Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

State Mining Corporation

State Mining Corporation

News

STAMICO YATOA FURSA ZA UWEKEZAJI WA KIBIASHARA KATIKA MNYORORO WA THAMANI WA MADINI, GEITA


Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeendelea kutoa fursa za uwekezaji wa kibiashara katika mnyororo wa thamani wa madini kupitia Mkaa Mbadala wa kupikia, Rafiki Briquette.


Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse wakati Mkuu wa Mkoa wa Geita Martin Shigella alipotembelea banda la STAMICO wakati maonesho ya tano ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.


Amesema STAMICO inajitahidi kushirikisha wananchi na wadau mbalimbali kuwekeza katika sekta ya madini, kupitia bidhaa hii mpya ya Rafiki Briquettes ili kila mdau mwenye nia na uwezo aweze kujipatia fursa ya kuwa wakala, aidha ametoa wito kwa wakazi wa Geita kuchangamkia fursa hii.


Naye Mkuu wa mkoa wa Geita Mhe. Shigella ameipongeza STAMICO kwa hatua hiyo na kutoa wito kwa wana Geita kuichangamkia fursa hii ambayo itatoa ajira na kuwaletea kipato na maendeleo ya kiuchumi.


Aidha katika Maonesho hayo Dkt. Mwasse alipata fursa ya kuwatembelea wadau na kuwashukuru kwa kushiriki kikamilifu katika kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Shirika yaliyofanyika mwezi Agosti 2022 mkoani Dodoma.


"Mwaka huu Shirika limefikisha miaka 50 huu ni umri mkubwa na kufika hapa sio jambo rahisi. Hivyo tunatambua mchango wa wadau wengine katika sekta ya madini ndio maana katika maonesho haya tumetumia fursa hii kuwatembelea na kuwapa zawadi ya kumbukumbu ya maadhimisho hayo ili kuthamini mchango wao kwa Shirika letu.


Amewataka wadau wote wa madini hususani wachimbaji wadogo kuendelea kushirikiana na Shirika wakati wote na kwamba lipo tayari wakati wote kutoa msaada wa kitaalamu ili kutatua changamoto za kiuchimbaji pale zinapotokea.


Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse amepokea cheti cha shukurani kutoka Chama cha Wasanii wa Mkoani Geita (TDFAA) kwa kutambua mchango wa Shirika katika kuwasaidia. Tukio hilo limetokea leo katika maonesho ya madini yanayofanyika Geita. Shirika liliweza kudhamini Mkutano Mkuu wa Chama hicho uliofanyika mwezi Mei mwaka huu.


Akizungumza alipokuwa akikabidhi cheti hicho Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji wa Filamu Mkoa wa Geita (TDFAA) Bi Rosemary Paul amesema kuwa wametoa chetu hicho kwa ajili ya kutambua mchango wa Shirika kwa jinsi waliyowaunga mkono katika mkutano wao.


"Tumekabidhi chetu hiki kwa Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO kwa mchango wake mkubwa wa kutambua na kuthamini shughuli tunazozifanya za sanaa hapa Mkoani kwetu"