News
"MAZINGIRA NI UHAI TUYATUNZE ILI YAJE YATUTUNZE SISI NA VIZAZI VYETU”
Hayo ni maneno yaliyosemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa(STAMICO) Dkt.Venance Mwasse wakati akiwahimiza wanawake kuendelea kutunza mazingira ikiwepo kupanda miti na kutumia Nishati Safi ya kupikia ya Rafiki Briquettes ili kuzuia mabadiliko ya tabia ya nchi yanayosababishwa na ukataji wa miti hovyo.
Dkt.Mwasse ameyasema katika eneo la Kiomoni Jijini Tanga wakati akishiriki zoezi la upandaji wa miti lililoandaliwa na kundi la wanawake na Samia Mkoa wa Tanga ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwepo matumizi ya mkaa safi na Salama uitwao Rafiki Briquettes. Katika zoezi hili zaidi ya miti 500 itapandwa .
Katika hafla hio fupi Dkt.Mwasse amewasisitiza wanawake hao kutunza misitu na kuzuia ukataji wa miti ili kuendelea kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan za kuendeleza ajenda ya matumizi ya nishati safi hapa nchini huku akiahidi kuwawezesha kiuchumi kwa kuwapatia upendeleo wa kuwa Mawakala wa Nishati Safi ya Rafiki Briquettes na kuwapatia Kontena moja ili kuweza kujikwamua kiuchumi kupitia Biashara.
Kwa nyakati tofauti Mwenyekiti wa Akina Mama na Samia mkoa wa Tanga B. Hamida Koja amemshukuru Dkt. Mwasse alimaarufu kama "Mjomba " kwa kuendelea kuwainua na kuwawezesha kiuchumi wanawake na Samia mkoa wa Tanga kwa kuwapatia Kontena hiyo itawapa chachu kufikia mafanikio.
Katika ziara hii Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt.Venance Mwasse amefanya uzinduzi wa zoezi la upandaji miti katika bonde la mto Pangani akiwa ameambatana na Afisa kutoka bonde la Mto Pangani ndugu Michael Busi, Mwenyekiti wa Akina Mama na Samia mkoa wa Tanga Hamida Koja , Mwenyekiti wa Mazingira Mkoa B.Mariam Mshana na Wilaya ya Tanga Juliana Kilumbi.