Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

State Mining Corporation

State Mining Corporation

News

DKT.MWASSE ATETA NA WANAWAKE STAMICO


Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt.Venance Mwasse leo ameongea na watumishi wanawake kuhusu umuhimu na mchango wao kiutendaji katika kuendeleza miradi ya Shirika.

Ameyasema hayo wakati wa kikao chake cha pamoja kilichofanyika jijini Dar es Salaam na kuwataka watumishi hao kufanya kazi kwa bidii na uaminifu bila kujali nafasi zao ili kuweza kuleta matokeo chanya yatakayopelekea shirika kusonga mbele na kufikia malengo yake.

Ametumia kikao hicho kuwaasa wanawake kutofautisha ya mazingira ya kazini na nyumbani, kwa kujiwekea utaratibu wa kukamilisha kazi wanazopewa na kuziwasilisha kwa wakati wakiwa ofisini ili kuweza kuongeza umakini na kutoa kazi zenye ubora na tija.

"Tunatambua wanawake wana majukumu mengi wafikapo nyumbani, nawasihi kutumia vizuri muda wenu kumaliza kazi mnazopewa muwapo kazini ili kuepuka kulimbikiza kazi na kupata muda wa kufanya majukumu ya nyumbani kama mwanamke" alisisitiza Dkt. Mwasse

Mwasse amesema STAMICO itaendelea kubeba ajenda ya kumuwezesha na kumhamasisha mwanamke kimaendeleo kwa kuthamini nafasi yake ndani na nje ya shirika na kutengeneza mazingira rafiki ya kukua kitaaluma na kikazi.

Amefarijika kuona idadi ya wanawake katika uongozi imeongezeka na kuwataka viongozi wanawake hao kujitambua, kujitofauti sambamba na kuwajibika kikamilifu kwa kutumia rasilimali walizonazo bila woga zikiwemo rasilimali watu, fedha na vifaa katika kufikia malengo ya Shirika

Sambamba na hayo Dkt.Mwasse amewapongeza wanawake wa STAMICO kwa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya Shirika jambo linalofanya shirika kujivunia uwepo wa wanawake wakiweo wahandisi.

Kwa namna ya pekee amempongeza Mhandisi Mchenjuaji Happy Mbenyange ambaye hivi karibuni alipata tuzo ya Mwanawake Mashuhuri katika sekta ya Uziduaji na kusema tuzo hii inamaana kubwa kwa Shirika.

Naye Mkurugenzi Rasilimali Watu na utawala Bw. Deusdedith amewapongeza wanawake wote kwa Kuwa mstari wa mbele katika kushiriki katika kutekeleza majukumu kwa ufasaha.

Akiongea kwa niaba ya watumishi mha. Mbenyange ameushukru uongozi wa STAMICO ambao umekuwa chachu ya yeye kupata tuzo, kwa kutoa fursa, kumuamini na kumwezesha mwanamke kushika nafasi ya kusimamia miradi mbalimbali jambo linalowapa kujiamini.

Wakati huohuo STAMICO ilipokea ujumbe wa shukrani kutoka kwa wadau wa Azurite ambao waliandaa sherehe za kutambua jitihada za Wanawake katika sekta ya uziduaji kuelekea siku ya Wanawake Duniani 2024 iliyofanyika Machi Mosi, 2024.

Akitoa shukrani zake Bi. Christer Mhingo ameipongeza STAMICO kwa mstari wa mbele katika kushirikiana na wadau kuibeba ajenda ya kuwaendeleza Wanawake kupitia sekta ya madini jambo lilipelekea wepesi kusaidia kufanikisha sherehe hizo.