*MAKAA YA KIWIRA SASA KUTIA FORA KWA UBORA*
- STAMICO NA WABIA WAKE WALETA TEKNOLOJIA YA KWANZA TZ NA UKANDA WA EA
- MD STAMICO AWAALIKA WADAU KUJA KUSHUHUDIA NA KUNUFAIKA NAYO
- MWAROBAINI UBORA WA MAKAA KWA VIWANDA VYA SIMENTI TZ WAPATIKANA
Kiwira, Songwe 07/12/2025
Shirika la Madini la Taifa ( STAMICO) limeendelea kuboresha shughuli za Uchimbaji kwa kufunga na kuanza kutumia mitambo ya kisasa ambayo ni ya kwanza kutumika Tanzania na katika ukanda wote Afrika Mashariki. Mitambo hiyo inajumuisha mmoja unaotumia Umeme (Intelligent Dry Sorting Machine) kutenganisha makaa ya kiwango bora na uchafu na unaotumia maji ( Water Washing Plant wenye uwezo wa kutenganisha Makaa yenye ubora na uchafu.
Akiongea katika ziara ya kukagua mitambo hii baada ya kuanza kutumika, Dkt Venance Mwasse, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO,
alisema teknolojia hii inaenda kutatua tatizo la ubora wa makaa. Pia aliendelea kuelezea kwamba mtambo unaotumia umeme ( Intelligent Dry Sorting Machine) una uwezo wa kuchambua Makaa ya Mawe yenye ukubwa wa milimita 50-100 na ule unaotumia maji (Washing Plant) una uwezo wa kuondoa takataka ( impurities) na kupata Makaa yenye ubora kuanzia ukubwa wa milimita 0-50.
Dkt. Mwasse alielezea uwekezaji huu utaongeza kiwango ambacho STAMICO inachimba na kuuza kitu ambacho kitasaidia kuongeza mapato ya Shirika lakini kuchangia kwa ukubwa kwenye pato la taifa. Katika ziara hiyo Dkt Mwasse aliambatana na Mha Baraka Manayma, Kaimu Mkurugenzi wa Migodi na huduma za kihandisi na Bwn Deus Alex, Meneja wa Masoko na Mahusiano ya Umma.
Naye Bw. Aron ambaye ni Mwakilishi wa Kampuni ya Yunda ambayo ndio imeshirikiana na STAMICO kuleta mitambo hii ya kisasa alisema " Mtambo huu wa umeme una uwezo wa kuchambua tani 100 za makaa yaliyochimbwa kwa saa na kubaki na tani zaidi ya 80 zenye ubora mkubwa. Kwa upande wa mtambo unaotumia maji alisema una uwezo wa kusafisha na kutoa takataka zote( impurities) na kubaki makaa yenye ubora mkubwa".
Dkt Mwasse alimalizia kwa kuwakaribisha wateja wote wanaohitaji Makaa ya Mawe yanayochimbwa katika Mgodi wa Kiwira kwa sababu ya ubora ambao upo nao.
Katika muendelezo wa ziara hiyo, Dkt Mwasse alitembelea shule ya msingi ya Kapeta ambayo Shirika limejenga madarasa matatu kupitia mpango wake wa kusaidia jamii inayozunguka maeneo yenye miradi yake. Madarasa hayo yana uwezo wa kuchukua watoto 45-50. Madarasa hayo yapo kwenye hatua ya kuezekwa na Dkt Mwasse ametoa maelekezo ya kazi kuisha mwezi huu wa 12 ili watoto wanaporudi shule waweze kutumia madarasa hayo.
Bwn Sayuni Cheyo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kapeta pamoja na Bwn Optatus Wangu, Mtendaji wa Kijji cha Kapeta waliishukuru STAMICO kwa kujenga madarasa haya ambayo yataiwezesha shule hiyo kuwa na uwezo wa kuchukua watoto 250 na pia kuwa sasa na uwezo wa kuwa na wanafunzi kuanzia darasa la kwanza mpaka darasa la saba. Kwa sasa shule hiyo ina wanafunzi takribani 180.
Shirika linaendelea kuboresha huduma zake na kuhakikisha inafikisha bidhaa zenye ubora katika soko. Sambamba na hilo Shirika linaendelea na jitihada za kuhakikisha linaendelea kujiendesha kwa ufanisi mkubwa.