Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Madini la Taifa

BODI YA WAKURUGENZI STAMICO YAZINDULIWA RASMI

Imewekwa: 14 April, 2026
BODI YA WAKURUGENZI STAMICO YAZINDULIWA RASMI

Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde leo tarehe 14 Aprili, 2026 amezindua Bodi ya Shirika la Madini la Taifa ( STAMICO ) na kuielekeza Bodi hiyo kusimamia mchakato wa uanzishwaji wa Kampuni tanzu chini ya STAMICO kusimamia leseni zote zinazorejeshwa na Serikali ili ziendelezwe kwa ufanisi zaidi.

Uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa Tume ya Madini jijini Dodoma ambapo Mhe. Mavunde alikuwa Mgeni Rasmi.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mhe. Mavunde alianza kwa kumpongeza Mwenyekiti wa Bodi hiyo na Wajumbe wapya wa Bodi hiyo kwa kuaminiwa na akawaelekeza kulisimamia Shirika la Madini la Taifa ( STAMICO ) ili liweze kuwa kama makampuni makubwa ya uchimbaji.

Mhe. Mavunde amesema kuwa, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza kuwa, leseni zote kubwa ambazo Serikali ililipa fidia katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi zinarejeshwa STAMICO. Maono ya Wizara ni kuona STAMICO inakuwa Shirika kubwa zaidi kwenye mapato, uwezo na rasilimali ili liweze kushindana na makampuni makubwa ya uchimbaji.

Pia Mhe. Mavunde ameitaka Bodi kuhakikisha kuwa, STAMICO inarejea tena na kuzidi ukubwa iliyokuwa nao miaka ya 90 na ndio maana wana kauli mbiu mpya ya MASTASHA kwa maana ya Make Stamico Shine Again yaani kuifanya STAMICO ing’are tena.

Awali Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa aliipongeza Bodi na kuahidi kuipa ushirikiano mkubwa na akawaambia milango yake yeye na Mhe. Waziri ipo wazi muda wote kwa msaada wowote watakaouhitaji.

Naye katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahaya Samamba ameipongeza Bodi hiyo na kuisisitiza kusimamia mchakato wa kuhakikisha nafasi zote ambazo hazijajazwa au zina watu wanaokaimu kwa muda mrefu zijazwe kwa haraka.

Awali akifanya mawasilisho kuhusiana na Shirika, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse aliwaeleza Wajumbe hao wa Bodi kuhusu Shirika lilipotoka na changamoto zote ambazo limepitia mpaka lilipofika hapa.

Dkt. Mwasse alisema kuwa, STAMICO ilianzishwa Mwaka 1972 kwa lengo la kuwekeza kwa niaba ya Serikali kwenye mnyororo mzima wa Sekta ya  Madini. Lengo hilo ndio linaloifanya STAMICO iwe Shirika muhimu na la kimkakati.

Aliongeza kwamba, STAMICO imejipanga kuendelea kuwa Shirika la mfano linalojiendesha kwa faida na tija.

Akitoa neno la shukrani baada ya uzinduzi wa Bodi hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO IGP Mstaafu Mhe. Balozi Simon Sirro ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma amesema, wao wameaminiwa kwa kupatiwa heshima hii na watahakikisha pale wengine walipoishia ndio waanzie na kuhakikisha wanalipeleka Shirika mbele zaidi.

STAMICO chini ya Bodi mpya imejipanga kuhakikisha Shirika linakuwa kubwa zaidi na la mfano kwa Mashirika mengine.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo