Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

State Mining Corporation

State Mining Corporation

News

STAMICO YATUMIA BARAZA LA WAFANYAKAZI KUBORESHA MIRADI YAKE


*STAMICO yajivunia kuendelea kutekeleza miradi yake kwa ufanishi kwa kipindi cha nusu mwaka 2023/24*

*Dkt. Mwasse awaasa wafanyakazi kubuni vyanzo vipya ya kuongeza Mapato na Kuchapa kazi kwa bidii na kwa kushirikiana*

Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt. Venance Mwasse ameongoza Kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Shirika hilo kilichofanyika leo Januari 29, 2024 katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.

Kikao hicho kimelenga kujadili na kuboresha kwa pamoja utekelezaji wa miradi yake sambamba na kujadili maoteo ya bajeti ijayo ya mwaka 2024/2025.

Akifungua kikao hicho Dkt. Mwasse ameanza kwa kuainisha mafanikio ikiwemo ni pamoja na kusimika mitambo mikubwa miwili kwa ajili ya kuzalisha nishati mbadala wa kupikia, mitambo ya kusaga makaa ya mawe kwa ukubwa tofauti sambamba na kuleta mitambo mitano mipya ya uchorongaji kwa ajili ya wachimbaji wadogo ambayo imeanza kazi maeneo ya huko Nyamongo mkoani Mara.

Dkt. Mwasse amewaasa watumishi wote na wajumbe wa Baraza hilo kubuni vyanzo vipya ya kuongeza Mapato na kushiriki kikamilifu katika utendaji kazi kwa ufanisi na weledi ili kuhakikisha wanaendana na kasi ya sasa ya Shirika hilo.

"Kila mtumishi ashiriki kikamilifu kwenye utekelezaji wa majukumu yake kwa weledi na ushirikianao ili kurahisisha utendaji kazi na kuweza kuendelea kupiga hatua zaidi ya hapa tulipo". amesema Dkt. Mwasse.

Naye Tunukiwa Kavana, Mchumi wa STAMICO kwa niaba ya Meneja wa Mipango na Uwekezaji amewasilisha Taarifa ya mpango wa Bajeti ya Shirika hilo kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 kwa kila mradi na utekelezaji wake.

Aidha, ametumia fursa hiyo kuainisha vipau mbele vya Shirika ikiwa ni pamoja na kuendelea na uzalishaji mkubwa wa Makaa ya mawe, kuongeza uzalishaji wa mkaa mbadala wa (Rafiki Briquettes) kutokana na mtambo mikubwa iliyoletwa pamoja na kuimarisha huduma za uchorongaji.

Kwa upande wa Chama cha Wafanyakazi (TAMICO) kitaifa katibu wa ameipongeza STAMICO kwa mafanikio na kuongeza kuwa mafanikio haya yaende sambamba na maboresho ya hali za Uchumi za wafanyakazi ili kuzidi kuleta morali.

Aidha ndugu Mohamed Kaunya Mwenyekiti wa TAMICO tawi ka STAMICO, ameushukru uongozi wa STAMICO kwa kuendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi wake sambamba na kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano.

Katika Kikao hicho, watumishi na wajumbe wote wamepata fursa ya kujadili utekelezaji wa majukumu ya Shirika hilo ikiwa ni pamoja na kuendelea na uzalishaji mkubwa wa Makaa ya Mawe, Kuimarisha biashara ya uuzaji wa Kemikali za Madini na Vilipuzi, Kuimarisha huduma za Uchorongaji kwa kuongeza vifaa vya Uchorongaji na kutafuta kandarasi za muda mrefu.

# STAMICOkwa Manufaa kwa Umma

#Vision2030MadininiMaishanaUtajiri#