BODI YA STAMICO YAKAGUA MIRADI YA SHIRIKA CHIGONGWE
Katika hatua inayofungua ukurasa mpya wa usimamizi wa rasilimali na miradi ya kimkakati, Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) leo tarehe 30/7/2026 imefanya ziara yake ya kwanza ku kagua Kiwanda Kipya cha Nishati Safi pamoja na Karasha la Kokoto katika eneo la Chigongwe, Jijini Dodoma, na kueleza kuridhishwa kwake na kasi ya uendeshaji.
Akiwasilisha taarifa ya uwekezaji huo, Mkurugenzi wa Migodi na Huduma za Kihandisi, Mhandisi Baraka Manyama, ameiambia Bodi kuwa STAMICO imewekeza kwenye mitambo ya kisasa yenye uwezo wa kuzalisha kati ya Tani 150 hadi 200 kwa saa na wenye uwezo wa kuzalisha kokoto za aina zote kulingana na mahitaji ya soko.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi, Makamu Mwenyekiti Dkt. Wilison Mutagavwa, alionyesha kuridhishwa na miundombinu hiyo na kutoa maelekezo ya kimkakati kwa Menejimenti kuongeza kasi ili STAMICO itawale soko la ujenzi linalokua kwa kasi jijini Dodoma na Mikoa jirani.
Katika ziara hiyo ya kwanza ya Bodi, wajumbe pia walikagua Kiwanda cha Nishati Safi cha *Rafiki Briquettes* ambapo walijionea maendeleo makubwa. Jengo la kiwanda limekamilika kwa asilimia 100, mitambo yote imesimikwa, na hivi sasa ipo kwenye hatua ya majaribio ya mwisho kabla ya kuzinduliwa rasmi.
Dkt. Mutagavwa aliitaka Menejimenti kuweka mipango thabiti ya masoko ili bidhaa hizo mbili—Kokoto na Nishati ya *Rafiki Briquettes ziwafikie wananchi wengi zaidi kwa haraka.
STAMICO inaendelea kuonyesha mfano wa ufanisi katika usimamizi wa miradi ya umma, ikilenga kuongeza mapato ya Shirika huku ikitengeneza fursa nyingi za ajira kwa wananchi wanaozunguka miradi hiyo.