News
STAMICO YANG'ARA MAONESHO YA MADINI
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) leo tarehe 12 Oktoba limeng'ara kwa kuzoa tuzo tatu katika maonesho ya madini yanayofanyika Mkoani Geita.
Tuzo hizo ni Mshindi wa Kwanza- Kampuni za UchImbaji wa Madini,Mshindi wa Kwanza-Makampuni Makubwa ya Uchorongaji na Mshindi wa Tatu kwa Udhamini wa maonesho haya.
Aidha,Kikundi cha Chama cha Wachimbaji Wanawake (TAWOMA) kimeshinda Tuzo ya Mshindi wa Kwanza-Wachimbaji Wadogo,Chama cha Wachimbaji Vijana (TYM) kimeshinda Tuzo ya Mshindi wa Pili-Wachimbaji Wadogo na Chama cha Wachimbaji Wanawake Mkoa wa Geita (GEWOMA) kimeshinda Tuzo ya Mshindi wa Tatu-Wachimbaji Wadogo.Vikundi hivi vimeshiriki kwenye "Kijiji cha STAMICO na Wadau Wake".
STAMICO imeshiriki katika maonesho haya kwa kutangaza huduma zake za uchorongaji kwenye migodi mikubwa ta GGML,Shanta Gold,Buckreef na mingine nchini.
Pia Shirika limeonesha nishati safi na salama ya kupikia ya Rafiki Briquettes ambayo imevutia wananchi wengi pamoja na huduma kwa wachimbaji wadogo.
Katika maonesho ya mwaka huu,STAMICO imewaleta pamoja wachimbaji wadogo,vikundi vya wanawake na wadau wengine kama vile watu wenye ualbino na wenye ulemavu wa kusikia.
Mpangilio wa washiriki kwa bidhaa mbalimbali kwenye sekta ya madini pia umevutia viongozi na wageni mbalimbali waliotembelea Kijiji cha STAMICO na wadau wake kwenye maonesho haya.
Vikundi ambavyo vimealikwa na STAMICO na kushiriki ndani ya banda moja ni pamoja na FEMATA,TAWOMA, TAMAVITA,FDH,Tanzania Youth Miners na Chama cha Wachimbaji Geita (GEREMA).
Wengine ni pamoja na kikundi cha Wanawake na Samia Geita na Chama cha Wanawake Geita (GEWOMA).
Wakati wa ziara yake kwenye Kijiji cha STAMICO na Wadau Wake leo,Naibu Waziri wa Madini,Dkt Steven Kiruswa alivutiwa na wazo la kuwaweka wadau wake pamoja.
Ameshauri uongozi wa Shirika uone uwezekano wa kuweka kijiji kama hiki wakati wa Maonesho ya Madini na Uwekezaji yatakayofanyika Dar es Salaam Novemba 19 hadi 21,mwaka huu.