Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

State Mining Corporation

State Mining Corporation

News

WANAWAKE STAMICO WATEMBELEA KIWANDA CHA MKAA MBADALA


Wafanyakazi wanawake kutoka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) wameunga mkono jitihada zinazofanywa na Shirika kuleta usawa katika kusimamia miradi yake kwa kutembelea kiwanda cha kuzalisha mkaa mbadala (Rafiki Briquette) kilichopo Mikocheni na baadaye kushiriki katika maandamano ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika viwanja vya Uhuru jijini Dar es Salaam.

Wakiongozwa na wahindisi wanawake wanaosimamia mradi huo, wanawake kutoka STAMICO wametembelea sehemu mbalimbali za kiwanda na kujionea jinsi mradi huo unavyofanya kazi kwa kutoa bidhaa bora zenye tija kwa wanawake na jamii kwa ujumla.

Mhandisi Happy Mbenyange alikuwa na haya ya kusema, "Ni furaha sana kwa wanawake wote wa STAMICO kusheherekea siku hii katika mtambo huu kwa kuwa bidhaa inayotoka hapa inakwenda kuwasaidia moja kwa moja kina mama na kuwapunguzia makali ya kupata nishati ya kupikia" Alisema.

Ameishukuru STAMICO kwa kuwapa nafasi wanawake ya kuonesha uwezo wao katika utendaji kazi bila ubaguzi wala upendeleo katika kutekeleza majukumu yao.

Katika maadhimisho hayo STAMICO imetoa pongezi kwa Serikali ya awamu ya Sita kwa jitihada za kuwawezesha Wanawake katika sekta mbalimbali na hususani kauli mbiu ya mwaka huu inasadifu yanayotekelezeka katika utendaji kazi wake.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mhandisi Mchenjuaji Madini kutoka STAMICO Pili Athumani kwa kusema kuwa STAMICO imezingatia hilo kwa kuwapa kipaumbele mwanawake na kutoa majukumu sawa na wanaume ili kutekeleza kauli mbiu ya Siku ya wanawake.

“STAMICO imekuwa miongoni mwa Taasisi ambazo zinazingatia misingi ya usawa katika kutekeleza majukumu yake na kuendesha miradi yake” alisisitiza.

Ameongeza kuwa katika sekta ya madini mwitikio wa wanawake umekuwa mkubwa katika shughuli zote za madini Wanawake wengi wamekuwa wakijitokeza na kujiajiri na kutumia fursa zilizomo.

STAMICO inaendelea kutoa nafasi sawa huku wakithamini mchango wa wanawake hivyo kuendana na kauli mbiu ya mwaka huu ambayo ni 'kizazi cha haki na usawa kwa maendeleo endelevu kwa jamii' katika Sekta ya Madini suala hili limepewa kipaumbele, kwani wanawake wamekuwa wanapewa kipaumbele.