCDs’)

Watumishi STAMICO kupigwa msasa kuhusu ugonjwa wa UKIMWI na magonjwa yasiyoambukiza (NCDs’)

Shirika la Madini la Madini la Taifa (STAMICO) linatarajia kufanya Semina kuhusu Virusi vya Ukimwi, Ugonjwa wa ukimwi na Magonjwa yasiyoambukiza (NCDs’), kwa watumishi wake ili kukukuza weledi kuhusu magonjwa hayo na mbinu za kuyatokomeza sehemu ya kazi, hatimaye kuinusuru nguvukazi ya Taifa.

Kaimu Meneja wa Rasilimaliwatu wa Shirika hilo Bw. Lameck Kabeho amesema Semina hiyo ya siku moja itafanyika leo tarehe 10/10/2017 na itashirikisha watumishi 60 wanaofanya kazi katika Makao Makuu ya Shirika hilo, yaliyopo barabara ya Umoja wa Mataifa, jijini Dar es Salaam.

Bw. Kabeho amesema STAMICO imeamua kufanya Semina hiyo ili kuunga mkono juhudi za Serikali za kudhibiti maambukizi ya virusi vya ukimwi sehemu ya kazi, Kutekeleza Sera ya Taifa ya VVU na Ukimwi na kushiriki katika Mkakati wa Kitaifa wa kutokomeza magonjwa yasiyoambukiza (NCDs’); huku ikiimarisha maadili ya watumishi wake, kwa lengo la kubadili tabia na mfumo mzima wa maisha yao ili kuwaepusha katika hatari ya kukumbwa na magonjwa hayo.

“Kimsingi HIV/AIDS na magonjwa sugu yasiyoambukiza kama vile shinikizo la damu, kisukari, magonjwa ya moyo, kiharusi, n.k yamekuwa tatizo kubwa katika jamii kutokana na mfumo mbovu wa maisha na tabia za watu kutopenda kufanya mazoezi. Hali hii inahatarisha nguvu kazi ya Taifa na kuathiri utendaji kazi wenye kasi ya matokeo chanya, hasa kwa watumishi walioathirika na magonjwa hayo wakiwa kazini.” Alifafanua Bw. Lameck

Semina hiyo ya siku moja imeandaliwa na STAMICO kwa kushirikiana na TACAIDS na PASADA na itahusisha upimaji wa hiari wa Virusi vya Ukimwi, Kisukari, Shinikizo la Damu na Body Mass Index kwa watumishi waliotayari kufanya hivyo, hatua ambayo itawawezesha kutambua hali yao ya  afya na hivyo kuweza kutibiwa au kuchukua tahadhari kwa haraka.

 

LAMECK

Mratibu wa Semina ya Siku Moja ya Watumishi wa STAMICO inayohusu Virusi vya Ukimwi, Ugonjwa wa Ukimwi na Magonjwa Yasiyoambukiza (NCD’s) ambaye pia ni Kaimu Meneja wa Rasilimaliwatu wa STAMICO Bw. Lameck Kabeho, akiwa katika kazi ya kumilisha maandalizi ya Semina hiyo Ofisini kwake, jijini Dar es Salaam (Habari na picha imeandaliwa na Koleta Njelekela-STAMICO).

 

==============================MWISHO=============================================

Imeandaliwa na:

Koleta Njelekela

Meneja Masoko na Mawasiliano kwa Umma,

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO),

S.L.P 4958,

Dar es Salaam.

Simu: +255-22-2150029, 

Barua Pepe: info@stamico.co.tz

Tovuti: http://www.stamico.co.tz

 

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 

Copyright © 2018 State Mining Corporation. All Rights Reserved.