News
PAC YAKAGUA MGODI WA BUCKREEF MKOANI GEITA
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Japhet Hasunga (Mb) wametembelea na kukagua utekelezaji wa Shughuli za Mgodi wa Buckreef unaomilikiwa kwa Ubia baina ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) (45%) pamoja na Kampuni ya TRX Gold ltd (55%) uliopo Mkoa wa Geita.
Akizungumza mara baada ya kutembelea na kujionea shughuli za uchimbaji, uchenjuaji na maeneo ya utafiti, Mhe. Hasunga amesema Kamati imejione kazi kubwa na nzuri inayofanywa na thamani ya fedha za umma iliyowekezwa inaoneka.
“Kamati imekuja kuona namna fedha za umma zilivyotumika, je zimefanya kazi iliyokusudiwa na Bunge? Lakini pia kuangalia thamani ya hizo fedha imeleta nn katika Taifa? Nyinyi wote mmeshuhudia tumezunguka kuangalia mgodi mzima ambao wanashirikiana na hiyo kampuni ya nje lakini kazi kubwa na nzuri wameifanya katika kipindi cha miaka miwili na wameweza kupata faida ya Tsh. Bil. 45 hicho ni kitu ambacho kama Kamati tumekifurahia sana.” Amesema Mhe. Hasunga
Aliongeza kuwa Kamati pia imefurahishwa na namna ambavyo fedha za umma zilizowekezwa kwenye mgodi huo zimeleta ajira kwa Watanzania ambapo zaidi ya mia nne (400) jambo ambalo linaendana na Sera ya Nchi.
“Mmesikia katika taarifa yao karibu asilimia mia moja ya wafanyakazi kwenye mgodi huu ni Watanzania, hicho ni kitu kizuri na kinaendana na sera ya Nchi kuhakikisha watanzania wanapata ajira hasa vijana wetu” alisema
Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za mgodi Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt Venance Mwase amesema mgodi umewekeza zaidi ya shilingi bil.164 ambapo uwekezaji wake umehusisha ujenzi mabwawa,vifaa na mitambo ya uchenjuaji ambavyo vyote Kamati imevikagua na kwa sasa mgodi unazalisha tani 45 kwa saa na mpango uliopo ni kuongeza kufika tani 90 kwa saa jambo ambalo litaleta tija na kuongeza mapato zaidi kwa serikali.