Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

State Mining Corporation

State Mining Corporation

News

STAMICO SHANTA GOLD ZASAINI MKATABA MNONO WA UCHORONGAJI


Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Kampuni ya uchimbaji wa dhahabu Shanta Gold Mine leo Februari 16, 2024 zimesaini mkataba wa kandarasi ya uchorongaji miamba yenye thamani ya dola za Marekani milioni 1.08 sawa na sh bilioni 2.7 kama sehemu ya uendelezaji wa mageuzi yanayoendelea kufanywa na shirika hilo kwenye shughuli za uchorongaji.

Utiaji saini wa mkataba huo umefanyika jijini Dodoma nchini Tanzania na utadumu kwa kipindi cha miezi sita na utahusisha shughuli za uchorongaji kwa ajili ya utafiti wa madini.

Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse amesema kuwa makubaliano ya kandarasi hiyo yamefunguwa njia kwa STAMICO kuingia rasmi kanda ya kati na hasa Mkoa wa Singida, kabla ya kusaini kandarasi zingine za uchorongaji Mkoani Dodoma kupitia kampuni ya Geita Greenfields Minerals Exploration Company Ltd.

“Kandarasi hii ni miezi sita na ina thamani ya dola milioni 1.08 sawa na bilioni 2.7, kandarasi amabayo sisi tunaheshimu na kupitia kandarasi hii sisi tunawahakikishia kuwapatia huduma stahili” Alisema Dkt. Mwasse

Kwa upande wake Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa SHANTA GOLD Mhandisi Honest Mrema amesema licha ya kuwa wameanza na kandarasi ya miezi sita, shauku yao kubwa ni kupanua zaidi baadhi maeneo ya utafiti na uchimbaji Mkoani Singida kwa sababu STAMICO imeonesha utayari wa kufanya nao kazi kwa ufanisi.

Ameeleza kuwa ikiwa STAMICO itafuata ufanisi wa makubaliano hayo wanaweza tena kusaini makubaliano mengine.

" Kama STAMICO itafuata ufanisi wa makubaliano haya, naamini tutakuja tena kukaa hapa na kusaini kandarasi nyingine” Aliongeza.

Hata hivyo aliongeza kuwa maeneo ya uchimbaji yaliopo Singida ni mengi na mazuri kwa uzalishaji na wanaamini mkataba uliosainiwa leo ni mwanzo wa mashirikiano ya muda mrefu zaidi na Mashirikiano hayo yakiendelea wanaweza kuvuka lengo la Serikali kupitia STAMICO kwa kununua vifaa vya kisasa.

“Napenda kumuhakikishia Mkurugenzi kwamba tuna malengo ya kuendeleza sekta ya madini nchini na kufikia malengo ya serikali kwani tunaamini Tanzania ina rasilimiali za kutosha” Alisema.