Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Madini la Taifa

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI YARIDHISHWA NA KITUO CHA MFANO CHA LWAMGASA

Imewekwa: 19 March, 2026
KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI YARIDHISHWA NA KITUO CHA MFANO CHA LWAMGASA

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeonyesha kuridhishwa na utaalamu wa mafunzo ya uchimbaji wa kisasa unaotelewa katika kituo cha mfano cha Lwamgasa kilicho chini ya Shirika la Madini la Taifa ( STAMICO ) kilichopo Mkoani Geita.

Hayo yameongelewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Subira Mgalu wakati kamati hiyo ilipofanya ziara ya kutembelea kituo hicho tarehe 16 Machi, 2026

Akizungumza baada ya ukaguzi wa kituo hicho, Mhe. Mgalu amekisifu kituo hicho kwa kuwa sehemu muhimu katika kuleta mapinduzi ya teknolojia kutoka uchimbaji wa mazoea Kwenda kwenye uchimbaji wa kisasa na wenye tija.

Mhe. Mgalu amesema kuwa, utaalamu unaotolewa na kituo hicho unawasaidia wachimbaji wadogo kuongeza kiwango cha Dhahabu wanayopata kutoka asilimia 30 hadi kufikia zaidi ya asilimia 80.

Ameongeza kuwa, kituo hicho kimekuwa kielelezo kizuri cha namna Serikali kupitia Wizara ya Madini na Shirika la Madini la Taifa inavyowezesha wachimbaji wadogo kupata vifaa vya kisasa na utaalamu wa kimaabara kwa gharama nafuu.

Kwa upande wake Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa, Sekta ya Madini inasimamia miradi ya kimkakati ambayo lengo lake kubwa ni kutoa huduma kwa wachimbaji wadogo ikiwemo uchorongaji wa miamba na uchenjuwaji bora kupitia teknolojia ya CIP. Aidha Mhe. Mavunde ameahidi kuwa, maoni yote yaliyotolewa na kamati hiyo yatafanyiwa kazi.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa STAMICO Bw. Deusdedith Magala ameifahamisha kamati hiyo kuwa, kituo hicho kimekuwa kikitoa mafunzo ya vitendo kwa vikundi mbalimbali vya wachimbaji, jambo ambalo limesaidia kuongezeka kwa uelewa kwa wachimbaji, kupunguza ajali migodini na kuongeza mapato Serikalini kupitia Mrahaba.

Kamati hiyo imehitimisha ziara yake kwa kuitaka Wizara ya Madini kuongeza vituo vingine kama hicho katika kanda nyingine za Madini nchini ili kuwafikia wachimbaji wengi zaidi na kuchochea ukuaji wa Sekta ya Madini.

Katika ziara hiyo Mhe. Mavunde aliambatana na Mh. Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa na wataalamu mbalimbali kutoka Wizara ya Madini.

STAMICO inaendelea kuwa kinara kwa kutumia teknolojia za kisasa katika miradi yake ili kuleta tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo