Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Madini la Taifa

STAMICO KUFUNGUA KIWANDA KINGINE CHA KUZALISHA NISHATI SAFI YA KUPIKIA YA RAFIKI BRIQUETTES MKOANI TABORA

Imewekwa: 27 January, 2026
STAMICO KUFUNGUA KIWANDA KINGINE CHA KUZALISHA NISHATI SAFI YA KUPIKIA YA RAFIKI BRIQUETTES MKOANI TABORA

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dkt. Venance Mwasse leo tarehe 24 Januari, 2026, amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya Kiwanda kipya kinachotarajiwa kuanza uzalishaji wa Nishati safi ya kupikia ya Rafiki Briquettes hivi karibuni. Kiwanda hicho kipo katika Mkoa wa Tabora.

Katika ziara hiyo, Dkt. Mwasse alikagua Kiwanda na kuangalia maeneo madogo madogo ambayo yalikuwa katika hatua za mwisho za kukamilishwa kwake. Kwa ujumla, Dkt. Mwasse aliridhishwa na kazi ambayo imefanyika mpaka sasa.

Ameelekeza maeneo ambayo yalikuwa bado kukamilika basi yakamilike kwa haraka ili Kiwanda kiweze kuanza uzalishaji ndani ya siku 100 za Uongozi wa awamu ya pili ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza na mafundi na baadhi ya wafanyakazi waliokuwepo katika ukaguzi huo, Dkt. Mwasse alisema kuwa, Kiwanda hiki kitakuwa suluhisho kubwa kwa kuzalisha Nishati safi ya Rafiki Briquettes ambayo ina ufanisi mzuri wa kukausha Tumbaku.

Aliongeza kwamba, uwepo wa Kiwanda hiki utakuwa mwarobaini wa changamoto zote ambazo wakulima wa Tumbaku wamekuwa wakikutana nazo kwa kutafuta Nishati sahihi ya kukaushia Tumbaku yao. Kiwanda hiki pia kitaleta fursa ya ajira kwa Vijana na kitakuwa chachu ya kuinua hali ya maisha kwa wakazi wa Tabora.

Alimalizia kwa kusema kuwa, uwepo wa Kiwanda hiki utapunguza ukataji wa miti kwa kiasi kikubwa katika Mkoa wa Tabora na maeneo yanayoizunguka.

STAMICO inaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha Watanzania wanatumia Nishati safi ili kufikia lengo la asilimia 80 kufikia Mwaka 2034.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo