Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

State Mining Corporation

State Mining Corporation

News

STAMICO KUANZA MRADI WA UZALISHAJI MADINI UJENZI


●Utazalisha tani 2000 kwa siku.

●Akiba ya malighafi ni tani milioni 13.1

● Awamu ya kwanza uzalishaji utafanyika kwa miaka 8

*Na.Samwel Mtuwa - Dodoma*

Shirika la Madini la Taifa ( STAMICO) linatarajia kuanza mradi wa uzalishaji wa madini ujenzi aina ya kokoto katika eneo la Chigongwe mkoani Dodoma ambapo unatarajia kuzalisha tani 150-200 kwa saa na tani 2000 kwa siku.

Hayo yamebainishwa leo januari 24, 2024 na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Deusdedith Magala katika ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilipotembelea mradi huo unaoendelea na usimikaji wa mitambo.

Magala amesema kuwa, utafiti umeonesha kuwepo kwa kiasi cha tani 13.1 cha akiba ya malighafi itakayovunwa kwa kipindi cha miaka nane kwa awamu ya kwanza katika leseni mbili kati ya kumi zilizopo.

Akielezea kuhusu mpango wa masoko amesema kuwa, uzalishaji utakapo anza asilimia ishirini imelengwa katika ujenzi wa makazi na asilimia themanini zitaenda katika miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa barabara, reli na viwanja vya ndege na michezo .

Kwa upande wake, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ameipongeza STAMICO kwa kuanza mradi huo wa kimkakati ambao utatatua changamoto ya kukosekana kwa madini ujenzi katika miradi ya maendeleo ndani na nje ya mji wa Dodoma.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. Dkt. David Mathayo (Mb) amelitaka Shirika la STAMICO kuongeza kasi katika ujenzi kwa kuzingatia vigezo husika vinavyotakiwa kuanzia usimikaji wa mitambo, ujenzi wa miundombinu pamoja na vigezo vya mazingira katika eneo lote la mradi.

Sambamba na hayo, Dkt. Mathayo ameipongeza STAMICO kwa kuweza kubuni mradi mkubwa wa maendeleo utakaosaidia upatikanaji wa malighafi za ujenzi aina ya kokoto.