Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

State Mining Corporation

State Mining Corporation

News

USHIRIKI WA STAMICO – MKUTANO WA 91 WA PDAC


Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeshiriki kwenye Kongamano la 91 la Jumuiya ya Watafutaji wa Madini na Wawekezaji katika sekta ya madini nchini Kanada “Prospectus and Developers Association of Canada” (PDAC), Mkutano uliofanyika Jijini Toronto nchini Canada kuanzia tarehe 5-8 Machi 2023. Mkutano huu hufanyika kila mwaka ukijumuisha wataalamu mbalimbali katika sekta ya uchimbaji madini na wawekezaji katika sekta hiyo kwa lengo la kutambua fursa zilizopo, mchango wa teknolojia na kukutanisha wadau mbalimbali wenye nia ya kuwekeza katika utafutaji na uchimbaji wa madini.

Katika mkutano huo ulioandaliwa na PDAC, Tanzania imeshiriki kupitia mwamvuli wa kampuni ya MineAfrica Inc. Co. Ushiriki wa Tanzania umehusisha Wizara ya Madini pamoja na Taasisi zilizo chini yake ambazo ni Tume ya Madini, STAMICO na GST.

Kongamano hilo lilitanguliwa na mafunzo mbalimbali kuhusu uthamini, tathmini ya madini, uongezaji thamani wa madini, masuala ya mazingira, jamii na utawala bora (ESG) na teknolojia katika masuala ya uzalishaji madini. Mafunzo hayo yalifanyika kuanzia tarehe 2-4 Machi, 2023 ambapo washiriki kutoka Wizara ya Madini walipata fursa ya kujifunza kwa nyakati tofauti. Aidha katika kongamano hilo pia, Wizara na Taasisi zake zilipata nafasi ya kueleza fursa za uwekezaji kupitia Semina ya 21 ya Uwekezaji wa madini barani Afrika “21st Annual Investing in Africa Mining Seminar” ambapo Shirika la Madini liliwasilisha wasilisho kuhusu uwekezaji kwenye madini muhimu ya kimkakati “Invest with STAMICO in critical mineral”.

Akiwasilisha wasilisho hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa, CPA Dkt. Venance B. Mwasse alieleza wadau kuhusu madini muhimu ya kimkakati ambayo STAMICO ina leseni za utafiti (lithium, Graphite na Rare Earth Element (REE). Aidha, katika wasilisho lake, Dkt. Mwasse ameeleza kuwa kwa sasa shirika linatafuta wawekezaji katika madini hayo kwa kuwa ndio muelekeo wa dunia kuhusu uzalishaji wa madini yasio haribu mazingira (green energy minerals). Dkt. Mwasse ametoa rai kwa wawekezaji wenye nia na uwezo wa kufanya utafiti kuja nchini na kushirikiana na STAMICO katika utafiti na uendelezaji wa leseni hizo.

Aidha, Dkt. Mwasse ameeleza fursa nyingine za shirika akiitaja kwa uzito biashara ya Makaa ya Mawe na Rafiki Briquettes, huduma za uchorongaji na fursa ya utafutaji wa madini ya bati na dhahabu. Pamoja na wasilisho hilo, Wizara ya Madini iliwasilisha wasilisho kuhusu fursa za uwekezaji wa madini nchini Tanzania (Dkt. Abdul Mwanga) na GST iliwasilisha wasilisho kuhusu fursa za uwekezaji kwenye Jiolojia ya Tanzania (Dkt. Mussa D. Budeba).