Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

State Mining Corporation

State Mining Corporation

News

WAZIRI MAVUNDE AIPONGEZA STAMICO KUONGEZA UZALISHAJI WA MAKAA YA MAWE


Waziri wa Madini, Mhe Anthony Mavunde amelipongeza Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wa makaa ya mawe yanayochimbwa katika Mgodi wa Kiwira - Kabulo.

Mavunde ameyasema hayo Januari 19, 2024 Kiwira,Wilaya ya Ileje,Mkoani Songwe alipotembelea Mgodi wa Kiwira - Kabulo na mitambo ya kuchakata makaa ya mawe iliopo Ileje Mkoani Songwe na kuitaka STAMICO kusaidia uzalishaji wa umeme

"Ninawapongeza STAMICO kwa kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wa makaa ya mawe ambao utapelekea kuongezeka kwa mapato ya shirika kutoka wastani wa bilioni 1 hadi bilioni 4 kwa mwezi. Mgodi huu una hazina ya mashapo ya makaa ya mawe zaidi tani milioni 80 ambayo yakizalishwa kwa wingi ndani ya muda mfupi manufaa yake ni makubwa na kuitaka STAMICO kujipanga kuzalisha tani milioni 1 kwa mwaka ndani ya kipindi cha miaka miwili ijayo.

"Ni dhamira ya Mh. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuona nchi yetu inajitosheleza kwa nishati ya umeme.Hivyo, naiagiza STAMICO iende kuharakisha makubaliano mliyoingia na TANESCO na kukamilisha zile hatua muhimu za awali ili muanze mradi wa kuzalisha Megawati 200 za umeme kutoka kwenye makaa ya mawe.

Tanzania imejaaliwa rasilimali za kutosha na hivyo ni lazima tuzitumie kwa maendeleo yetu kama ambavyo makaa ya mawe haya yanavyoweza kutumika kama chanzo cha nishati badala ya kutegemea chanzo kimoja (energy mix) hivyo pamoja na TANESCO lakini pia fungueni milango kwa wadau mbalimbali wenye nia ya uzalishaji wa umeme ili kutimiza lengo hili," amesema Mavunde

Aidha, katika hatua nyingine Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO Meja Jenerali Mstaafu Michael Isamuhyo ameahidi kusimamia maelekezo ya Waziri Mavunde kwa uongozi wa STAMICO kuhakikisha ifikapo Februari 1, 2024 unaanza mara moja ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa ya Shule ya Msingi Kapeta ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa urejeshaji kwa jamii.

Awali, akitoa taarifa ya mradi wa makaa ya mawe Kiwira-Kabulo, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse alieleza kwamba Shirika kwa sasa limejipanga kutekeleza mikakati ya kulifanya liendelee kupata faida na kuendelea kuongeza mapato

Awali, akitoa taarifa ya mradi wa makaa ya mawe Kiwira-Kabulo, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse alieleza kwamba Shirika kwa sasa limejipanga kutekeleza mikakati ya kulifanya liendelee kupata faida na kuendelea kuongeza mapato ya Serikali kupitia Mrabaha, ada mbalimbali na gawio kwa Serikali ambapo kwa sasa wamewekeza zaidi ya Shilingi Bilioni 9 kwa ajili ya ununuzi wa mitambo na vifaa vya uzalishaji.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Mhe. Farida Mgomi amesema Mh.Rais Samia ametoa zaidi ya Shilingi Bilioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 5 kutoka eneo la machimbo mpaka Mgodini Kiwira ambapo awali walikuwa wanazunguka kwa kutumia kilomita zaidi ya 70 kutoa makaa ya mawe kwenda kuchakatwa katika eneo la Mgodi wa Kiwira.