Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

State Mining Corporation

State Mining Corporation

News

STAMICO YA SHEHEREKEA SIKU YA WANAWAKE KITOFAUTI


Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) leo limeungana na watu wote duniani kusheherekea siku ya wanawake ikiwa na kauli mbiu ya kitaifa ya “Wanawake Katika Uongozi, Chachu Kufikia Dunia yenye Usawa” yenye lengo la kuhamasisha usawa na uwajibikaji hasa katika nafasi za uongozi.

Akiongea kwa niaba ya Mkurugezi Mtendaji wa STAMICO Bw. Deusdedith Magala amewapongeza wafanyakazi wanawake kwa jitihada wanazozifanya katika utendaji kazi kwani wamekuwa na mchango mkubwa sana katika Shirika bila kujali muundo wa kazi za sekta ya madini ambazo mara nyingi zinawafanya kuwa mbali na familia zao.

“Mmekuwa wafanyakazi Hodari mnaoweza kufanya kazi katika mazingira yoyote, ukizingatia kazi za madini zina changamoto sana, kwa kuwa nyingi hufanyika mbali na maeneo ya mjini jambo linalopelekea ninyi kukaa mbali na familia zenu. Nawapongeza sana endeleeni kuchapa kazi kwa bidii”

Katika kusheherekea sikukuu hiyo wafanyakazi wanaume wa STAMICO nao wameamua kushikilia kwa muda majukumu ambayo yanashikiliwa na wafanyakazi wanawake ili kuwaruhusu wanawake hawa kwenda kushiriki ipasavyo katika maadhimisha ya siku ya sherehe hiyo.

Akiongea kwa niaba ya wafanyakazi wanaume wa STAMICO, Afisa Masoko Mwandamizi Bw. Bilton Otto Alikuwa na haya ya kusema, “leo tumeamua kushikilia kwa muda majukumu yao ya ofisini ili kuwaunga mkono katika siku yao hii muhimu na kuleta hamasa ya usawa hapa ofisini.

Ni furaha kwetu kuona wanawake wanajitokeza kwa ujasiri kufanya kazi katika sekta ya madini”.

Aidha wafanyakazi wanawake wameushukuru na kufurahia ushirikiano wanaoupata kutoka kwa viongozi wa STAMICO jambo linalowarahisishia utendaji kazi na kuwafanya wasione utofauti katika maeneo ya kazi.

STAMICO imekuwa ikishiriki katika maadhimisho haya kila mwaka ili kuleta hamasa kwa wananchi kujiunga katika uchimbaji na biashara ya madini ili waweze kujikwamua kiuchumi.