Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

State Mining Corporation

State Mining Corporation

News

WAZIRI MKUU AIPONGEZA STAMICO KUENDELEA KUNADI MATUMIZI YA NISHATI MBADALA


Waziri Mkuu Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa amelipongeza Shirika la Madini la Taifa STAMICO kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati Mbadala kwa wananchi.

Amesema STAMICO imetumia fursa nzuri kwa kuungana na Wahiriri katika Mkutano wao wa Mwaka kuhamasisha matumizi ya Nishati ya Rafiki Briquette ili kuokoa mazingira.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Novemba 13, 2023 kwenye Mkutano Mkuu wa Saba wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), unaofanyika kwa siku tatu Mkoani Lindi.

Amesema kuwa STAMICO imejipambanua katika kuhakikisha inaleta nishati mbadala , kwa kuwa nishati hiyo itaokoa miti mingi inayotumika kutengeneza mkaa.

"Mmetumia Jukwaa sahihi kufanya hamasa ya mkaa huu, niwapongeze sana kwa jinsi mlivyojitahidi kuleta mkaa utokanao na mabaki ya mkaa utakaozuia ukataji wa miti mingi kwa kuzalisha mkaa kidogo" Amesisitiza Mhe Waziri Mkuu.

Akiongea kwa niaba ya STAMICO Afisa Masoko wa STAMICO Bw Mark Stephano amesema Shirika limejipanga vyema kuhakikisha nishati hiyo inasambaa katika maeneo mengi nchini Tanzania ikiwemo mkoa wa Lindi.

"Tayari Shirika limeleta na kuifunga Mitambo mikubwa miwili ya kuzalisha Mkaa wa Rafiki Briquettes yenye uwezo wa kuzalisha mkaa tani 20 kwa saa, ambayo imefungwa katika mkoa wa Pwani na Songwe eneo la Kiwira" amesema Stephano.

Jukwaa la Wahariri Tanzania limekutana Mkoani lindi katika Mkutano wake Mkuu wa saba tangu kuanzishwa kwake wenye kaulimbiu isemayo 'Uandishi wa Habari, Gesi na Uchumi Endelevu kwa Nchi.