Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Madini la Taifa

KAMATI YA BUNGE YA KUDUMU YA NISHATI NA MADINI YAIPONGEZA STAMICO KWA UBUNIFU KATIKA MATUMIZI YA NISHATI SAFI

Imewekwa: 13 March, 2026
KAMATI YA BUNGE YA KUDUMU YA NISHATI NA MADINI YAIPONGEZA STAMICO KWA UBUNIFU KATIKA MATUMIZI YA NISHATI SAFI

Serikali imejipanga kuhakikisha matumizi ya Nishati safi yanaongezeka katika Mkoa wa Tabora kufuatia kufunguliwa kwa Kiwanda cha kuzalisha Nishati safi ya kupikia ya Rafiki Briquettes inayozalishwa na STAMICO chenye uwezo wa kuzalisha tani 20 kwa saa.

Hayo yameelezwa leo tarehe 12 Machi, 2026 Mkoani Tabora na Dkt. Steven Kiruswa , Naibu Waziri wa Madini wakati akitoa taarifa kwa kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilipokuwa ikikagua miradi inayosimamiwa na Wizara ya Madini.

Dkt. Kiruswa amesema kuwa, STAMICO  tayari imeshanunua mitambo minne yenye uwezo wa kuzalisha tani 20 ya Nishati hiyo kwa saa. Mitambo hiyo tayari imeshasimikwa katika maeneo ya Kiwira Mkoani Songwe, Visegese Mkoani Pwani katika Wilaya ya Kisarawe, Chigongwe Mkoani Dodoma na Kiloleni Mkoani Tabora.

Dkt. Kiruswa amefafanua kuwa, kwa Mkoa wa Tabora, STAMICO imelenga kuhamasisha matumizi ya Nishati safi kwa wakulima wa Tumbaku ambao wamekuwa wakitumia kuni kwa wingi kwa ajili ya ukaushaji wa Tumbaku. Pia Shirika limezilenga Taasisi mbalimbali za Mkoa huo pamoja na watu binafsi.

Kwa upande wake Mhe. Subira Mgalu, Mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya kudumu ya Nishati na Madini ameipongeza STAMICO  kwa ubunifu wa miradi endelevu ambayo inaleta mchango mkubwa kwa Taifa ambao unaunganisha mnyororo mzima wa thamani Madini.

Mhe. Mgalu ameitaka STAMICO kupitia mradi wa Rafiki Briquettes kuhakikisha unafika Mikoa mbalimbali Nchini ili kutekeleza Agenda ya Kitaifa inayohusu matumizi ya Nishati safi na utunzaji wa Mazingira ndani ya Sekta ya Madini.

Kwa upande wake Mhe. Msafiri Mbibo , Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini, ameishukuru kamati kwa maoni mbalimbali yaliyolenga uboreshaji wa mradi huo hususani katika upande wa ajira na usimikaji wa mitambo ya uzalishaji.

Awali akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi huo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Ndg, Deusdedith Magala amesema kuwa, mradi wa Rafiki Briquettes unatarajia kuzalisha ajira kwa Watanzania wengi katika Mikoa mbalimbali.

STAMICO imejipanga kuendelea kuwa kinara wa kutekeleza Agenda ya Serikali ya awamu ya sita katika kuhamasisha matumizi ya Nishati safi.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo