Home » News and Events » Waziri Kairuki – “STAMICO songeni mbele hakuna kulala”

Waziri Kairuki – “STAMICO songeni mbele hakuna kulala”

IMG_0092

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Kanali Mha. Sylvester Ghuliku (wa pili kulia) akimuelezea Waziri wa Madini Mhe. Angellah Kairuki namna shughuli za uchimbaji wa Makaa ya Mawe unavyoendelea Mgodini Kabulo.

Waziri wa Madini Mhe. Angellah Kairuki amelipongeza Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na wafanyakazi wake kwa juhudi na uzalendo katika utendaji kazi uliopelekea kuanza kwa uzalishaji wa makaa ya  Mawe katika mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kabulo –Kiwira.

Akiongea wakati wa ziara yake mgodini hapo jana tarehe 28 Novemba 2018, Kairuki ametoa pongezi hizo kufuatia uzalendo na juhudi za wafanyakazi wa STAMICO zilizopelekea kufufuliwa kwa mitambo iliyokuwa imechakaa baada ya kukaa muda mrefu bila kutumika, mitambo ambayo kama ingenunuliwa mipya ingeigharimu Serikali fedha nyingi.

“Naomba niwapongeze STAMICO kwa hiki mlichokifanya, na Serikali ya awamu ya tano inasisitiza uzalendo na moyo wa kujitolea kwa ajili ya Taifa hili na nyinyi STAMICO mmeonesha mfano. Hii mitambo kama mngesubiri Serikali iwanunulie mipya pengine uzalisha huu ungekuwa bado haujaanza. Naomba niwapongeze kwa hili na endeleni kusonga mbele na hakuna kulala” alisema Mhe. Kairuki.

Aidha, Waziri Kairuki amesema pamoja na juhudi zote zinazofanywa na STAMICO Wizara yake itaendelea kushirikiana na STAMICO katika mambo mbalimbali kuhakikisha mradi huu unakuwa na tija kwa Taifa na kuwanufaisha wananchi kwa kuzalisha mkaa wa aina mbalimbali utakaotumika viwandani na majumbani.

“STAMICO mmepiga hatua kubwa sana, mimi kama Waziri ningependa kuiona STAMICO inasonga mbele zaidi katika uzalishaji wa makaa ya mawe na kufikia viwango ya kimataifa katika uzalishaji wa makaa ya mawe kama ilivyo kwa nchi ya Afrika Kusini inayoongaza kwa Afrika katika uzalishaji wa makaa ya mawe” aliongeza Mhe. Kairuki.

Waziri wa Madini Mhe. Angellah Kairuki akisikiliza kwa makini maelezo ya kitaalam kuhusu Makaa ya Mawe kutoka kwa Mjiolojia wa STAMICO Bw. Nobert Mkopi

Waziri wa Madini Mhe. Angellah Kairuki akisikiliza kwa makini maelezo ya kitaalam kuhusu Makaa ya Mawe kutoka kwa Mjiolojia wa STAMICO Bw. Nobert Mkopi

Akiongea mbele ya Waziri wakati wa ziara hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Kanali Mha. Sylvester Ghuliku amemshukuru Waziri kwa ushirikiano wake kwa Shirika kwani amekuwa bega kwa bega na ushauri wake wa mara kwa mara unasaidia Shirika kusonga mbele katika kuhakikisha miradi yetu inaanza uzalishaji ili iweze kutoa mchango kwa Taifa.

“Lengo la STAMICO pamoja na miradi mingine, mradi wa Makaa ya Mawe unakuwa na tija kwa Taifa na kuleta faida kwa Shirika, faida ambayo itatumika kuboresha mgodi na mitambo” alisema Ghuliku.

Kwa upande wake Mratibu wa mradi huo Mha. Peter Maha, amesema uzalishaji unaoendelea mgodini hapo umeongeza  uhakika wa upatikanaji wa nishati ya makaa ya mawe na kuongeza wateja wapya na kuwarudisha wateja waliopotea siku za nyuma.

Ziara ya Waziri Kairuki mgodini Kabulo ni utimilifu wa ahadi aliyoitoa katika ziara yake aliyoifanya STAMICO Makao Makuu  jijini Dar es salaam mwanzoni mwa mwezi Novemba mwaka huu.

==================================================================================================

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 

Copyright © 2019 State Mining Corporation. All Rights Reserved.