Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

State Mining Corporation

State Mining Corporation

News

KAMATI YA UWEKEZAJI YA BUNGE YARIDHISHWA NA UTENDAJI MZURI WA STAMICO


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma imeishauri Wizara ya Madini kuelekeza migodi yote ambayo serikali inaubia isafishe dhahabu zake katika kiwanda cha kusafisha dhahabu kilichopo Jijini Mwanza (Mwanza Precious Metals Refinery( MPMR).

Ushauri huo umetolewa leo Machi 26,2023 na Makamu Mwenyeki wa Kamati hiyo Mhe. Vuma Augustine baada ya kutembelea na kukagua kiwanda hicho kilichopo kata ya Pasiansi Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza ambacho kimegharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 16 ambapo hisa zake zinamilikiwa na Shirika la madini la Taifa,(STAMICO) kwa asilimia 25.

"Mradi ni mzuri sana ni wa kisasa na una tija, tumetembelea na tumethibitisha yote hayo, tunaipongeza Wizara ya Madini inafanya kazi nzuri sana kuilea STAMICO, wote tunafahamu kwamba mwaka 2017 kushuka chini, Shirika hili lilikuwa linatengeneza hasara kubwa mpaka ilifikia kipindi sisi kama kamati tulitaka kuishauri serikali ilifute Shirika hilo.

"Lakini kwa sasa limeweka mikakati na limejipanga vizuri kupitia miradi yake, limekuwa ni shirika linalopata faida, wajibu wetu ni kuisimamia serikali na mashirika yake kuhakikisha inafanya uwekezaji wenye tija na hatimaye yalete gawio kwa Serikali."amesema Mhe.Augustine.

Aidha, ametoa wito kwa STAMICO kuendelea kubana matumizi na kufanya uwekezaji wenye tija ili waendelee kupata faida na kutoa gawio kwa Serikali.

Pia Kamati hiyo imeshauri kuwa kiwanda hicho kutoa kipaumbele kwa kuwaajiri wazawa wenye sifa.

Kwa Upande wake Waziri wa Madini Mheshimiwa Dkt.Doto Biteko amewataka watanzania wote wanaojihusisha na uchimbaji wa madini kusafisha madini hayo kabla ya kuyasafirisha nje ya nchi.

"Na huu ndiyo msukumo wetu mkubwa, tumejenga hivi viwanda si kwa kubahatisha bali viweze kufanya kazi, madini yote na dhahabu yanayochimbwa yasafishwe ndiyo yauzwe nje ya nchi." Amesema Mhe.Biteko.

Akitoa neno ka shukrani kwa kamati ya Uwekezaji Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO Meja Jenerali Mstaafu Michael Isamuhyo amesema STAMICO imefurahi sana kupokea ujumbe huu ambao umeweza kultembelea kiwanda hicho na kujionea namna kinavyofanya kazi.

Amesema STAMICO imepokea ushauri uliotolewa, kufuata na kuyafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa ili kuleta tija kwenye mradi huu.