Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

State Mining Corporation

State Mining Corporation

News

STAMICO YASHIRIKI MAADHIMISHO YA SIKU YA WAFANYAKAZI KIKAMILIFU


Wafanyakazi wa Shirika la Madini la Taifa leo Mei 01, 2022 wameungana na Wafanyakazi wengine Duniani kote kusheherekea sikukuu ya Wafanyakazi Duniani kwa kushiriki maandamano katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dodoma, Dar es Salaam na Songwe.


Akiongea kuhusu maadhimisho hayo Kaimu Mkurugenzi wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse amesema, STAMICO imeshiriki katika kuadhimisha siku hii ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango unaofanywa na Wafanyakazi wa Shirika hilo katika kuhakikisha miradi yake inaendelea kwa ufanisi.


Amesema siku hii ni muhimu na inaleta hamasa miongoni wa wafanyakazi kwa kuwa kuna baadhi ya watumishi wameibuka kuwa Wafanyakazi hodari katika idara zao hivyo kuwa chachu kwa wengine.Amewataka wafanyakazi wote kushikamana katika kufanya kazi kwa bidiii na uaminifu na ili kuleta tija kwa Shirika na miradi yake.


Naye Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala Bw. Deusdedith Magala amesema STAMICO inaendelea kuthamini mchango wa Wafanyakazi wake wote katika kuleta ubunifu na uthubutu jambo lililopelekea Shirika kufanikiwa sambamba na kuanza uzalishaji wa bidhaa mpya ya Mkaa mbadala wa kupikia ujulikanao kwa jina la Rafiki Briquette.

Amesema jitihada hizi zina maana kubwa katika kuleta ufanisi wa Shirika na hawana budi kupongezwa.

Kwa upande wa Wafanyakazi, Bw. Samwel Kibaranga ambaye ameibuka kuwa mfanyakazi Hodari wa Shirika ameishukuru STAMICO kwa kutambua mchango wa kazi wanazozifanya na kutoa zawadi ya Wafanyakazi Hodari na kwamba nafasi hiyo ameichukua kama chachu katika kujiboresha zaidi kiutendaji katika kipindi kijacho.


Amesema siri kuu ya ushindi wake ni kuwa na nidhamu, uthubutu, kufanya kazi kwa bidii na kujituma katika kutekeleza majukumu yake.
STAMICO imeendelea kuungana na Taasisi nyingine za Serikali kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ambapo kitaifa yamefanyika jijini Dodoma, Mgeni rasmi alikuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan.