STAMICO YASAINI MKATABA WA KUCHIMBA DHAHABU KATIKA LESENI ZAKE ZA KIGOSI NA KAMPUNI YA PLANTCOR YA AFRIKA KUSINI
Shirika la Madini la Taifa ( STAMICO ) limesaini Mkataba wa mashirikiano na Kampuni ya uchimbaji ya Plantcor ya Afrika Kusini kwa ajili ya uchimbaji wa Dhahabu katika leseni zake za Kigosi Wilayani Bukombe, Mkoani Geita.
Hafla hiyo ya utiaji saini imefanyika leo tarehe 24 Februari, 2026, ambapo imeshuhudiwa na Mhe. Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa Pamoja na Uongozi wa Mkoa wa Geita.
Akizungumza katika Hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse alieleza kuwa, Mkataba huo unalenga kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika uchimbaji wa Dhahabu katika leseni ya Kigosi.
Ameongeza kuwa ushirikiano huo utawezesha kufanyika kwa tafiti za anga ( Airborne Servey ) zitakazohusisha matumizi ya Ndege maalum kwa ajili ya uchunguzi wa Kijiolojia katika eneo lote la Kigosi, hatua itakayonufaisha wachimbaji wengi zaidi kwa kupata taarifa za Kijiolojia katika maeneo hayo.
Dkt. Mwasse ameongeza kuwa, mashirikiano haya yataleta neema ya Ajira na fursa za Biashara kwa wakazi wa Bukombe na maeneo ya jirani. Alisema Shirika pia litazingatia kutoa kipaumbele kwa wazawa katika fursa zote za Biashara na Ajira.
Naye Mgeni Rasmi Mhe. Dkt. Kiruswa Naibu Waziri wa Madini aliipongeza STAMICO kwa hatua hii ya kupata wawekezaji watakaosaidia kuchimba na kufanya utafiti katika leseni za Kigosi. Alitoa maelekezo kwa STAMICO kuhakikisha inatekeleza wajibu wake wa kurudisha kwa jamii ( CSR ) kwa kuhakikisha jamii inayozunguka maeneo ya Kigosi inaneemeka.
Alisisitiza pia, kuhakikisha uchimbaji unazingatia utunzwaji wa mazingira pia kuhakikisha wazawa wanapewa kipaumbele katika fursa za Ajira na Biashara zitakazotokana na mradi huo kupitia Sera ya Local Content.
Aidha Dkt. Kiruswa ameitaka Menejimenti ya STAMICO kushirikana kwa ukaribu na Plantcor ili kuhakikisha mradi unasimamiwa kwa weledi na uwazi na kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa. Vilevile amewataka wawekezaji hao kutimiza ahadi zote za uwekezaji, uhamishaji wa teknolojia na kuzingatia Sheria za Nchi ili mradi huo uwe mfano bora wa ubia kati ya Serikali na Sekta binafsi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO, Mhe. Balozi IGP Mstaafu Simon Sirro, amesema utiaji saini wa Mkataba huo ni ishara ya kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji Nchini akibainisha kuwa, ubia huo unatekelezwa kwa mujibu wa Sheria huku maslahi ya Wananchi yakilindwa kwa uwazi.
Naye Afisa Mtendaji wa Plantcor Mha. Josef Wilmans amesema, Kampuni hiyo ina uzoefu wa zaidi ya miongo miwili katika shughuli za Madini kuanzia utafiti, uchimbaji, uchenjuaji hadi usambazaji wa bidhaa Sokoni.
Amebainisha kuwa, Kampuni imeleta utaalamu wa kiteknolojia na kifedha utakaosaidia kuongeza uzalishaji na Ajira kwa Watanzania, huku akiishukuru Serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekwezaji na kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini.
Akiongea kwa upande wa Mkoa wa Geita, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martin Shigella aliahidi kuwa, Serikali ya Mkoa wa Geita ipo tayari kutoa ushirikiano kwa STAMICO na wabia wake kuhakikisha mradi huu unapata mafanikio.
Amesema kuwa, Mkoa wa Geita umebarikiwa kuwa na Rasilimali nyingi za Madini na akamshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kuufungua mradi wa Kigosi, hatua inayoendelea kuimarisha Uchumi wa Mkoa wa Geita.
Kwa upande wa Mhe. Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Dotto Mashaka Biteko ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu Mstaafu, ameipongeza STAMICO kwa kuimarisha ushirikiano huo na kuamua kusaini Mkataba huo. Amesema kuwa, Serikali ya awamu wa sita chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wachimbaji wa Madini, hali inayowezesha Wananchi kunufaika zaidi na Rasilimali za Taifa.
Dkt. Biteko amewataka Wananchi wa Bukombe kuchangamkia fursa zitokanazo na uwekezaji huo na kutoa ushirikiano kwa wawekezaji ili kuhakikisha mradi wa Kigosi unakuwa chachu ya Maendeleo endelevu kwa Wilaya, Mkoa na Taifa kwa ujumla.