STAMICO YAWAFUNDA VIONGOZI WA WACHIMBAJI NA WAFANYABIASHA WA MADINI
Shirika la Madini la Taifa ( STAMICO ) katika azma yake ya kuhakikisha inaendelea kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo kuwafanya wawe bora, imefanya mafunzo maalumu kwa Viongozi wa wachimbaji na wafanyabiashara wa Madini.
Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa African Dream jijini Dodoma tarehe 25/04/2026 na kuhudhuriwa na Viongozi wa FEMATA, CHAMATA, TAWOMA, TYM, TBMA pamoja na TASPA.
Akiongea kabla ya kuanza kwa mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea Viongozi hao uwezo mpana wa kuongeza thamani katika sekta ya madini, nafasi ya wachimbaji wadogo kuelekea utekelezwaji wa DIRA 20250, ilinziwa mazingira, dhana ya ESG, Afya na usalama mahala pa kazi.
Ameongeza maarifa ambayo Viongozi wote wanaosimamia Kamati mbalimbali ndani ya FEMATA yatasaidia katika kuongeza ushirikiano mzuri kati ya wachimbaji na Serikali.
Akifungua mafunzo hayo, kwa niaba ya Waziri wa Madini, Kamishna wa Madini Dkt. Abdulrahman Mwanga amewataka Viongozi hao kutanguliza uzalendo na uadilifu katika kusimamia rasilimali madini ili utajiri huo uendelee kuwanufaisha Watanzania wa leo na vizazi vijavyo.
Dkt. Mwanga amesema kuwa, rasilimali madini ni nguzo kwa uchumi wa Taifa ambayo inatoa fursa za kiuchumi kwa Watanzania kunufaika moja kwa moja kupitia mapato au miradi mikubwa ya Kitaifa inayotokana na sekta ya madini kupitia programu maalum ya uwajibikaji wa Makampuni kwa jamii ( CSR ) na uwezeshwaji wa jamii kwenye rasilimali zinazoizunguka ( Local Content ).
Dkt. Mwanga ameongeza kuwa, uchimbaji madini unaendana na utunzaji wa mazingira, jambo ambalo ni la kimkakati kwa Taifa na ustawi wa jamii nzima kwa lengo la kutekeleza takwa la kisheria linalohusu Usalama Mahala pa Kazi.
Kuhusu utoroshaji wa Madini, Dkt. Mwanga amefafanua kuwa, suala la utoroshaji wa madini ni kinyume na Sheria ya Madini Sura Namba 123 na Sheria nyingine za nchi, hivyo amewaasa Viongozi hao kutojihusisha na mifumo yoyote ya utoroshaji madini nchini.
Aidha ameongeza kuwa, utoroshaji wa madini unasababisha hasara kubwa za kiuchumi na kijamii, hii ni kutokana na Serikali kukosa mapato ya kodi, jambo linalopelekea kurudisha nyuma maendeleo ya Taifa.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Madini, Bw. Augustino Olal amesema, mafunzo hayo ya kimkakati yameletwa kwa mpango maalum ambao utaleta matokeo chanya kwenye uongozi katika sehemu za kazi na kuongeza uzalishaji madini nchini.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Wachimbaji Wadogo Tanzania ( FEMATA ) Bw. John Bina ameiomba STAMICO kutoa mafunzo kwa Viongozi wa Serikali za Mitaa kupewa Semina kuhusu Sheria za Madini na kanuni zake ili kuondoa mgongano wa maslahi katika mnyororo mzima wa thamani madini.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji Chumvi Tanzania ( TAPSA ) Bi. Hawa Ghasia, ameipongeza Wizara ya Madini kupitia STAMICO kwa kutatua changamoto 7 kati ya 13 ambapo nyingine zilizobaki zikiendelea kutafutiwa ufumbuzi.
Ameishukura Serikali kwa kuweka miundombinu mizuri kwenye mashamba ya chumvi pamoja na ujenzi wa Kiwanda cha kuchakata chumvi kilichopo mbioni kukamilika.
Pamoja na mambo mengine, vyama vingine kikiwemo Chama cha CHAWATA, TAWOMA, vimeipongeza Wizara ya Madini kwa ushirikiano mzuri unaoendelea katika sekta ya Madini.
STAMICO inaendelea na azma ya kuendelea kuwapatia mafunzo Wachimbaji wadogo kama sehemu ya ulezi wake wa kuwajengea uwezo katika mnyororo mzima wa Madini.