BODI YA WAKURUGENZI STAMICO YARIDHISHWA NA UTENDAJI WA KIWANDA CHA RAFIKI BRIQUETTES KISARAWE
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Mhe. Balozi IGP Mstaafu, Simon Nyakoro Sirro, akiwa pamoja na Wajumbe wa Bodi, wametembelea Kiwanda cha Rafiki Briquettes kilichopo Kisarawe mkoani Pwani leo tarehe 8 Juni 2026 na kueleza kuridhishwa kwao na maendeleo pamoja na utendaji kazi wa kiwanda hicho.
Katika ziara hiyo, wajumbe wa Bodi walipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya uzalishaji, kujionea teknolojia inayotumika katika uzalishaji wa Nishati Safi ya Rafiki Briquettes na kupokea taarifa ya maendeleo ya kiwanda pamoja na mchango wake katika kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya kupikia nchini.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Balozi Sirro, amepongeza juhudi zinazofanywa na Menejimenti pamoja na wafanyakazi wa kiwanda hicho kwa kuendelea kuzalisha bidhaa bora zinazokidhi mahitaji ya soko na kuchangia jitihada za Serikali za kulinda mazingira na kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya kupikia.
Aidha, Mhe Balozi Sirro amesisitiza umuhimu wa wananchi kuchangamkia fursa ya matumizi ya Rafiki Briquettes kutokana na manufaa yake mbalimbali, ikiwemo kuwa Nishati safi, salama kwa mazingira na yenye ufanisi mkubwa katika matumizi. Ameeleza kuwa bidhaa hiyo hutumia kiasi kidogo cha nishati katika kuandaa chakula, hivyo kusaidia watumiaji kupunguza gharama za matumizi ya nishati huku ikichangia juhudi za uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dkt. Venance Mwasse, alielezea chimbuko la mradi wa Rafiki Briquettes na umuhimu wake katika kuunga mkono ajenda ya Taifa ya matumizi ya Nishati Safi ya kupikia. Alifafanua kuwa mradi huo ulianzishwa na STAMICO kwa lengo la kutoa suluhisho la nishati mbadala ya kupikia ili kuepukana na Nishati ambazo sio safi na salama.
Dkt. Mwasse aliongeza kuwa, Shirika limefanya uwekezaji mkubwa katika ujenzi na maendeleo ya Kiwanda cha Rafiki Briquettes, ikiwemo ununuzi wa mitambo ya kisasa, uboreshaji wa miundombinu ya uzalishaji na kuimarisha mifumo ya uendeshaji wa kiwanda.
Alibainisha kuwa uwekezaji huo umeongeza uwezo wa uzalishaji wa kiwanda, umeimarisha ubora wa bidhaa na kuwezesha Rafiki Briquettes kuendelea kuwa miongoni mwa suluhisho muhimu katika utekelezaji wa mkakati wa Taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kiwanda cha Rafiki Briquettes, Mha. Happy Mbenyange, aliieleza Bodi historia ya kiwanda hicho tangu kuanzishwa kwake hadi kuanza kwa uzalishaji wa Rafiki Briquettes.
Alibainisha kuwa kiwanda hicho kimeendelea kukua na kuimarika katika uzalishaji wa nishati safi ya kupikia, hatua inayochangia upatikanaji wa bidhaa bora sokoni na kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini.
Aidha, Bodi imehimiza kuongeza uzalishaji wa Rafiki Briquettes ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya bidhaa hiyo nchini, pamoja na kuendelea kutafuta masoko mapya ndani na nje ya nchi yatakayoongeza ushindani na mapato ya Shirika.
Bodi ya Wakurugenzi ya STAMICO imeeleza kuwa mafanikio ya Rafiki Briquettes ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa mkakati wa Shirika wa kuendeleza bidhaa zenye thamani, kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda na kuunga mkono ajenda ya Taifa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.
STAMICO itaendelea kuimarisha uwekezaji katika miradi yake ya kimkakati ili kuongeza tija, ajira na mchango katika maendeleo ya Taifa.