Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

State Mining Corporation

State Mining Corporation

News

JESHI LA MAGEREZA TAASISI YA KWANZA YA SERIKALI KUTUMIA MKAA MBADALA WA RAFIKI BRIQUETTES UNAOZALISHWA NA STAMICO


KATIKA kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, Jeshi la Magereza limeingia makubaliano maalumu na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa ajili ya mauziano ya nishati safi ambayo ni mkaa mbadala wa kupikia (Rafiki Briquettes) unaozalishwa na shirika hilo.

Pia STAMICO imeingia mkataba wa ushirikiano na Jeshi hilo la magereza kwa ajili ya kuendeleza utafiti na uchimbaji wa maeneo yenye leseni ya uchimbaji madini.

Makubaliano hayo yamesainiwa leo tarehe 8 June 2024 jijini Dar es Salaam na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP), Mzee Ramadhan Nyamka pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dk.Venance Mwasse.

Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo, Kamishna Jenerali wa Magereza amesema utiaji saini baina ya taasisi hizo mbili ni muendelezo wa utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia aliyoyatoa tarehe 8 Mei mwaka huu wakati akizindua mkakati wa taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwamba taasisi zote zinazolisha zaidi ya watu 100 kwa siku, zianze kutumia nishati safi ya kupikia.

“Leo nimekabidhiwa mkaa rafiki ambao unatokana na makaa ya mawe mkaa huu utatufanya tuondokane na matumizi ya kuni na mkaa hivyo na sisi magereza tutakuwa tumechangia uhifadhi na utunzaji wa mazingira yetu hasa ikizingatiwa tumeambiwa ipo stock ya kutosha ya mkaa huu katika kutumika kulisha magereza yote nchini kwa miaka mingi ijayo,” amesema.

Amesema jeshi hilo linayo magereza 129 yenye uwezo wa kuhifadhi wafungwa 29,902 kwa siku nchini ambapo wafungwa hao huhitaji huduma za malazi, chakula na matibabu.

Amesema chanzo kikuu cha nishati ya kupikia kwenye magereza ni kuni na mkaa, hivyo kwa siku magereza hayo hutumia kuni zenye ujazo wa mita91,591.25 kwa ajili ya kupikia.

“Ukiangalia tasfiri yake ni miti mingi sana inabidi ikatwe kwa siku ili kuwezesha kuwapikia wafungwa chakula. Sasa tunakwenda kuondokana na uharibifu wa mazingira kupitia makubaliano haya,” amesema na kuongeza;

“Pia ndani ya magereza tunaenda kupata faida ya kulinda afya za wapishi ambao ni wafungwa na askari wanaosimamia kutokana na moshi uliokuwa unatokana na kuni na mkaa.”

Aidha, kuhusu utafiti na uchimbaji wa madini, amesema baadhi ya maeneo yamefanyiwa utafiti na kuonekana kuna madini mbalimbali, hivyo ushirikiano huo wa STAMICO na magereza utatumika kuimarisha uchimbaji endelevu kwa masilahi ya watanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dk. Venance Mwasse amesema mbali na kuwashukuru magereza kwa mwitikio wao wa kutumia nishati hiyo safi ya kupikia, pia amewaahidi kutekeleza makubaliano hayo kwa asilimia 100.

Amesema kutokana na uwekezaji uliopo STAMICO wanawahakikishia upatikanaji wa nishati hiyo mbadala kwa muda wote.

“Uzalishaji utakuwepo mkubwa kwani mwisho wa mwezi huu tunakwenda kukamilisha ujenzi wa kuna viwanda vyenye uwezo wa kuzalisha tani 20 kwa saa. Kiwanda kimoja kipo Kisarawe mkoani Pwani na kingine kipo Kiwira mkoani Mbeya.

“Pia katika bandari ya Dar es Salaam tayari yametua makontena 14 yenye urefu wa futi 40 ambapo ndani yake kuna mitambo ya uzalishaji wa mkaa huu ambayo itakwenda kufungwa mkoani Dodoma na Tabora. Pia mitambo hii itakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 20 kwa saa,” amesema.

Akizungumzia kuhusu mkataba wa uchimbaji madini, Dk. Mwasse amesema STAMICO ambayo ina uzoefu wa zaidi ya miaka 50 kwenye tasnia ya madini, wanakwenda kuunda kikosi kazi katika kutekeleza makubaliano ya mkataba huo ambao ni utafiti na uchimbaji wa madini hasa ikizingatiwa shirika hilo linao wafanyakazi wa kutosha wenye uzoefu katika sekta hiyo.