Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

State Mining Corporation

State Mining Corporation

News

MD STAMICO ATOA DARASA KWA UJUMBE WA SHIRIKA LA MADINI LA TAIFA LA UGANDA KUNUFAIKA NA RASILIMALI MADINI


Leo tarehe 27 Januari, 2025 Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limetoa darasa la ushiriki wa Serikali katika kusimamia uvunaji wa rasilimali madini kwa manufaa ya Umma kwa ujumbe kutoka Shirika la Madini la Uganda (Uganda National Mining Company). STAMICO imetumia nafasi kuelezea namna inavyofanya kazi katika kusimamia miradi yake.

Akitoa uzoefu wa kuendesha miradi Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO CPA Dr. Venance B. Mwasse amesema STAMICO imekuwa lango kuu la maendeleo ya uchumi utokanao na madini huku akieleza umuhimu kwa Serikali na Shirika kuwekeza katika kuvuna rasilimali madini ili kuwavutia wawekezaji.

Ameongeza kuwa ili kuweza kufikia malengo ni lazima taasisi iweze kujiendesha kibiashara kama taasisi binafsi katika masuala ya uwajibikaji, utendaji na mifumo.

Akitoa wasilisho Mjiolojia Bw. Alex Rutagwelela ametoa sababu ambazo STAMICO imejiwekea katika kuwavutia wawekezaji katika madini ikiwemo uzoefu wa miaka mingi kufanya shughuli za madini nchini na mifumo imara ya kushirikisha wadau.

Licha ya mafanikio ambayo Shirika imeyafikia kuna baadhi ya changamoto ambazo zimekuwa zikilikumba Shirika kwa vipindi tofauti tangu kuanzishwa kwake zikiwemo mabadiliko ya bei za soko la dunia, mabadiliko ya teknolojia, mabadiliko ya kimifumo na ujuzi.

Naye Bw. Mukasa James Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Madini Uganda ameishukuru STAMICO kwa ushirikiano walioutoa katika kuhakikisha ujumbe huo unapata taarifa zenye tija kwa maendeleo ya mamlaka hiyo na kuwanufaisha wananchi huku akipongeza kwa hatua ambayo Shirika limepiga kwa kipindi kifupi.

Katika miaka ya hivi karibuni STAMICO imeendelea kupokea wageni wanaokuja kujionea na kujifunza jinsi Shirika linavyoshiriki kusimamia na kuvuna rasilimali katika sekta ya madini kwa manufaa ya Taifa.