Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

State Mining Corporation

State Mining Corporation

News

SHIRIKA LA MADINI LA TAIFA (STAMICO) LAFANYA MAZUNGUMZO NA SHIRIKA LA MADINI LA TAIFA INDONESIA (MIND ID)


Ujumbe wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Venance Bahati Mwasse leo tarehe 24/01/2024 umekutana na kufanya kikao na ujumbe wa Shirika la Madini la Taifa la Indonesia katika Hotel ya Sheraton jijini Jakarta nchini Indonesia. Katika kikao hicho masuala mbalimbali kuhusu uendelezaji wa kazi za utafiti wa madini katika leseni zinazomilikiwa na STAMICO yalijadiliwa.

Akiongea katika kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Venance B. Mwasse aliushukuru ujumbe wa MIND ID ukiongozwa na Makamu wa Rais ndugu Pandan kwa kukubali kutenga muda wa kufanya majadiliano na STAMICO ikiwa ni jitihada za kufanikisha utekelezaji wa hati ya makubaliano (MoU) iliyosainiwa na taasisi hizi mbili tarehe 22 Agosti, 2023, Ikulu jijini Dar es Salaam. Dkt Mwasse aliipongeza kamati ya watalaamu iliyoundwa kusimamia utekelezaji wa makubaliano (Joint Working Group) ikiwa na wajumbe kutoka pande zote kwa namna walivyoweza kuoiga hatua kubwa za utekelezaji ndani ya muda mfupi. Hata hivyo, Dkt. aliwataka wajumbe kuongeza kasi ya kufikia malengo yaliyokusudiwa na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa kamati kila mara kamati itakapohitaji msaada kutoka STAMICO.

Akiongea katika kikao hicho Makamu wa Rais wa MIND ID ndugu Pandan aliahidi kuwa MIND ID iko tayari kusimamia shughuli za utafiti wa madini hasa madini ya kimkakati yanayopatikana nchini Tanzania. Ndugu Pandan alikiri kuwa kwa kuanzia atafurahi kuona MIND ID ikifanya uwekezaji mkubwa kwenye uvunaji wa madini ya Kinywe (Graphite) yanayopatikana kusini mwa Tanzania mkoani Lindi. "Graphite inayopatikana mkoani Lindi nchini Tanzania ina ubora wa hali ya juu duniani hivyo MIND ID imevutiwa kufanya uwekezaji wa mapema katika madini hayo nchini Tanzania. Nae Meneja wa Utafiti wa Shirika la Madini la Taifa ndugu Fredrick Mangasini akichangia katika kikao hicho alieleza uwepo wa leseni za kutosha za madini ya kimkakati zinazomilikiwa na STAMICO. Ndugu Mangasini aliyataja madini ya kimkakati kuwa ni Lithium, Cobalt, Nickel, Iron Ore, Graphite, Tin na Shaba. Vilevile alieleza kuwa jiolojia ya Tanzania ni ya kipekee duniani kwani ina miamba yenye umri na maumbile mbalimbali ambayo ni chanzo cha kuwepo kwa aina nyingi za madini yapatikanayo duniani na baadhi yake yakipatikana Tanzania peke yake. Pia ndugu Mangasini alieleza namna ambavyo STAMICO imejipanga kuvutia fursa za uwekezaji kwenye madini kwa kuendelea kufanya tafiti nyingi kupitia vyazo vyake vya ndani pamoja na watalaamu wake. Mkakati huu unalenga kupata taarifa za kijiolojia za kutosha zitakazovutia uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya madini. Akihitimisha mazungumzo hayo mkuu wa kitengo cha utafiti cha MIND ID ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya utekelezaji wa hati ya makubaliano katika ya STAMICO na MIND ID ndugu Hasharik Kamaruddin alisema kuwa, anaridhishwa na mchango wa kila mjumbe wa kamati anayoiongoza ambapo yeye kama mwenyekiti ameendelea kupata ushirikiano wa karibu kutoka kwa wajumbe wote. Pamoja na shukrani hizo ndugu Kamaruddin alieleza dhamira ya kamati anayoiongoza ya kuhakikisha utafiti unafanyika hadi upeo wa juu (Advanced Exploration Stage) itakapofikia mwisho wa mwaka 2024. Ndugu Kamaruddin alihitimisha kwa kuutakia ujumbe wa STAMICO mafanikio katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji litakalofanyika siku ya tarehe 25/01/2024 katika Hotel ya Mulia jijini Jakarta ambapo mgeni rasmi atakuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kongamano hilo litawakutanisha kwa pamoja wafanyabiashara wa Tanzania na wafanyabiashara wa Indonesia kwa ajili ya kujenga mahusiano ya kibiashara na uwekezaji baina ya nchi hizi mbili.