Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

State Mining Corporation

State Mining Corporation

News

DKT. BITEKO AWATAKA WATUMISHI WA STAMICO KUENDELEA KUNG'ARISHA SHIRIKA LA MADINI


Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amewataka wafanyakazi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuendelea kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili Shirika lizidi kusonga mbele kwa mafanikio.

Ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya Maadili ya Utumishi wa Umma, UKIMWI na Magonjwa yasiyoambukiza yaliyofanyika jijini Dodoma, Januari 21,2023

Amewataka wafanyakazi kuzingatia mafunzo hayo yanayotolewa ili kuweza kuepuka kujiingiza katika mambo yenye viashiria vya ukiukaji wa maadili na kujiletea matatizo mahali pa kazi.

Ameishukuru Sekretariati ya ya Maadili ya viongozi kwa kukubali kuja kutoa mafunzo hayo kwa wanastamico jambo litakalowasaidia kufanya kazi kwa kujipima kwa mujibu wa Maadili ya kiutumishi wa umma.

Dkt. Biteko ametumia nafasi hiyo kuipongeza Bodi, Menejimenti na wafanyakazi wa STAMICO kwa kufanya kazi kwa bidii na kulipatia sifa Shirika na Wizara kwa ujumla.

Amesema kutokana na jitihada hizo zimeifanya STAMICO kuwa miongoni mwa Mashirika bora barani Afrika ambapo mashirika mengine yanakwenda kujifunza namna ya utekelezaji wa majukumu yake kwa mafanikio.

Amesisitiza kuongeza mitambo ya uchenjuaji katika vituo vya Mfano vya wachimbaji wadogo ili kurahisisha huduma ya uchenjuaji na kupunguza foleni kwa wachimbaji wadogo.

Amesema ni vyema watumishi wakatambua kuwa Serikali inaliangalia Shirika hili kwa macho mawili na ipo mstari wa mbele kuhakikisha Shirika linafikia mafanikio yake hivyo ni vyema wakafanya kazi kwa uadilifu na kujituma.

Akiongea kwa niaba ya Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Madini Bw. Issa Nchasi ametaka wafanyakazi kufuatilia mafunzo hayo kwa umakini ili kujiepusha na migogoro ya kimaadili inayoweza kujitokeza pindi mtu atakapokiuka kanuni za maadili ya utumishi wa umma kwa kisingizio cha kutofahamu kanuni hizo.

Kwa upande wa STAMICO Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Venance Mwasse ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kusimamia utekelezaji wa miradi ili kuongeza mapato ya Shirika.

Amesema STAMICO inazidi kujipambanua katika miradi yake kwa kuongeza mitambo ya uchorongaji hadi kufika 14 na mtambo 5 kwa ajili ya wachimbaji wadogo, kununua mitambo mikubwa ya kuzalisha Mkaa mbadala sambamba na kuanzisha mgodi wake wenyewe.

Kwa upande wa watoa mafunzo kutoka Sekretariati ya maadili kwa viongozi Bw. Salvatory Kirasala ametoa rai kwa wafanyakazi kuzingatia kanuni za utumishi wa umma zikiwemo kutoa huduma bora, utii kwa Serikali, Bidii ya kazi, kutoa huduma bila upendeleo na kufanya kazi kwa uadilifu ili kuleta manufuaa kwa Shirika.

Akiongea kwa niaba ya wafanyakazi, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi TAMICO Bw. Mohamed Kaunya ameishukuru Wizara, Bodi na Menejimeti ya STAMICO kwa kuandaa mafunzo haya adhimu yebye manufaa kwa Shirika.

Ameahidi kuyatekeza yale yote yaliyofundishwa kwa uaminifu

STAMICO imetoa mafunzo kwa wafanyakazi wake wote wakijuishwa wale waliopo katika maeneo ya mradi ili kuweza kuboresha utendaji kazi hasa katika wakati huu wanapofungua mwaka.