Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

State Mining Corporation

State Mining Corporation

News

STAMICO YAWAPA MAFUNZO WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI KUHUSU UPATIKANAJI WA MITAJI YA KUWEZESHA SHUGHULI ZA UCHIMBAJI


Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BOT), limeandaa na kutoa mafunzo maalum kwa wachimbaji wadogo wa madini kuhusu *Mfuko wa Dhamana ya Mikopo* unaotolewa na Serikali kupitia BOT.

Mafunzo haya yametolewa kwa Wachimbaji Wadogo wa madini na wafanyabiashara wa madini (dealers na brokers) katika maeneo mbalimbali kwenye mikoa ya *Songwe, Singida, Mara, Mbeya, Shinyanga, Mwanza, na Geita.*

Lengo kuu la mafunzo haya ni kuwawezesha wachimbaji wadogo na wa kati kupata mitaji kupitia Taasisi mbalimbali za fedha ili kuendeleza shughuli za uchimbaji zinazofanywa na wachimbaji hawa kwa *Mfuko wa Dhamana ya Mikopo*

Katika kuwezesha wachimbaji kupata mikopo tayari STAMICO imeingia *Makubaliano ya Awali (MOU)* na Taasisi mbalimbali (Mabenki) kuwakopesha Wachimbaji Wadogo na Wa-Kati mitaji ya kuendeleza shughuli zao.

Katika mafunzo haya, STAMICO pia imeeleza fursa zilizopo za *mitambo ya uchorongaji (drill rigs)* maalum kwa wachimbaji wadogo. Mitambo hii inawawezesha wachimbaji kupata taarifa za kijiolojia na mashapo ya madini, kuongeza uhai wa migodi ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya shughuli za uchimbaji.

Hadi sasa, mitambo ya uchorongaji mitano inafanya kazi katika maeneo mbalimbali, na hivi karibuni mitambo mingine kumi itawasili na kusambazwa kwenye maeneo ya uchimbaji nchini. Hii ni kutekeleza maagizo ya *Dkt. Samia Suluhu Hassan*, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alipokuwa akizindua mitambo hii mwezi *Oktoba 2023 jijini Dodoma*.

Uwepo wa mitambo hii ya uchorongaji ni utekelezaji wa Maono ya Wizara ya Madini ya *Vision 2030 - "Madini ni Maisha na Utajiri"*, ambayo inalenga kuwezesha upatikanaji wa taarifa za kijiolojia za maeneo mbalimbali hapa nchini ili kukuza shughuli za uchimbaji wa madini, hivyo kuongeza mchango wake kwenye Pato la taifa.

Taasisi zilizoshiriki mafunzo haya ni pamoja na BOT, STAMICO, Tume ya Madini kupitia Ofisi za Mikoa na FEMATA kupitia Viongozi wa Vyama vya Wachimbaji wa Mikoa (REMAs).Zifuatazo ni baadhi ya Picha za Matukio.