REA YARIDHISHWA NA UZALISHAJI WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA YA RAFIKI BRIQUETTES INAYOZALISHWA NA STAMICO
Bodi ya Wakurugenzi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeridhishwa na hatua zinazofanywa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) katika kuhakikisha upatikanaji wa Nishati safi ya kupikia ya Rafiki Briquettes pamoja na kuendeleza kuboresha ubora wa Nishati hii. Sambamba na hao imeridhishwa na kasi ya kuongeza idadi ya Viwanda vyake kufikia vinne ambapo viwili vya Kisarawe na Kiwira vikiwa vinafanya kazi kwa uwezo wa kuzalisha tani 20 kwa saa, huku kingine cha Tabora kikiwa katika hatua ya uzinduzi hivi karibuni na cha Dodoma kikiwa katika hatua ya usimikaji wa mitambo.
Akiongea katika ukaguzi wa Kiwanda cha kuzalisha Nishati safi ya kupikia ya Rafiki Briquettes cha Kisarawe leo tarehe 24 Januari, 2026,Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa REA, Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu, amesema, yeye pamoja na wajumbe wake walioambatana katika ziara hiyo wamefurahishwa kuona jinsi STAMICO walivyopiga hatua ya kujenga Viwanda vya kuzalisha Nishati safi yakupikia ya Rafiki Briquettes ambayo ni mbadala wa matumizi ya Nishati ambazo sio safi kama vile kuni na mkaa. Ameongeza kwa kusema kuwa, wamefarijika kuona mfumo mzima wa uandaaji wa Nishati hii na hatua ambazo STAMICO imekuwa ikizichukua kuendela kuboresha Nishati hii. Katika ziara hiyo, ujumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa REA uliambatana na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mha. Hassan Said.
Kwa upande wake Mha. Hassan ameitaka STAMICO kuangalia jinsi ya kuwafikia Wananchi wengi kwa kuangalia wanavyoweza kushirikiana na Taasisi nyingine za binafsi ili kutekeleza kwa vitendo lengo kuu la kufikisha Nishati hii Nchi nzima. Aidha alisema ili kufanikisha adhma ya kufikisha Nishati safi Nchi nzima, STAMICO haina budi kuangalia jinsi ya kushirikiana na Taasisi nyingine binafsi ambazo zinaweza kusaidia kusambaza Nishati hii kwa kasi. Aliongeza kuwa, REA ipo tayari kutoa Ruzuku kwa Taasisi ambazo zinatengeneza majiko banifu ili Wananchi wengi waweze kuyanunua na kuweza kutumia Nishati ya Rafiki Briquettes kwa ufanisi.
Alisema tayari REA wameshawapa STAMICO ufadhili kwa ajili ya Kiwanda cha Geita na sasa wapo tayari kutoa ufadhili kwa Kiwanda kingine cha Tanga.
Awali akiwasilisha taarifa ya mradi huu, Kaimu Mkurugenzi wa STAMICO, Mha. Baraka Manyama aliwaeleza mipango ya Shirika ni kuhakikisha Nishati hii inasambaa Nchi nzima. Mha. Manyama alisema kuwa, STAMICO inaendesha Viwanda viwili vikubwa vya Kisarawe na Kiwira na sasa Shirika lipo mbioni kuzindua Viwanda viwili vya Tabora na Dodoma ambavyo vinatarajiwa kuanza uzalisha Mwezi Februari Mwaka 2026.
Pia ameongeza kuwa, ujenzi wa mitambo ya Kiwanda cha Geita umefikia asilimia 50 wakati taratibu za kumpata Mkandarasi wa ujenzi wa Kiwanda zikiendelea. Kwa upande wa Masoko, Mha. Manyama aliwaeleza kwamba tayari Taasisi kama Magereza yote 129, kambi za JWTZ, JKT, Taasisi za Elimu kwa maana ya Shule na Vyuo, Taasisi kama Hospitali, pia Masoko ya nyama choma, masoko ya Feri ya kukaanga Samaki pamoja na watu binafsi wanatumia Nishati ya Rafiki Briquettes.
Alisema Shirika limeshafanya majaribio ya kukausha mazao ya Chai na Tumbaku na yameenda vizuri. Tayari wakulima wa Tumbaku wa Tabora wameomba Nishati hii ipelekwe wanapoanza kuvuna zao hili mwishoni mwa Mwezi Januari. Sambamba na hao pia Kampuni kadhaa za Chai zimeshaanza kuagiza Nishati hii kwa ajili kukaushia.
Kwa upande wa Masoko ya Kimataifa, Mha. Manyama amesema tayari Shirika limeshafanya mawasiliano na kuwatembelea Jeshi la Magereza Uganda na wamepanga kuja kutembelea Kiwanda Mwezi wa Februari.
Baada ya mazungumzo na mawasilisho hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Wajumbe wa Bodi, Menejimenti na Watumishi wa REA, walionyeshwa ufanisi wa Rafiki Briquettes kwa kuonyeshwa jinsi inavyochoma nyama, kupika vyakula vigumu kama mahindi na maharage, kukaanga chips na kuchoma kuku pamoja na kuona mifumo ya majiko ambayo inaifanya Rafiki Briquettes iwe na ufanisi zaidi. Viongozi hawa na Watumishi wa REA walifurahia chakula ambacho kiliandaliwa kwa kutumia Rafiki Briquettes.
Mwenyekiti wa wa Bodi ya REA, Mhe. Kingu aliwashukuru STAMICO kwa makaribisho mazuri na kukiri kuwa Nishati hii ina nafasi nzuri ya kuwafikia watu wengi kutokana na gharama zake kuwa za kawaida. Alisisitiza STAMICO kuongeza kasi ya kuisambaza Nchi nzima.
STAMICO imejipanga kuendelea kuwa Kinara wa kuhakikisha inashiriki kikamilifu katika kuzalisha Nishati hii ya Rafiki Briquettes ili kufikia lengo la asilimia 80 ya matumizi ya Nishati safi ya kupikia ifikapo 2024.