Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

State Mining Corporation

State Mining Corporation

News

MWENYEKITI NA MAKAMU MWENYEKITI WA BODI WATEMBELEA MGODI WA KUCHIMBA MAKAA YA MAWE KABULO KIWIRA


Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Meja Jenerali mstaafu Michael Isamuhyo

amefanya ziara katika mgodi wa Kiwira mapema mwezi Machi 2021, ili kuangalia na kukagua maendeleo ya mgodi huo ikiwa ni sehemu mojawapo ya kufuatilia utendaji kazi katika miradi ya Shirika.

Wakati wa ziara hiyo Meja Jenerali mstaafu Michael Isamuyo amefurahishwa na jitihada za watendaji wa STAMICO za kufanya kazi kwa uzalendo na kujituma katika kuhakikisha miradi yote inasonga mbele na kuwapongeza kwa hatua wanazozichukua katika kuendesha shughuli za uchimbaji makaa ya mawe ya Kabulo na kusimania mgodi wa Kiwira.

Amesema ni wakati sasa wa kuendelea kuchapa kazi na kuendeleza ukarabati katika maeneo mbalimbali ili kuleta mpangilio mzuri wa kazi na pia kushughulikia changamoto na mapendekezo yaliyotolewa wakati wa ziara hiyo.

Ameahidi kutoa ushirikiano kipindi chote cha uongozi wake na kuwataka wana STAMICO kuongeza ubunifu, uthubutu ili kuweza kufikia malengo.

“Nimefurahishwa sana na utendaji kazi wenu kwani nilikuja kwa kushtukiza bila taarifa yoyote lakini nimekuta kazi zinaendelea vizuri, hii inayoonesha uzalendo wenu katika mgodi huu. Sisi viongozi wenu wa Bodi tupo tayari kuifikisha STAMICO kwenye mafanikio”Alisisitiza Meja Jenerali Isamuyo .

Ziara hii imetoa fursa kwa uongozi wa Bodi pamoja na watendaji kutatua kwa pamoja changamoto zinazoukabili mradi huo na kutafuta njia ambayo itakayoleta tija katika kuongeza thamani ya makaa ya mawe.

Aidha, Makamu Mwenyekiti wa Bodi Mh. Lukas Selelii amesisitiza kuhusu kujitanua kibiashara kwa kuongeza masoko ya makaa ya mawe nje ya nchi, kuendeleza utafiti wa kijiolojia na kuzidisha ubunifu ili kufika mbali. Ameongeza kuwa kwa sasa Bodi ina imani na menejimenti na wafanyakazi wake hivyo itaendelea kutoa ushirikiano kuhakikisha inafikia malengo yake.

Kwa upande wa STAMICO Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Venance Mwasse amesema ziara hiyo imeleta hamasa kwa wana STAMICO na kuwaongeza ujasiri katika utendaji kazi, kutokana na ushirikiano wanaoupata kutoka kwa Bodi hiyo katika kutatua changamoto zinazohusiana na miradi mbalimbali.

Viongozi wa bodi ya STAMICO wamefanya ziara katika eneo la mgodi wa Kabulo, na kisha kuangalia sehemu ya mauzo ya mkaa na baadae kukagua eneo uchimbaji wa chini na mtambo wa makaa ya mawe uliopo Kiwira ili kujionea maendeleo ya mradi.