Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

State Mining Corporation

State Mining Corporation

News

KAMISHNA WA MADINI AHIMIZA UAMINIFU NA UTUNZAJI WA SIRI MAHALI PA KAZI KWA WATUMISHI


Kamishna wa Madini kutoka Wizara ya Madini Dkt. Abdulrhaman Mwanga amewaagiza watumishi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuwa waaminifu na kuzingatia utunzaji wa siri za Shirika ili kuliletea maendeleo ya shirika hilo.

Ameyasema hayo wakati wa anafungua mkutano wa Kumi wa Baraza la Wafanyakazi wa STAMICO kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw Adolf Ndunguru, uliofanyika Januari 20, 2023 jijini Dodoma.

Dkt. Mwanga amewataka wana STAMICO kuongeza uwajibikaji na kushugulikia masuala yanayohusu Shirikia na watumishi sambamba na kuyapeleka mahali husika yale yote yaliyo nje ya uwezo ili yaweze kutafutiwa ufumbuzi na watu husika ili kuharakisha upatikanaji wa huduma.

Ameongeza kuwa ushirikiano na mawasiliano mazuri kazini ni chachu ya mafanikio kwani huwezesha watumishi kufanya kazi kwa tija.

Sambamba na hayo Dkt. Mwanga amewataka watumishi kutunza siri za Shirika na kuwa waaminifu katika kutekeleza majukumu yao ili kuleta maendeleo kwenye miradi kwa kuwa STAMICO ni Shirika linajihusisha na biashara.

"Ni vizuri tukakumbuka viapo na kanuni za kimaadili katika kutwkeleza wajibu wetu inavyotakiwa, tufanye kazi kwa bidii ili kuhakikisha malengo ya kuanzishwa kwa STAMICO yanafikiwa.

Naye Dkt. Venance Mwasse Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi STAMICO amewataka watumishi kutambua dhamana na umuhimu mkubwa walionao katika kuleta mafanikio ya Shirika.

Amewaomba wadau wa Shirika kuendelea kushirikiana na STAMICO kwa karibu ili kuliwezesha kutimiza malengo iliyojiwekea kwa wakati.

Akiongea kwa niaba ya watumishi wa STAMICO Bw. Mohamed Kaunya ametoa shukrani kwa Menejimenti ya STAMICO kwa kuendelea kutoa nafasi na kuwezesha kufanyika kwa baraza la wafanyakazi kwa wakati.

Ametumia fursa hiyo kuwaomba wajumbe wa baraza kutumia nafasi hii adhimu, kujadili Bajeti hiyo kikamilifu ili kuleta tija katika utekelezaji wa miradi ya Shirika.

STAMICO imefanya kikao cha kumi cha baraza ili kujadili bajeti ya utekelezaji wa miradi ya Shirika ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya Ushirikishwaji wa pamoja mahali pa kazi kwa mujibu wa Sheria ya utumishi wa umma na. 8 ya mwaka 2004 na kanuni zake za utumishi wa Umma za mwaka 2003.