News
ZIARA YA MD STAMICO YAMWAGA NEEMA TAWOMA TANGA, AWAKUTANISHA NA KIWANDA CHA NEELKANTH WAPATA SOKO LA UHAKIKA TANI ZAIDI YA 200 KWA SIKU
*Wachimbaji Wanawake Mkoa wa Tanga sasa kuuza Madini ya Limestone Kiwanda cha Neelkanth Lime Mkoani Tanga*
*Mkurugenzi Mtendaji afanya kikao na Uongozi wa Kiwanda kuhusu kuwawezesha Wachimbaji Wadogo Wanawake kupata soko la Madini ya Dolomite, Limestone na Calcite
Katika kuhakikisha Wachimbaji Madini Wanawake mkoa wa Tanga wananufaika na raslimali ya madini ya viwandani wanayoyachimba leo tarehe *16 Agosti, 2024* Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt.Venance Mwasse akiwa ameambatana na Mwenyekiti wa Wachimbaji Madini Wanawake mkoa wa Tanga(TAWOMA) Bi. Mariam Mshana sambamba na Kaimu Afisa Madini Mkazi mkoa wa Tanga Mhandisi Jackson Shirima wamekutana na kufanya mazungumzo na Meneja Mkuu wa kampuni ya Neelkanth Lime Ltd yenye makazi yake Kiomoni Jijini Tanga ndugu Benny P. Pathrose.
Katika kikao hicho Dkt Mwasse ameeleza dhamira ya Serikali na Shirika ni kuona Wachimbaji Wadogo wa Madini hasa Wanawake wananufaika na shughuli ya uchimbaji ili kujikwamua kiuchumi lakini katika mkoa wa Tanga hali ni tofauti kutoka na Wachimbaji hawa kupata changamoto ya kulifikia soko la kiwandani moja kwa moja na hivyo kusababisha kunyonywa na wanunuzi wa kati. Katika utatuzi wa changamoto hiyo Dkt. Mwasse amewaomba Uongozi wa Kiwanda hicho kuwapa nafasi hawa wachimbaji wanawake ili waweze kuuza Madini wanayoyachimba (Limestone, Dolomite na Calcite) kiwandani hapo.
Mkurugenzi Dkt. Mwasse alimweleza Meneja huyo kuwa Serikali kupitia *Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hasan* Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inafanya juhudi za makusudi katika kumwezesha mwanamke aweze kujikombao kupitia shuhuli mbalimbali za kiuchumi hususani uchimbaji wa madini. Hii inatekelezwa kupitia *slogan ya 4R.* Mkurugenzi aliendelea kusema idadi ya kwa mujibu ya takwimu za Sensa ya watu ya makazi kwa Mwaka 2022 ilionesha ni zaidi ya Asilimia Hamsini (50%) hivyo kumuwezesha mwanamke ni kuwezesha jamii ya Watanzania. Hivyo STAMICO na Neelkant wakifanya kazi kwa pamoja kuwawezesha Wanawake italeta mapinduzi makubwa katika kuboresha maisha ya jamii ya watanzania.
Naye Meneja Mkuu wa Kiwanda Bw. Pathrose ameeleza shughuli mbalimbali zinazofanyika hapo kiwandani na fursa zilizopo za kufanya biashara za Madini hususani Madini viwanda,mwishoni alimalizia kwa kupokea kwa uzito changamoto zilizoelezwa na ombi maalum kutoka kwa Mkurugenzi wa STAMICO na hivyo ametoa nafasi ya upendeleo kwa wanawake wachimbaji Madini mkoa wa Tanga(TAWOMA) wa kuuza *Tani Mia Mbili (200) kwa siku za Madini ya Chokaa.*
Aidha katika kuitikia wito wa STAMICO Kampuni itakuwa ikilipa malipo ya Mirabaha yote kwa niaba ya Wanawake Wachimbaji watakaouza madini kiwandani hapo.
Akizungumza katika kikao hicho *Mwenyekiti wa Wachimbaji Madini Wanawake mkoa wa Tanga* Bi. Mariam Mshana amesema wamepokea kwa furaha nafasi hiyo waliyoipata ya kuuza Madini ya Chokaa kiwandani moja kwa moja kwani itawawezesha kujiongezea kipato maradufu tofauti na hapo awali walikuwa wanapunjwa kupitia madalali. Bi. Mshana ameushukuru uongozi wa STAMICO kupitia Dkt. Mwasse kuwawezesha kupata soko la moja kwa moja kiwandani hii inaonesha dhamira ya dhati ya Shirika kuwa Walezi wa Wachimbaji Wadogo hapa nchini kwani tayari wamepatia vifaa vya uchimbaji na hivi karibuni kitafunguliwa kituo cha kuuza baruti hivyo kuwawezesha kupata kwa bei nafuu na kwa urahisi kuliko sasa.
Mwishoni Dkt. Mwasse ameishuru kampuni ya Neelkanth Lime Ltd kupitia Meneja wake kwa namna alivyoitatua changamoto ya soko la Madini ya viwandani kwa Wachimbaji Wadogo na kuahidi kufanya nawe kazi kwa pamoja kwa maendeleo ya sekta ya Madini.
*Hii ni mwendelezo wa ziara za Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO kusikiliza changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo na kuzitafutia ufumbuzi azazofanya maeneo mbalimbali hapa nchini.*