News
STAMICO YAELEZA MIKAKATI YAKE KATIKA KUSHIRIKI NA KUTIMIZA VISION 2030- MADINI NI MAISHA NA UTAJIRI
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeweka bayana namna lilivyojipambanua kuhakikisha watanzania wanashiriki katika uvunaji wa rasilimali madini kupitia kazi mbalimbali zinazofanyika katika mnyororo mzima wa thamani wa Madini.
Akizungumza hayo wakati wa kipindi cha Good Morning kinachorushwa na redio na Mitandao ya Jamii ya Wasafi Media leo Novemba 9 jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse amesema Shirika limefanya mageuzi makubwa katika miradi yake ili kuhakikisha sekta ya madini inawanufaisha watanzania.
Amesema STAMICO imeboresha uendeshaji wa miradi yake na kuifanya kuwa sehemu ya kukusanya mapato na sio sio matumizi jambo lilipelekea kuongezeka kwa mapato ya Shirika kutoka Bilioni 1.31 hadi kufikia Bilioni 61.8 kwa mwaka 2022/2023 .
Amesema sekta ya madini inazo fursa nyingi ambazo zinawataka watanzania kuchukua hatua na kushiriki kwa vitendo katika shughuli hizo za uchimbaji ili kuweza kupata tija.
Amesema kupitia shughuli za uchorongaji STAMICO inawaajili vijana hata wale wenye ujuzi tu ili waweze kufanya kazi kwa kutumia ujuzi wao.
"STAMICO imewaajiri vijana wengi kupitia mradi wa uchorongaji ili kuhakikisha haiwaachi nyuma katika kushiriki kwenye fursa za sekta ya Madini", amesema Dkt. Mwasse.
Aidha, amesema STAMICO imeendelea kuchangamkia fursa ya kuwekeza katika Madini ya Kimkakati kwa kuchukua leseni za madini hayo ili kwenda na kasi ya mabadiliko ya Dunia ambapo inachagiza matumizi ya Nnshati safi ili kuokoa mazingira.
Ameendelea kusema STAMICO imechagiza kuanzishwa kwa kiwanda cha Kusafisha Dhahabu cha Mwanza Refinery Precious Metals Co. Ltd ambacho kimechochea kwa kiasi kikubwa ongezeko la thamani ya madini yetu, ajira kwa Watanzania sambamba na kuleta teknolojia mpya kwa watanzania.
"kupitia miradi ya ubia STAMICO inahakikisha miradi hiyo inarithisha teknolojia na kutoa ajira kwa Watanzania" Dkt.Mwasse
Pamoja na hayo STAMICO haijawaacha nyuma Wachimbaji Wadogo ambapo imeendelea kutoa elimu ya teknolojia kwa vitendo sambamba na kuongeza Kituo cha Umahili cha mfano kwa ajili ya wachimbaji wa chumvi mkoani Lindi ili kuhakikisha wanazalisha chumvi yenye ubora kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.
Kwa upande mwingine, STAMICO imeendelea kutafuta suluhisho dhidi ya changamoto ya upatikanaji wa mikopo kwa Wachimbaji Wadogo na kuelezea,
"STAMICO imedhamiria kuleta suluhisho la kudumu la upatikanaji wa Mikopo kwa Wachimbaji Wadogo kwa kuhakikisha inasimamia kuanzishwa kwa Benki ya wachimbaji ambapo taratibu za kuanzishwa kwa benki hiyo zimeshaanza kufuatiliwa".